EBENEZA MARCH 9 2014

EBENEZA MARCH 9 2014

Monday, December 9, 2013

MJUE MANDELA NA MICHEZO


MANDELA AKIWA NA TIMU YA OLIMPIKI YA TANZANIA MWAKA 2000 MJINI SYDNEY, AUSTRALIA
“Jela si kuwa inachukua uhuru wako pekee, badala yake inachukua hata utambulisho wako wa wewe ni nani kwa kuwa kila mmoja anavaa sare, anakula chakula sawa na wengine na anafuata ratiba zilezile.

“Kwa kifupi ni wizi wa uhuru wa mhusika na kama mpigania uhuru na mwanaume wa shoka, kikubwa ni kupambana kwa nguvu zote na hali hiyo ambayo inaua au kupoteza muonekano wa uwezo wa watu husika.”
Maneno hayo yako mwanzo kabisa kinapoanza kitabu cha Long Walk To Freedom Volume 2 cha Nelson Mandela ambacho nilikinunua Mei 24, 2003 kwenye nyumba ya makumbusho ya Mandela iliyoko katika Mtaa wa Villakazi, Soweto jijini Johannesburg.
Ni miaka kumi na ushee sasa tangu wakati huo, tukiwa na watu wengine wachache tulipata kuonyeshwa vyombo, nguo, viatu na vitu vingine alivyokuwa akivitumia Mandela wakati akiishi katika nyumba hiyo na mkewe, Winnie Mandela.
Baadaye tukatembezwa kwenye nyumba ambayo alihamia Mandela na ile aliyokuwa akiishi mkewe wa zamani, Winnie Mandela. Pamoja na mengi makubwa aliyofanya Mandela, kwangu kilichonivutia zaidi kwake ni namna alivyoshiriki michezo.
Huenda wengi wameelezea, lakini ukiangalia picha zake zilizokuwa katika nyumba hiyo ya makumbusho zinaonyesha alikuwa ni mwanamichezo wa kweli, kwani si ngumi tu, mchezo uliojulikana kuwa kipenzi chake, lakini soka na kikapu pia alishiriki.
Kwangu naamini wanaoshiriki michezo wanaaminika kuwa binadamu wenye maamuzi ya haraka zaidi kuliko wengine, angalia mpira wa kikapu, soka na hata ngumi namna mtu mmoja ambavyo huamua vitu vingi kwa wakati mmoja kwa kuwa muda ni mchache na mambo mengi hutakiwa kufanyika katika kipindi kifupi.
Kwa Mandela hakuwa Mzungu, inaonekana imekuwa ni vigumu kwa Wazungu kutamka kuwa ndiye binadamu maarufu zaidi kuliko wengine wote duniani katika kipindi hiki.
Kifo chake, bado kinamfanya awe mwanasiasa maarufu zaidi kuliko wengine wote duniani, hasa aliyeshiriki katika kupigania uhuru wa nchi fulani kwa muda mrefu zaidi na kusaidia kuiokoa nchi.
Baada ya kuwa rais mweusi wa kwanza wa Afrika Kusini, Mandela amekuwa ndiye kiongozi mwanasiasa maarufu zaidi na kipenzi cha wanamichezo kuliko wengine wote duniani.

Makocha maarufu, akiwemo Alex Ferguson, amewahi kueleza namna alivyofurahishwa na maisha au ushujaa wa Mandela, alimtembelea na kuonyesha furaha yake kwake wakati Manchester United ilipokuwa Afrika Kusini kwa mechi za kirafiki.
Tanzania:
Kuna mengi yanayoonyesha kuwa Mandela alikuwa na urafiki mkubwa na Tanzania, kwani hata alipokamatwa Agosti 5, 1962 na baadaye kuhukumiwa gerezani, inaelezwa alikuwa anatokea hapa nchini.
Lakini kwenye kitabu chake cha Long Walk To Freedom, kuna maneno kadhaa ya Kiswahili yaliyotumika, ikionyesha wazi namna alivyokuwa na mapenzi na nchi hii.
Moja ya picha kwenye kurasa hizi zinamuonyesha akiwa na timu ya taifa ya Olimpiki ya Tanzania ambayo alipiga nayo picha mwaka 2000.


Kiswahili:
Pamoja na kutumia Lugha ya Kiswahili katika sehemu mbalimbali, Mandela amewahi kuonyesha ujuzi wake wa kuzungumza lugha hiyo alipokutana na timu ya Olimpiki ya Tanzania ambayo awali aliifananisha na Jamaica.
Daktari Mwanandi Juma Mwankemwa, ambaye sasa ni daktari wa Azam FC, aliyekuwa kwenye timu hiyo, anasimulia namna Mandela alivyozungumza nao kwa Lugha ya Kiswahili:
“Ilikuwa mwaka 2000 katika Michezo ya Olimpiki kule Sydney, Australia. Siku hiyo Mandela alikuwa anapewa digrii ya heshima katika chuo kimoja katika mji huo. Sisi tulikuwa kati ya wanamichezo tulioteuliwa kupanga mstari kumsalimia.
“Alipotoka baada ya kuona ‘trak suti’ zetu, akatuuliza kama sisi ni timu ya taifa ya Jamaica, tulipomuambia ni Tanzania, akaonyesha kufurahi sana, mara moja akabadili lugha na kuanza kuzungumza Kiswahili akisema maneno haya, namnukuu.
“Watanzania rafiki zangu, wiki iliyopita nilikuwa Arusha na rais wenu Mkapa, tulikuwa na mkutano. Hamjambo kabisa ndugu zangu, sogeeni tupige picha.
“Baada ya hapo tulipiga naye picha tukiwa kati ya watu wachache tuliopata nafasi hiyo ya upendeleo ambayo aliitoa yeye binafsi. Leo ninaona kweli ilikuwa bahati kwangu na wenzangu kama Selemani Nyambui na marehemu Erasto Zambia kwa kuwa tulipata picha na Mandela,” anasema Mwankemwa.
Ngumi:
Katika kitabu chake cha Long Walk To Freedom, Mandela anaelezea namna ambavyo hakuwa na mapenzi na mchezo wa ngumi, hasa lilipofikia suala la kuumizana.
Anasema pamoja na wengi kuamini alikuwa akiupenda sana, lakini yeye alivutiwa na baadhi tu ya sehemu kama namna mtu anavyojipanga kujilinda na anavyocheza ulingoni kumhadaa adui.
Hata baada ya kuingia kwenye siasa rasmi na kuamua kupambana kwa ajili ya uhuru wa Afrika Kusini, Mandela hakutaka kuendelea na mchezo huo kabisa, ndiyo maana hakufika mbali pamoja na kudaiwa alikuwa na kipaji cha juu katika mchezo huo. Imekuwa ikielezwa, alipenda soka zaidi.
Liverpool:
Mandela alikuwa ni shabiki mkubwa wa Liverpool, mtu wa kwanza kutangaza hilo alikuwa ni John Barnes, winga wa zamani mwenye kasi wa timu hiyo kigogo England.
Mwaka 1994 akiwa tayari rais wa kwanza mweusi wa Afrika Kusini, Liverpool ilitembelea nchini humo na Mandela akapata nafasi ya kukutana na wachezaji wa kikosi hicho, Barnes akamkabidhi jezi, naye akaivaa.
Baadaye alipata nafasi ya kuzungumza naye kwa saa tatu na mwisho Mandela alimtamkia kwamba yeye ni shabiki wa Liverpool.
Katika mahojiano na FA mwaka 2003, Barnes alisema: “Tangu nikiwa mtoto, sikuwa na tabia ya kutaka kupata sahihi za wachezaji maarufu kama wenzangu walivyokuwa wakifanya. Lakini ilikuwa tofauti nilipokutana na Mandela, sikujivunga hata kidogo.
“Hata kidogo wala siwezi kuona haya kusema kuwa nimetundika ukutani nyumbani kwangu, picha niliyopiga na Mandela kipindi hicho.”
Baada ya Barnes kueleza kuwa Mandela ni shabiki wa Liverpool, picha yake akiwa na jezi ya Liverpool iliwekwa kwenye mtandao wa “105 celebrity fans". Baada ya hapo watu kibao wali-like na kati yao walikuwemo nyota kadhaa wa Marekani na wengine kama Dr Dre, Pope John Paul II, Samuel L. Jackson, Halle Berry, Elvis Costello na Michael Schumacher.
Sahihi yake:
Mandela ndiye binadamu pekee ambaye wanamichezo wengi nyota duniani walitaka kupata sahihi yake kama kumbukumbu.
Mara nyingi mashabiki wa michezo mbalimbali wamekuwa wakililia kupata sahihi za mastaa wa timu katika michezo wanayoihusudu, lakini mambo yalikuwa tofauti kwa Mandela.
Nyota lukuki kama David Beckham, Rio Ferdnand, Tiger Woods, Robinho, Adebayor, Cristiano Ronaldo na wengine wengi walimuomba kiongozi huyo awasainie kwenye kofia, fulana au jezi walizokuwa nazo.
Maana yake, katika michezo saini maarufu zaidi na iliyokuwa ikitafutwa zaidi ni ya Mandela kwa kuwa hata ambao saini zao zimekuwa zikitafutwa kwa juhudi kubwa, nao wamekuwa wakiitafuta yake kwa udi na uvumba.
Ukaribu:
Mandela ndiye kiongozi mkubwa na maarufu zaidi duniani aliyekaribisha au kuwatembelea wanamichezo wengi zaidi kuliko mwingine yeyote duniani.
Pamoja na kuwa na majukumu mengi, madaktari kumtaka apumzike muda mrefu lakini Mandela alikuwa akitembelea sehemu mbalimbali zilizowahusisha wanamichezo.
Aliwahi kuhudhuria fainali ya Kombe la Mataifa Afrika mwaka 1996 wakati Afrika Kusini ilipolibeba kwa kuichapa Tunisia. Aliwahi pia kuhudhuria mechi ya Liverpool aliyokuwa akiishangilia, vilevile Arsenal na alikaribishwa na nahodha Tony Adams.
Ukiachana na hivyo, pamoja na kuwa na umri wa zaidi ya miaka 85, aliendelea kutembelewa na wanamichezo mbalimbali ambao walitamani kumuona kila walipofika Afrika Kusini.
Pamoja na msisitizo wa madaktari kwamba alitakiwa kupumzika, mara zote alitoa ruhusa wanamichezo kumtembelea kila aliposikia walitaka kufanya hivyo.
Manchester United, Manchester City na timu ya taifa ya England wamewahi kumtembelea kiongozi huyo. Licha ya uzee kuwa kikwazo kwake kuzungumza nao akiwa na nguvu vizuri, lakini bado alifurahi kuwaona wakiwa pamoja naye.
Dawa:
Wakati fulani mmoja wa madaktari wa Mandela aliwahi kueleza michezo ilikuwa ni kama sehemu ya dawa ya kiongozi huyo kwa kuwa mara kadhaa alitaka kuangalia michezo mbalimbali, soka ukiwa wa kwanza, ngumi na kikapu.
Kingine ni kutembelewa na wanamichezo, kila ilipotokea akatembelewa na mchezaji, kocha au timu, baada ya kuondoka, Mandela alionekana ni mchangamfu sana.
Daktari huyo alieleza kuwa uchangamfu wake umekuwa ukiendelea hata angalau wiki nzima kila baada ya kupata ugeni wa wanamichezo, hali ambayo wao walipenda kumuona akiwa nayo.
Katika moja ya vitabu vyake vya Long Walk To Freedom, Mandela pia ameeleza namna alivyokuwa akiitumia michezo kama sehemu ya kutafuta nguvu mpya.
Ameelezea mazoezi yalivyokuwa yakimsaidia, lakini namna alivyoshiriki michezo kama sehemu ya kuupoza mwili wake na pilika za siasa.

No comments:

Post a Comment