RAIS wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete ametoa changamoto kwa
uongozi mpya wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kusukuma
mbele zaidi gurudumu la maendeleo ya mchezo huo nchini. Ametoa
changamoto hiyo katika barua yake kwa Rais mstaafu wa TFF, Leodegar
Tenga na kumtaka asichoke kutoa ushauri na uzoefu wake kila
utakapohitajika katika shughuli mbalimbali zinazohusu maendeleo ya mpira
wa miguu Tanzania. Rais Kikwete ametoa changamoto hiyo wakati akijibu
barua ya Tenga iliyokuwa ikimuarifu kuhusu kumaliza kipindi chao cha
uongozi, na kumshukuru yeye binafsi (Rais Kikwete) na Serikali
anayoiongoza kwa mchango waliotoa katika kuendeleza mpira wa miguu
nchini. “Pongezi zako zimetupa moyo na ari ya kuongeza maradufu juhudi
zetu za kuboresha kiwango cha ubora wa mchezo wa mpira wa miguu
nchini. “Kwa niaba ya Serikali napenda kuchukua nafasi hii kutoa pongezi
za dhati kwako wewe na uongozi wote uliopita wa TFF kwa mchango wenu
muhimu mlioutoa wa kuendeleza mpira wa miguu nchini. “Mafanikio ya kutia
moyo yamepatikana chini ya uongozi wako,” amesema Rais Kikwete katika
barua yake hiyo na kumtakia kila la heri Tenga katika shughuli
zake. Hata hivyo, ameongeza kuwa Tanzania bado haijafika pale ambapo
inapataka, lakini dalili njema zimeanza kuonekana, hivyo kinachotakiwa
sasa ni uongozi mpya kusukuma mbele zaidi gurudumu la kuendeleza mpira
wa miguu nchini. Tenga ambaye hivi sasa ni mjumbe wa Kamati ya Utendaji
ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) na Mwenyekiti wa Baraza la
Vyama vya Mpira wa Miguu Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) aliiongoza
TFF kwa vipindi viwili kuanzia Desemba 2004 hadi Oktoba 2013.
HAPATOSHI LIGI YA MABINGWA BARANI ULAYA.
WAKATI hatua ya makundi
ya michuano ya Ligi ya Mabingwa barani Ulaya ikielekea mwishoni wiki hii
timu kadhaa zitaungana na Manchester United, Real Madrid, Paris
Saint-Germain, Bayern Munich, Manchester City, Chelsea, Atletico Madrid
na Barcelona katika hatua ya timu 16 bora. Timu zilizopo kundi A na D
zitacheza mechi zake za mwisho kesho wakati makundi mengine yaliyobakia
yatacheza mechi zao Jumatatu huku timu kadhaa zikihitaji ushindi ili
kusonga mbele katika michuano hiyo. Katika kundi A Shakhtar Donetsk
wanaweza kukata tiketi ya kusonga mbele kama wakifanikiwa kuifunga
Manchester United ugenini wakati sare inaweza pia kuwavusha kama Bayer
Leverkusen ikishindwa kuifunga Real Sociedad. Kwa upande wa kundi D
Juventus itajihakikishia kuendelea kuwepo katika michuano hiyo kama
wakishinda au kutoa sare dhidi ya Galatasaray jijini Instabul wakati kwa
upande mwingine Galatasaray watasonga mbele kama wakifanikiwa kuchukua
alama zote tatu kutoka Juventus.
DROGBA, EBOUE MATATANI KWA KUONYESHA FULANA KUMKUMBUKA NELSON MANDELA.
KAMATI ya nidhamu ya
Shirikisho la Soka la Uturuki-TFF linatarajia kuwahoji nyota wawili wa
kimataifa wa Ivory Coast wanaocheza klabu ya Galatasaray, Didier Drogba
ba Emmanuel Eboue kufuatia kuonyesha ishara katika mechi ya kumkumbuka
rais wa zamani wa Afrika Kusini Nelson Mandela aliyefariki dunia
Alhamisi. Baada ya Galatasaray kushinda mabao 2-0 dhidi ya SB Elagizspor
katika mchezo wa Kombe la Ligi Ijumaa, nyota hao wawili walivua fulana
zao na kubakia na vesti zilizokuwa na ujumbe kuhusu Mandela. Mara baada
ya Drgba kuvua fulana yake vesti aliyokuwa amevaa ndani ilikuwa na
maandishi yaliyosema “Thank you Madiba” akimaanisha asante Madiba wakati
vesti ya Eboue ilikuwa na maandishi yaliyosomeka “Rest in Peace Nelson
Mandela” akimaanisha pumzika kwa amani Nelson Mandela. TFF linakataza
kuonyesha fulana yoyote yenye ujumbe unaohusiana na mambo ya siasa
wakari wa mechi ya soka.
WENGER ALIKATAA BAO LA KUSAWAZISHA LA EVERTON.
MENEJA wa klabu ya
Arsenal, Arsene Wenger ameonyesha kutofurahishwa na bao la kusawazisha
la Everton baada ya timu hiyo kushindwa kukaa kileleni kwa tofauti ya
alama saba kwenye msimamo wa Ligi Kuu nchini Uingereza. Bao la
kusawazisha la Everton lililofungwa na Gerard Deulofeu katika dakika ya
84 liliifanya Everton kuchukua alama muhimu katika Uwanja wa Emirates
baada ya pia ya kuwafunga Manchester United katikati ya wiki. Lakini
Wenger ambaye pia hakufurahishwa na mchezo wa nguvu waliokuwa wakicheza
Everton alisikitishwa na bao hilo kuruhusiwa baada ya kuonekana kuwa
Romelo Lukaku alikuwa amezidi wakati akitengeneza nafasi ya kufunga bao
hilo. Mbali na Lukaku kuzidi Wenger anaamini kuwa nyota huyo wa
kimataifa wa Ubelgiji pia alicheza faulo kwa beki wake Laurent
Koscielny.
VURUGU BRAZIL, HELIKOPTA YATUA UWANJANI KUOKOA MAJERUHI.
MICHUANO ya Kombe la
Dunia 2014 itakayofanyika nchini Brazil imeingia doa baada ya mashabiki
watatu kuumizwa vibaya katika vurugu zilizotokea katika mchezo wa ligi
ya nchi hiyo. Polisi wamedai kuwa mashabiki wa timu za Atletico Paraense
na Vasco da Gama walikuwa wakipigana huku wakikimbia katika majukwaa
katika Uwanja wa Catarina mara baada ya Atletico kufunga bao la kuongoza
dakika ya 17 ya mchezo.
Helikopta ya polisi
ililazimika kutua uwanjani ili kumaliza vurugu hizo na kusaidia majeruhi
kuwapeleka hospitali. Mchezo huo ulisimamishwa kwa saa moja kabla ya
kuanza tena.
RATIBA YA KOMBE LA FA HADHARANI.
KLABU ya Arsenal
imepangwa kucheza na wapinzani wao kutoka London ya Kaskazini, Tottenham
Hotspurs katika mzunguko wa tatu wa michuano ya Kombe la FA. Kwa upande
mwingine Manchester City wao watasafiri kuifuata Blackburn Rovers,
Chelsea watakuwa ugenini kukwaana na Derby County wakati Manchester
United wao watakuwa wenyeji wa Swansea. Mabingwa watetezi wa kombe hilo
Wigan Athletic wataanza kampeni zao kwa kuikaribisha Milton Keynes Dons
huku Liverpool wakimenyana wababe wao waliowafunga mabao 3-2 msimu
uliopita timu ya Oldham au Mansfield. Mechi zingine za mzunguko huo
zitakuwa kati ya West Bromwich dhidi ya Crystal Palace, Newcastle United
dhidi Cardiff City na Norwich dhidi ya Fulham.
No comments:
Post a Comment