CHAMA cha
Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimefanikiwa kunasa siri za mipango ya
hujuma zilizokuwa zimeandaliwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika
uchaguzi mdogo wa udiwani katika kata nne za Jiji la Arusha, Tanzania
Daima Jumatano limebaini.
Habari
kutoka vyanzo mbalimbali vya kuaminika, zimebainisha kuwa CHADEMA katika
uchaguzi huo kilifanikiwa kushinda kata hizo baada ya kuvunja ngome ya
CCM iliyokuwa ikiongozwa na Naibu Katibu Mkuu wa CCM, Mwigulu Nchemba.
Kwa mujibu
wa habari hizo, mipango karibu yote iliyokuwa ikifanywa na CCM, ikiwemo
halali na haramu, ilivuja na kufika mikononi mwa wapinzani wao ndani ya
muda mfupi hata kabla ya utekelezaji.
Imedaiwa
kwamba baadhi ya watu waliokuwa katika kambi ya CCM, waliamua kwa siri
kufichua mipango hiyo na kuifikisha kwa mahasimu wao kutokana na kile
kilichodaiwa kuchoshwa kushiriki katika mambo ya kidhalimu.
Habari
zinasema maofisa kadhaa wa CCM ambao wamekuwa wakiratibu na kusimamia
mipango karibu yote miovu dhidi ya wapinzani, waliamua kwenda kinyume na
makubaliano hayo, na kwa njia ya siri wakafanikiwa kutoa mpango mzima
hadharani.
Mmoja wa
maofisa wa CHADEMA ambaye awali alikana taarifa hizo, kabla ya kukiri
baada ya kubanwa, amedai zilifikishwa kwao na watu wenye mapenzi mema na
nchi.
“Hata nasi awali tulishangaa, lakini tulilazimika kuziamini baada ya kuzifanyia kazi na kubaini kwamba zilikuwa za kweli.
“Kwa mfano
taarifa za kuwepo kwa mipango ya kutumbukiza kura bandia, kununua
shahada za kupigia kura ilivuja mapema nasi tukaamua kuweka mitego kila
mahali tulipoambiwa, kiasi cha kuwafanya washindwe kutimiza lengo lao,”
alisema ofisa huyo.
Habari
zimezidi kufichua kuwa, kambi hiyo ya CCM ilianza kuyeyuka mapema mchana
wa Jumapili, siku ambayo ilikuwa ya uchaguzi, baada ya kuhisi kuwa
mambo yao yamekwama kutokana na viongozi na vijana wao kuonekana katika
maeneo yote muhimu yaliyokuwa yamepangwa na chama hicho tawala kuendesha
hujuma zake.
Chanzo
kimoja cha habari cha kuaminika kimeliambia Tanzania Daima kuwa
‘usaliti’ huo wa baadhi ya watendaji wa chama hicho tawala umetokana na
kutopendezwa na mtindo wa utendaji kazi za kisiasa unavyoendeshwa na
Mwigulu na baadhi ya viongozi wa juu wa chama hicho tawala.
“Wameanza kuchoshwa na siasa za majitaka ambazo zimezidi kulichafua taifa na kuangamiza maisha ya watu.
“Ni kweli
tunataka ushindi, lakini wengi hawataki utokane na kuumiza watu ambao
wana haki ya kuunga mkono na kufuata chama wanachotaka,” kimesema chanzo
hicho, ambacho kimeomba jina lake lisitajwe kutokana na sababu za
kiusalama.
Mbali na
sababu hizo, taarifa zimebainisha kuwa sababu nyingine zilizowafikisha
baadhi ya watendaji wa CCM kusaliti, ni kasi ya CHADEMA kuungwa mkono na
wananchi, pamoja na vitisho, na vitendo vingi vya ukatili ambavyo
viongozi na wanachama wa chama hicho pinzani wamekumbana navyo.
Hadi sasa,
viongozi wakuu wote wa CHADEMA wameonja adha ya polisi kwa kukamatwa,
wengine kupigwa na hata kufikishwa mahakamani kwa tuhuma mbalimbali.
“Tunao
wanachama waaminifu ambao wamo ndani ya CCM na wamekuwa sehemu muhimu ya
intelijensia ya chama chetu,” alitoboa mmoja wa maofisa wa CHADEMA.
Katika
uchaguzi huo mdogo wa udiwani katika kata nne za Jimbo la Arusha ambao
ulifanyika Jumapili CHADEMA iliweza kushinda kata zote.
Awali
uchaguzi huo uliahirishwa mwezi uliopita kutokana na mlipuko wa bomu
katika mkutano wa kampeni za CHADEMA uliosababisha vifo vya watu wanne
na wengine zaidi ya 70 kujeruhiwa.
No comments:
Post a Comment