Chama cha
Demokrasia na Maendeleo(Chadema) kimesema Msajili wa Vyama vya Siasa,
John Tendwa alibariki kuundwa kwa makundi ya vijana ndani ya chama
hicho, yanayoitwa ‘Red Brigade’.
Hatua hiyo
ya Chadema imekuja baada ya Tendwa kutishia kuifuta Chadema, iwapo
wataendelea na mpango wao wa kuanzisha kambi za mafunzo ya kujilinda kwa
vijana wake nchini.
Katika
taarifa yake, aliyoitoa kwa vyombo vya habari jana, na kusainiwa na
Naibu Msajili, Rajab Juma kwa niaba yake, Tendwa alieleza kushangazwa na
kusikitishwa na hatua hiyo ya Chadema kwa kuwa walishakatazwa mpango
huo tangu mwaka 2004.
“Msajili
anavikumbusha vyama vyote vya siasa hasa Chadema kuwa, kifungu cha 19
cha Sheria ya vyama vya siasa kinampa uwezo wa kufuta usajili wa chama
chochote kinachokiuka masharti ya usajili au kifungu chochote cha sheria
ya vyama vya siasa. Kifungu cha 20 cha sheria ya vyama vya siasa
kinasema uamuzi wa msajili ni wa mwisho na hauwezi kukatiwa rufaa
mahakamani,” alisema Msajili.
Hata hivyo,
Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Chadema ambaye pia ni Mbunge wa Ubungo,
John Mnyika alisema: “Tendwa alikuwepo kwenye mkutano wa Chadema wa
Agosti 13, 2006 uliopitisha katiba mpya ya chama hicho.
“Katika katiba mpya tuliweka kifungu kinachosema, Chadema itakuwa na chombo cha kulinda
uongozi na mali za chama kikiitwa Red Brigade...Tendwa katika mkutano aliipongeza Chadema kwa mabadiliko hayo ya katiba.
“Katiba ya Chadema ilisajiliwa katika ofisi yake kwa mujibu wa sheria mwaka 2006 na kusema Chadema imekidhi matakwa yote,”
Kuhusu madai
ya Chadema kwamba CCM kina kambi ya namna hiyo, Tendwa alisema hayana
msingi, badala yake amekitaka kuwasilisha ushahidi katika taasisi husika
ikiwamo ofisi yake unaoonyesha kambi za mafunzo za vijana wa CCM, ili
suala hilo liweze kushughulikiwa kisheria.
“Kwa kuwa
hivi sasa sheria zinakataza suala hili, hazijabadilika na viongozi wa
Chadema ni walewale waliositisha kutekeleza mpango huo mwaka 2004,
haieleweki nia yao sasa ni nini.
Kama ni kupima matokeo iwapo watatekeleza mpango huo, utakuwa si uamuzi wa busara kwa uhai wa chama chao,’’ alisisitiza msajili.
Alisema kuwa
mwaka huo 2004 hata Chama cha Wananchi(CUF)kupitia kwa aliyekuwa Katibu
Mkuu wa chama hicho, Wilfred Lwakatare kiliwahi kuomba ufafanuzi kwa
msajili kuhusu nia yao ya kutaka kuanzisha mafunzo ya ukakamavu wa
kujilinda kwa vijana wake kila wilaya, ambapo walikataliwa kwa kuwa ni
kinyume cha sheria.
Msajili
pia alitumia fursa hiyo kuviasa vyama vyote vya siasa kutumia muda wao
kufanya shughuli za siasa,ili kuchangia maendeleo ya nchi, badala ya
kutumia uwezo wao na muda kubuni mambo yanayoleta mtafaruku na
kuhatarisha amani na utulivu nchini.
No comments:
Post a Comment