EBENEZA MARCH 9 2014

EBENEZA MARCH 9 2014

Tuesday, April 1, 2014

UINGEREZA SASA KUMWAGA MISAADA KWA TANZANIA

Rais Jakaya Kikwete akizungumza na Waziri Mkuu wa Uingereza  David Cameron alipomtembelea ofisini kwake mtaa wa 10 Downing jijini London kwa mazungumzo juzi. Picha ya Ikulu 


Dar es Salaam. Uingereza imeahidi kuendelea kuisaidia Tanzania katika kupambana na umaskini, ufisadi na kuimarisha utawala bora.
Ahadi hiyo imetolewa na Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameron wakati akizungumza ofisini kwake 10 Downing Street na Rais Jakaya Kikwete, ambaye yupo nchini humo kwa ziara ya siku tatu.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka Ikulu, Waziri Mkuu Cameron pia alijivunia nchi yake kwa kuongoza kwenye sekta ya uwekezaji nchini humu.
“Tunakaribia mwisho wa muda wa Malengo ya Milenia Mwaka 2015, tutahitaji kuweka vipaumbele vingine baada ya hivyo kama kuondoa umaskini, majisafi na salama, masuala ya ufisadi na utawala bora,” alikaririwa Cameron katika taarifa hiyo.
“Natumaini utaendelea kutoa mchango wako baada ya malengo hayo kufikia tamati,” alisema Waziri Mkuu Cameron, pia Rais Kikwete amekubali ombi hilo na kuahidi ushirikiano wake.
Akizungumzia kuhusu uwekezaji, Cameron ameahidi kuendelea kuisaidia Tanzania katika jitihada zake za kiuchumi na kuleta maendeleo.
Rais pia alipata fursa ya kufungua mkutano kuhusu uwekezaji, ambako aliitumia kuelezea nafasi za uwekezaji nchini Tanzania na vivutio mbalimbali vilivyopo.
“Fursa ni nyingi, amani, usalama, soko la kutosha na kubwa kwa vile Tanzania iko katika Umoja wa Afrika Mashariki, Ukanda wa Maziwa Makuu na Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (Sadc), hivyo kuwa na uhakika wa soko kubwa na pana,” alisema Rais Kikwete.
Rais pia amekutana na Watanzania waishio huko, na kufanya mazungumzo na Mstahiki Meya wa Jiji la London, Mama Alderman Fiona Woolf, ambaye ameahidi kutembelea Tanzania, Septemba mwaka huu.

No comments:

Post a Comment