EBENEZA MARCH 9 2014

EBENEZA MARCH 9 2014

Tuesday, February 25, 2014

MGIRIKI AKAMATWA UWANJA WA NDEGE WA MWL:NYERERE NA KILO 5.3 ZA MADAWA YA KULEVYA

Raia wa Ugiriki, Alexndrios Atanasios, aliyekuwa akisafiri kwa ndege ya shirika la Swiss Air kwenda nchini kwao kupitia Zurich, alipokaguliwa na Maofisa wa Usalama wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam na kutuhumiwa kukutwa na kilo 5.3 za dawa za kulevya.
Raia  wa Ugiriki, Alexandria Athanasios (30), amekamatwa kwa tuhuma za kukutwa na kilo 5.3 za dawa za kulevya aina ya heroine katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) jijini Dar es Salaam.

Meneja Usalama wa uwanja huo, Clemence Jingu, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kwamba raia huyo wa kigeni alikamatwa juzi saa 3:00 usiku uwanjani hapo.

Mkuu wa Kitengo cha Kupambana na Dawa za Kulevya nchini, Godfrey Nzowa, akifafanua zaidi tukio hilo alisema Athanasios alikamatwa wakati akijiandaa kusafiri na ndege ya shirika la Swiss Air kutoka Dar es Salaam kwenda Ugiriki kupitia Zurich.

Alisema mtu huyo alikamatwa na maofisa wa uwanja huo kwa kushirikiana na polisi wakati akikaguliwa mizigo yake.

Kamanda Nzowa alisema mtu huyo anaendelea kushikiliwa na polisi na kwamba uchunguzi wa kujua dawa hizo zina thamani gani unaendelea kufanyika na upepelezi ukikamilika atafikishwa mahakamani.

Kukamatwa kwa dawa hizo kumekuja wiki tatu ndani ya mwezi huu tangu raia 12 wa Pakistan na Iran walipokamatwa na shehena ya dawa za kulevya zaidi ya kilo 201 katikati ya Dar es Salaam na Zanzibar katika Bahari ya Hindi.

Kukamatwa kwa kiasi hicho kikubwa cha dawa kulizua taharuku kubwa katika Jiji la Dar es Salaam na kusababisha wananchi kulazimika kukimbilia katika Bandari ya Dar es Salaam kushuhudia tukio hilo.

Watu hao walikamatwa wakiwa katika jahazi ijulikanayo Aldanial iliyotokea nchini Iran mali ya Raisee, raia wa Iran.

Waliokamatwa katika tukio hilo ni Muhamad Hassan (30), Abdul Nabii (30), Fahir Muhamad (34) na Rahim Baksh (30), wote raia wa Pakistan.

Raia wa Iran waliokamatwa ni Abdulsamed Badreuse (47), Ayoub Hot (50), nahodha wa jahazi hilo, Hazra Azat (60), Nahim Mussa (35), Khalid Ally (35), Kher Muhamad (75), Said Muhamad (34) na Murad Gwaharam (38).

CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment