RENE
MEULENSTEEN, aliekuwa Meneja wa Fulham ambayo iko mkiani kwenye Ligi
Kuu England, ameondolewa kwenye wadhifa huo na kupewa aliekuwa Kocha wa
zamani wa Bayern Munich Felix Magath.
Katika tamko la Fulham la kutangaza ujio
wa Felix Magath, haikusemwa lolote kuhusu hatima ya Meulensteen na
inaaminika Mkataba wake unaendelea.
Lakini mwenyewe Meulensteen, ambae
aliwahi kuwa Kocha wa Manchester United chini ya Sir Alex Ferguson na
ambae alimrithi Martin Jol aliefukuzwa Umeneja Mwezi Desemba na kushinda
Mechi 4 tu kati 17 alizosimamia, ameeleza: “Wameweweseka kwa
woga…lakini hii ni Soka. Najua Wamiliki wa Klabu walikuwa wakiogopa Timu
kushuka Daraja. Tulichojadiliana ni kuendelea kupigana lakini hatua hii
ni ya woga. Sijali nini wamesema kwenye tamko lao!”
Katka Taarifa yao iliyotolewa na Mmiliki
wa Fulham, Shahid Khan, Raia wa Marekani mwenye Asili ya Pakistan,
ilisema: “Zikiwa zimebaki Mechi 12, hakika hatuwezi kukubali kutopokea
Matokeo mazuri. Ilibidi hatua ichukuliwe!”
Katika Mechi zao mbili zilizopita za
Ligi, Fulham ilifanikiwa kupata Sare ya Bao 2-2 huko Old Trafford
walipofanikiwa kusawazisha katika Dakika ya mwisho walipocheza na
Manchester United lakini Juzi wakafungwa na Liverpool Bao 3-2 Uwanjani
kwao Craven Cottage kwa Bao la Penati ya Dakika ya 90.
Felix Magath, Miaka 60, amesaini Mkataba wa Miezi 18.
Magath ameshatwaa Ubingwa wa Bundesliga
mara 3 akiwa kama Meneja na mara ya mwisho ni Mwaka 2009 alipokuwa na
Wolfsburg na atakuwa Meneja wa kwanza kutoka Germany kuendesha Klabu ya
Ligi Kuu.
+++++++++++++++++++++++++++
Felix Magath
-Alitwaa Bundesliga mara 3 kama Mchezaji
akiichezea Hamburg, kati ya Miaka 1978 na 1983, wakicheza pamoja na
Nguli wa England, Kevin Keegan
-Mwaka 1983 alitwaa European Cup, akifunga Bao la ushindi dhidi ya Juventus
-Alianza kuwa Meneja Mwaka 1995 akiwa na Hamburg in 1995
-Alitwaa Ubingwa wa Bundesliga akiwa Meneja wa Bayern Munich Mwaka 2005 na 2006
-Alitwaa Ubingwa wa Bundesliga akiwa Meneja wa Wolfsburg Mwaka 2009
+++++++++++++++++++++++++++
Magath amekuwa hana kazi tangu aondoke
Wolfsburg Mwaka 2012 na miongoni mwa Kikosi chake cha Timu hiyo
kilichotwaa Bundesliga Mwaka 2009 wapo Wachezaji watatu ambao sasa wako
Ligi Kuu England ambao ni Edin Dzeko wa Man City na wawili ambao wapo
Fulham, Ashkan Dejagah na Sascha Riether.
Magath anatarajiwa kukutana na Wasaidizi
wa Meneja wa Fulham, Alan Curbishley na Ray Wilkins, kabla ya kuanza
kuitayarisha Fulham ambayo Mechi yao inayofuatia ni Ugenini hapo
Jumamosi Februari 22 watakapocheza na West Bromwich Albion ambao wako
Nafasi ya 17.
No comments:
Post a Comment