EBENEZA MARCH 9 2014

EBENEZA MARCH 9 2014

Tuesday, February 25, 2014

CHADEMA YASEMA OLE WAKE DAMU YA WANAKALENGA IMWAGIKE

Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Willibrod Slaa.
Katibu  Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Willibrod Slaa, ameapa kuwa chama chake hakitakuwa tayari kuona damu ya wakazi wa Kalenga inamwagika katika kampeni za uchaguzi mdogo wa jimbo hilo unaoendelea, huku baadhi ya wakazi wake wakibaki na ulemavu wa kudumu kwa lengo la kujibu mapigo ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Akizungumza katika uwanja wa Ifunda katika Jimbo la Kalenga, Dk. Slaa alisema Chadema hakitishiki na kauli iliyotolewa na CCM inayowataka wanachama wake kuacha unyonge na kujibu mapigo ya Chadema.

”Hatutaki na hatutakubali Grace Tendega (mgombea ubunge wa Chadema), aende bungeni Machi 18, mwaka huu huku nyuma akiwa ameacha vilema na baadhi ya wananchi wamefariki dunia kwa sababu tu CCM wameambiwa waache unyonge.


Nyie Polisi wa Iringa, hii ni fursa nyingine ambayo Mwenyezi Mungu amewaletea ili muwasaidie maskini wenzenu kupata kiongozi anayefaa na si kupendelea,” alisema Dk. Slaa.

Alisema licha ya ukarimu aliokuwa nao aliyekuwa Mbunge wa jimbo hilo, marehemu Dk. William Mgimwa, kuamua kuwasomesha watoto wa wananchi wasio na uwezo, lakini fadhila hizo haziwezi kugeuzwa fadhila ya kupeana madaraka ya kurithishana baba na mtoto kwa kuwa jambo hilo linawadhalilisha na kuwanyima wananchi wengine fursa ya kuongoza.

Katika hatua nyingine, Dk. Slaa alisema ajenda kuu atakayokwenda nayo bungeni Tendega iwapo wakazi wa Kalenga watampa ridhaa ya kuwaongoza, ni pamoja na kuihoji serikali mabilioni ya fedha za wafadhili yanayotolewa kila mwaka na Jumuiya ya Ulaya (EU) kwa ajili ya maendeleo ya serikali za mitaa yanakwenda wapi kama si kugeuzwa saccos ya wakubwa na watendaji wa halmashauri.

Mwenyekiti wa Chadema, Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Dk. Steven Kimondo, alisema wananchi wa Kalenga wanapaswa kuonyesha hasira zao kwa vitendo dhidi ya CCM kwa kumchagua mama wa familia na anayejali wanaomzunguka kwa kuwa mpinzani wao mkuu, Godfrey Mgimwa, anayegombea kupitia CCM, hajui matatizo ya Kalenga kwa sababu anaishi Uingereza na ameoa Mwingereza.

“Huyu (Grace) ni wa kwenu, lakini jamaa yetu (Godfrey Mgimwa), akikosa ubunge atarudi Uingereza, ila mama huyu atabaki hapa hapa na familia yake.  Maskini mwenzenu anayetibiwa na nyie hospitali ambazo hazina dawa na amesoma kwa kukaa chini kama nyie katika shule hizi hizi,” alisisitiza Dk. Kimondo.

Kwa upande wake, Tendega aliwaomba wananchi wa Ifunda wamchague ili akajenge hoja bungeni, ni kwa nini fedha za mfuko wa jimbo zinazotolewa na Bunge kwa ajili ya kusaidia shughuli za maendeleo ya wananchi zinatolewa kwa upendeleo.

Alisema wananchi wenye itikadi tofauti na CCM wanaojiunga katika vikundi wanabaguliwa.

“Hizi fedha zinatolewa kwa wana-CCM tu na kama wakibaini kuna kikundi kina mrengo fulani na hawamuungi mkono mbunge, wanatoswa kimya kimya na wala hawajali kama hivi ni vicoba, saccos au vikundi vya wajasiriamali wadogo...sitakubali maana nataka kwenda kuleta usawa huko Dodoma nawaomba sana mnipe kura ili tumalize wizi huu,” alisema Tendega.

CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment