EBENEZA MARCH 9 2014

EBENEZA MARCH 9 2014

Tuesday, September 24, 2013

RAIS OBAMA AMIMINIA PONGEZI KWA TANZANIA


Sep 24, 2013
*AMKUMBATIA RAIS KIKWETE NA KUMWITA 'KAKA NA RAFIKI WA KWELI' 
Maktaba: Rais Obama na Rais Jakaya Kikwete
MAREKANI
Rais wa Marekani Mheshimiwa Barack Obama ametoa pongezi na sifa kwa Tanzania kwa kuwa miongoni mwa nchi chache duniani ambazo zimetia saini mkataba wa Ushirikiano wa Serikali Zinazoendeshwa kwa Uwazi ambao unalenga kujenga na kuendeleza nafasi ya taasisi zisizokuwa za Kiserikali katika utawala bora, uwazi na uwajibikaji katika uendeshaji wa Serikali.
Rais Obama ametoa pongezi hizo kwa Tanzania leo, Jumatatu, Septemba 23, 2013, wakati akizungumza katika mkutano maalum aliouandaa mwenyewe Rais Obama kuzungumzia nafasi za Serikali katika kuunga mkono na kuendeleza asasi na taasisi zisizokuwa za Kiserikali na kuzishirikisha zaidi katika kuboresha shughuli za utawala bora uliofanyika kwenye Hoteli ya Hilton, mjini New York, Marekani.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete alikuwa miongoni mwa viongozi wachache duniani walioalikwa kushiriki mkutano huo maalum ambao pia ulishirikisha wawakilishi wa asasi zisizokuwa za Kiserikali 300.
Baadhi ya nchi nyingine za Afrika zilizoalikwa na kushiriki katika mkutano huo ni pamoja na Liberia, Ghana, Benin, Libya, Tunisia, Senegal, Afrika Kusini na Botswana.
Shabaha kuu ya mkutano huo wa saa moja ilikuwa ni kutafuta namna ya kuongeza kiwango cha kuungwa mkono kwa taasisi na asasi hizo na jinsi gani ya kuzilinda ili kuziwezesha kufanya kazi kwa ufanisi zaidi.
Aidha, mkutano huo ulilenga kuzitaka Serikali ambazo zinaweka vikwazo kwenye utendaji wa asasi hizo kuondoa vikwazo hivyo haraka ambavyo vinahujumu utendaji kazi na mchango wa asasi hizo katika uendeshaji wa utawala bora.
Katika hotuba yake ya ufunguzi wa mkutano huo, Rais Obama amezisifia nchi kama Tanzania ambazo zimetia saini makubaliano ya Ushirikiano wa Serikali Wazi ambayo yanalenga kupandisha nafasi ya asasi zisizokuwa za Kiserikali katika Utawala Bora,Uwazi na Uwajibikaji katika Serikali.
Amesema kuwa binafsi alikuwa ameamua kukutana na viongozi wa asasi zisizokuwa za kimataifa wakati wa ziara yake ya karibu katika Afrika ambako miongoni mwa nchi nyingine alitembelea Tanzania.
Rais Obama alifurahi sana kukutana na Rais Kikwete. Rais Obama alimkumbatia Rais Kikwete akimwelezea kama “kaka wa karibu na rafiki mzuri” kauli na kitendo ambacho kiliwashangaza mamia ya watu waliokuwa kwenye ukumbi.

JK: TUWASAIDIE WACONGO, WAMECHOSHWA NA VITA



RAIS KIKWETE
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete ameitaka Jumuia ya Kimataifa kufanya kila linalowezekana kumaliza mzozo wa kisiasa na mapigano katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), ili kutoa nafasi kwa wananchi wa Congo kuishi katika amani na kujitafutia maendeleo.
“Hawa ni watu walioteseka sana na kwa muda mrefu, wana haki ya kupata amani, wana haki ya kupata muda wa kupumzika kutokana na vita na mapigano,” Rais Kikwete ameuambia mkutano wa pili wa wakuu wa nchi zilizotia saini mkataba wa kutafuta amani, usalama na ushirikiano katika DRC chini ya Umoja wa Mataifa (UN).
Katika mkutano huo, uliofanyika leo, Jumatatu, Septemba 23, 2013, kwenye Umoja wa Mataifa mjini New York chini ya Uenyekiti wa Katibu Mkuu wa UN, Mheshimiwa Ban Ki Moon kama ulivyokuwa mkutano wa kwanza uliofanyika Februari 24, mwaka huu, 2013, mjini Addis Ababa, Ethiopia, Rais Kikwete amewaambia viongozi wenzake wa nchi wanachama wa Umoja wa Nchi za Maziwa Makuu (ICGLR) na wengine waliotia saini mkataba huo:
“Nadhani hatua zilizochukuliwa mpaka sasa kuhusu DRC ni nzuri na mchakato wa kutafuta amani nchini humo unakwenda vizuri. Ni muhimu tukafikia mwisho wa tatizo hili kwa sababu wananchi wa DRC wametesema mno na kwa muda mrefu. Wana haki ya kupata amani, wana haki ya kupata muda wa kutosha wa kufanya mambo ya maana kama ya maendeleo yao badala ya kukaa na kufikiria vita,” Rais Kikwete amesema kwenye mkutano huo.
Rais Kikwete amesema kuwa siri ya kufanikiwa katika DRC ni kutekeleza yale yote ambayo nchi hizo zimekubaliana kutekeleza katika DRC akisisitiza: “La msingi ni kila mmoja wetu kutekeleza yale yote tuliyokubaliana. Hiyo ndiyo siri ya kuleta amani na utulivu katika DRC.”
Mbali na Rais Kikwete, mkutano huo wa leo umehudhuriwa na Rais Yoweri Museveni wa Uganda ambaye pia ni Mwenyekiti wa ICGLR, Rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini, Rais Joseph Kabila Kabange wa DRC, Rais Paul Kagame wa Rwanda, Rais Joyce Banda wa Malawi ambaye ni Mwenyekiti wa Jumuia ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika (AU) Mheshimiwa Nkosazana Dlamini-Zuma, na Katibu Mkuu wa UN ambaye alikuwa mwenyekiti wa mkutano huo.
Aidha, mkutano huo umehudhuriwa na Makamu wa Rais na wawakilishi wa Jamhuri ya Congo (Congo-Brazzaville), Zambia, Angola na Sudan Kusini.
Kwenye mkutano huo, wasemaji wengi wamesisitiza kuwa hakuna amani ya kweli katika DRC na nchi za Maziwa Wakuu bila viongozi wa nchi hizo kukubali kuzungumza na kukubaliana na vikundi mbali mbali ambavyo vinapigana dhidi ya baadhi ya nchi hizo.
Baadaye leo, Rais Kikwete amehudhuria mkutano wa Baraza la Uongozi la Umoja wa Kutafuta Usalama wa Chakula na Ushirikiano wa Grow Africa uliofanyika kwenye Ofisi za Taasisi ya Uchumi Duniani (WEF) uliofanyika kwenye ofisi za taasisi hiyo katika Marekani mjini New York.
Rais alizungumza kwa ufupi katika mkutano huo ambako alitaka wafadhili wa miradi ya kilimo katika Afrika kuongeza kasi ya kutoa fedha za kuleta mageuzi ya kilimo katika Bara la Afrika kwa sababu kila mmoja wa wadau anatekeleza majukumu yake kwa haraka zaidi kuliko wafadhili.

MZEE MWINYI AWAONYA WANAOTUMIA ELIMU NA UJUZI WAO KUANGAMIZA USTAWI WA JAMII

DSC_1114
Elizabeth Mwase Programu Manager wa Mtandao wa Watoto na Vijana kutoka Imani Mbalimbali (GNRC) akimpokea Mzee Ali Hassan Mwinyi Rais Mstaafu wa awamu ya pili ambaye alikuwa mgeni rasmi ya Siku ya Kimataifa ya Amani iliyoadhimishwa mwishoni mwa Juma jijini Dar es Salaam ukumbi wa Don Bosco.
DSC_1121
Mgeni Rasmi Mzee Mwinyi akisalimiana na baadhi ya mabalozi na wawakilishi wa jumuiya za maendeleo za nchi wa hisani wakati wa maadhimisho hayo jijini Dar es Salaam.
DSC_1120
Mgeni Rasmi Rais Mstaafu wa awamu ya pili Alhaji Ali Hassan Mwinyi akipokea mfano wa ndege wa Amani kutoka kwa wanafunzi wa shule mbalimbali za jijini Dar es Salaam wakati wa maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Amani duniani jijini Dar.
DSC_1196
Mgeni Rasmi Mzee Mwinyi akihutubia wageni waalikwa (Hawapo pichani) wakati wa sherehe za Siku ya Kimataifa ya Amani leo asubuhi jijini Dar. Kulia ni balozi wa Rwanda nchini Ben Rugangazi na kushoto kwa mgeni rasmi ni Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia Watoto (UNICEF) Jama Gulaid.
DSC_1126
Meza kuu.
DSC_1130
Baadhi ya wanafunzi wa sekondari mbalimbali za jijini wakitumbuiza kwa nyimbo mbalimbali zenye ujumbe wa kudumisha Amani na upendo duniani.
DSC_1216
Mgeni Rasmi Mzee Mwinyi akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya mabalozi na wawakilishi wa ofisi za mabalozi waliohudhuria sherehe hizo kwenye ukumbi wa Don Bosco.
DSC_1143
Baadhi ya wageni waalikwa waliohudhuria sherehe hizo.
  

MZEE MWINYI AWAONYA WANAOTUMIA ELIMU NA UJUZI WAO KUANGAMIZA USTAWI WA JAMII

*Awaasa vijana kutotumiwa na wanasiasa kwa maslahi yao
*Ashangaa wajuzi walivyompachika jina la Ruksa enzi za miaka 1990s

Rais Mstaafu wa awamu ya pili, Alhaji Ali Hassan Mwinyi amesema kuna baadhi ya watu katika jamii hutumia elimu, ujuzi na maarifa yao kuangamiza, kubomoa na kudumaza Ustawi wa Jamii kwa maslahi binafsi na si ya Umma. Mo blog inaripoti.
Mzee mwinyi amesema hayo wakati wa kuadhimisha siku ya Kimataifa ya Amani Duniani inayoadhimishwa 21th Septemba kila mwaka ambayo imefanyika katika ukumbi wa Don Bosco jijini Dar es Salaam, amesema kuna baadhi ya watu wanatumia elimu yao vibaya kwa kupanga kuua watu wengine kwa maslahi yao aidha ya kisiasa au ya kiuchumi.
“Elimu kwa kawaida kuleta matokeo mazuri kwa jamii husika endapo itatumika sawia kwa malengo yaliyokusudiwa na kwa maendeleo endelevu ya taifa kwa ujumla, ila kuna baadhi ya wanajamii kutumia ujuzi huu vibaya na kuangamiza ustawi wa jamii husika,” amesema. 
Mzee Mwinyi aliendelea kusema kwamba katika kuadhimisha siku ya kimataifa ya amani duniani yenye kauli mbiu “Education for Peace” ni lazima elimu kwa ajili ya amani iwe endelevu hapa duniani ili iweze kuleta suluhu na utengamano katika jamii na mataifa yote duniani.
Amesema kwamba vijana nchini lazima waepuke kutumiwa na wanasiasa kwa maslahi yao ya kisiasa na wajifunze kutatua matatizo yao kwa njia ya amani bila ya kuwa na mihemko, jazba, misongo na hasira ili kuendelea kudumisha amani na upendo katika nchi yetu ambayo ni kisiwa cha amani.
“nawaasa vijana wakitanzania wa leo hata kama mmenyimwa haki zenu ni bora kutumia njia ya kistaarabu na kutumia elimu mnayopata mashuleni bila kusahau macho, masikio na vipawa vyenu mlivyopewa na mwenyezi mungu katika kutafuta haki yenu kwa njia ya amani bila misukosuko,” aliongeza.
Mzee Mwinyi alitumia nafasi hiyo kuwashangaa baadhi ya watu kwa kutumia ujuzi na elimu yao kwa kumpachika jina la Ruksa bila yeye kujua wametumia muktha gani kumpa jina hilo, lakini Mzee Mwinyi alitumia jukwaa hilo pia kuwapa ruksa vijana kutumia elimu yao kuleta hali ya amani na utulivu ndani ya nchi.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto (UNICEF) Jama Gulaid amesema kwamba Umoja wa Mataifa uliweka maazimio siku ya kimataifa ya amani duniani ili watu wanaogombana na kupigana kwa shida mbalimbali kupata nafasi ya kuweka silaha zao chini katika siku hii adhimu.
Amesema kupitia azimio hilo ambalo lilizinduliwa mwaka 1982 kwa mara kwanza linatambua uwepo wa watu wanaoathirika na vita katika sehemu mbalimbali duniani na waliokwishapoteza maisha kutokana na matatizo vita vya wenyewe kwa wenyewe.
Naye Mratibu na Mtathimini wa Mtandao wa watoto na vijana kutoka Imani Mbalimbali (GNRC) Bi, Joyce Mdachi amesema swala la amani na utulivu linaanzia kwenye kaya hadi ngazi ya taifa kwahiyo ni muhimu kwa jamii na vijana kuelewa amani inaanzia nyumbani.
“jamii iliyolelewa katika mazingira mazuri ina nafasi kubwa ya kuleta matokeo chanya kwenye mustakabali wa taifa kwa ujumla lakini jamii iliyolelewa vibaya haiwezi kubadilisha taifa kwa sababu ni zao la tunda baya,” alisema.
Mdachi alisisitiza kwamba kuporomoka kwa maadili ndani ya jamii ya leo swala hilo pia lilianzia kwenye kaya ya mtu mmoja mmoja hadi ngazi ya taifa ambapo leo hii taifa linashuhudia mambo ya kifisadi, rushwa na ubadhilifu wa mali za umma kunakofanywa na viongozi waandamizi.

ATHUMANI HAMIS BALOZI WA USALAMA BARABARANI KWA UTHAMINI WA AIRTEL

 Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Kampuni ya mawasiliano ya simu za mkononi Airtel (T) ambao wamekuwa wadhamini wakuu wa Maadhimisho ya wiki ya Nenda kwa Usalama Barabarani kwa mwaka wa tano mfululizo Bi. Beatrice Singano Mallya akisalimiana na  Mwandishi wa Habari Athumani Hamisi ambaye ameteuliwa kuwa balozi wa Usalama Barabarani na kudhaminiwa na Airtel katika wiki hii ya usalama barabarani mkoani mwanza. Athumani alipata ajali ya gari ambayo ilisababisha baadhi ya viungo vyake kupooza licha ya kupata matibabu nchini Afrika ya Kusini na India.

MWANZA, TANZANIA
 KAMPUNI ya Mawasiliano ya Simu ya Airtel imesema kuwa itahakikisha suala la Usalama barabarani linazingatiwa na jamii ya Watanzania ili kupunguza ajali za barabarani .
Kauli hiyo ilitolewa jana na Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Airtel, Beatrice Mallya kwenye ufunguzi wa Maadhimisho ya Wiki ya Usalama Barabarani,yanayofanyika Jijini Mwanza.

Alisema kama wadau wa usalama barabarani,wamedhamini maadhimisho hayo ili kuwezesha jamii kupata elimu na uelewa kuhusu matumizi ya barabara,sheria, kanuni na taratibu za usalama barabarani katika kupunguza ajali nchini.

Alisema ajali nyingi nchini zinachelewesha maendeleo na kupunguza uchumi wa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.

“Sisi kama wadau tumedhamini maadhimisho haya kwa mwaka wa tano mfululizo,lengo letu tunataka jamii ipate uelewa na hatimaye kupunguza ajali za barabarani zinaoweza kuepukika,ndiyo sababu tuko hapa,” alisema.

Alisema kutokana na kuonesha umahiri wameanzisha mfumo mpya wa ulipiaji  wa leseni za magari kwa kupitia  njia ya Airtel Money.

------
1. usalama barabarani airtel 1
Waziri wa Mambo ya ndani ya Nchi Emmanuel Nchimbi akisalimiana na
Mwandishi wa Habari Athumani Hamisi ambaye ameteuliwa kuwa balozi wa Usalama Barabarani na kudhaminiwa na Airtel katika wiki  ya usalama barabarani, mwandishi huyu alipata ajali ya gari ambayo ilisababisha baadhi ya viungo vyake kupooza licha ya kupata matibabu nchini Afrika ya Kusini na India.

1. usalama barabarani airtel 2 na 3
Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Kampuni ya mawasiliano ya simu za mkononi
Airtel Tanzania ambao wamekuwa wadhamini wakuu wa Maadhimisho ya wiki
ya Nenda kwa Usalama Barabarani kwa mwaka wa tano mfululizo Bi.
Beatrice Singano Mallya akisalimiana na  Mwandishi wa Habari Athumani
Hamisi ambaye ameteuliwa kuwa balozi wa Usalama Barabarani na
kudhaminiwa na Airtel katika wiki hii ya usalama barabarani mkoani
mwanza. Athumani alipata ajali ya gari ambayo ilisababisha baadhi ya
viungo vyake kupooza licha ya kupata matibabu nchini Afrika ya Kusini
na India.
 

PRESIDENTE JAKAYA KIKWETE PARTICIPATES IN NUTRITION CONFERENCE

President Dr. Jakaya Mrisho Kikwete speaks during a meeting on Scaling up Nutrition held in New york yesterday morning. (photos by Freddy Maro)

WANAOTUMIA TAKWIMU ZA UONGO KUKIONA:SERIKALI

Sep 23, 2013
 DAR ES SALAAM, Tanzania
 KAMISHNA wa Sensa ya  Watu na Makazi ya Mwaka 2012, Hajjat Amina Mrisho ametoa onyo kwa watu watakaotumia takwimu ambazo si sahihi wakati wanapotoa taarifa mbalimbali kuwa wawe makini kwa kuwa sheria  ya kuwabana iko mbioni.

Aidha  Hajjat Amina   amesema  kwamba kwa watendaji wa Serikali, na wanasiasa  watakaotoa takwimu za uongo katika taarifa mbalimbali  wajiandae kuong’ooka  katika nyadhifa zao.

Kauli hiyo imetolewa leo na Kamshina huyo wakati  akizungumza na waandishi wa habari kwenye ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu(NBS) kuhusu uzinduzi wa kitabu cha pili  cha idadi ya watu cha umri na jinsi, ambacho kitasaidia kupanga mikakati mbalimbali ya kimaendeleo.

“Muswada wa Sheria ya   Takwimu wa mwaka 2013 imeshasomwa mara ya kwanza Bungeni ,unasubiriwa  kusomwa kwa mara ya pili katika Bunge lijalo. Hivyo  itakapokamilika  sisi tutapambana na watu wanaotoa takwimu ambazo si sahihi. Kwa watendaji wa Serikali watakaotumia takwimu ambazo si sahihi wakati wanapotoa taarifa mbalimbali mfano tatizo la njaa linawakabili watu kiwango  kipi  wajiandae kufukuzwa kazi,” alisema Hajjat Amina.

 Alisema suala linatakiwa pia kuzingatiwa watu wataotangaza au kuandika,wakiwemo waandishi wa habari  takwimu zilizotajwa na mtu bila ya kufanyiwa uchunguzi kupitia mtandao wa ofisi hiyo watachukuliwa hatua kulingana na sheria hiyo.

Hajjat Amina alifafanua kuwa takwimu hizo zitakuwa zitaboreshwa kwa kila mwaka, hivyo aliwataka watu kuzitumia ipasavyo  kulingana na taarifa za kila mwaka.

Akizungunzia kuhusu uzinduzi huo, alisema utafanyika Septemba 25, mwaka huu katika ukumbi wa mikutano wa Mwalimu Julius Nyerere uliopo jijini Dares Salaam, ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi  Sief  Ali Iddi .

Aidha Hajjat Amina aliongeza kuwa  ofisi hiyo itato vitabu 2 , kitabu cha tatu kuhusu takwimu za walemavu kifuata kitazinduliwa mwishoni mwa mwezi wa Okctoba na cha nne kitakachoonesha  takwimu za kila mkoa, utakuwa na chake

POLISI WATATU WAFARIKI, NANE WAJERUHIWA KATIKA AJALI YA GARI WAKITOKA KATIKA OPERESHENI KIMBUNGA

Na Chibura Makorongo,Kahama 
POLISI watutu wa wa mkoa wa Njombe wamekufa na wengine wanane kujeruhiwa wakiwemo maofisa uhamiaji baada ya gari walilokuwa wakisafiria kupinduka katika kijiji cha Malenge  wilayani Kahama mkoa wa Shinyanga.
Ajali hiyi imetokea ikihusisha gari lenye namba PT 0762 aina ya Landrover 110 kupinduka jana saa 12:00 jioni lilipokuwa likitokea mkoani Kagera katika operesheni Kimbunga ya kuwaondoa wahamiaji haramu  ambapo lilikuwa njiani kurudi mkoani Njombe.
Kaimu kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga Kihenye Kihenya alisema  marehemu hao walitambulika kwa jina moja kuwa ni PC Marco wa kituo cha polisi Njombe,  D-CPL Fredy  pamoja na PC Sufiani wote wa kituo cha polisi Makambako.
Aidha kaimu kamanda aliwataja majeruhi ambao ni askari polisi kuwa ni Pc Hussein aliyepata jeraha kichwani pamoja na mguu wa kushoto na hali yake inalezwa kuwa ni mbaya ambapo hadi sasa hajazinduka,  Inspekta Leornad aliyemia kiuno, PC Yusuph ambaye ndiye dereva wa gari hilo aliyeumia kiuno wote kutoka kituo cha Njombe.
Wengine ni  DC Lambuli aliyeumia paji la uso pamoja na mguu wa kulia, PC James aliyeumia goti pamoja na mkono wa kushoto pamoja na PC Adamu aliyeumia paji la uso nao kutoka kituo cha polisi cha Njombe.
Maafisa uhamiaji waliokuwemo kwenye ajli hiyo aliwataja kuwa ni Glory Temu kutoka mkoa wa Mbeya na inaelezwa kuwa hali yake ni mbaya ambapo hadi sasa hajapata fahamu pamoja na Augustino Nanyambe kutoka mkoa wa Rukwa aliyeumia goti pamoja na mkono wa kushoto.
Kamanda Kihenya alisema kuwa miili ya marehemu hao imehifadhiwa katika hospitali ya wilaya ya Kahama huku pia majeruhi hao wakipatiwa matibabu katika hospitali hiyo na kuongeza kuwa chanzo cha ajali hiyo hakijafahamika ambapo polisi bado wanaendelea na uchunguzi.

CCM YAWA LULU NYAMONGO, WILAYANI TARIME


 Katibu Mkuu wa CCM Ndugu Abdulrahman Kinana akikata utepe kama ishara ya kufungua ofisi ya CCM Tawi la Nyabichune,wilaya ya Tarime mkoani Mara.

Ofisi ya CCM Tawi la Nyabichune wilaya ya Tarime mkoani Mara ambalo Katibu Mkuu wa CCM Ndugu Abdulrahman Kinana alilizindua rasmi leo tarehe 23 Septemba 2013..
 Katibu wa NEC Itikadi na Uenezi Nape Nnauye akihutubia wakazi wa Nyamongo na kuwaeleza namna ambavyo wamejipanga kutatua tatizo la muda mrefu baina ya wakazi wa eneo hilo na wamiliki wa mgodi wa North Mara .
 Katibu Mkuu wa CCM Taifa Ndugu Abdulrahman Kinana akimsikiliza mmoja wa wakazi wa Nyamongo Chacha Magayo Butora ambaye alifafanua kwa kina matatizo yanayowakabili wakazi wa eneo hilo,Katibu Mkuu alitumia Demokrasia ya hali ya juu baada ya kuwapa nafasi watu watatu mbali mbali ambao wananchi waliwachagua waje kuelezea matatizo yao.
 Katibu Mkuu wa CCM Ndugu Abdulrahman Kinana akihutubia wakazi wa Nyamongo wilaya ya Tarime mkoani mara ambapo aliamua kufuta kila kitu kwenye ratiba yake na kutaka wananchi wateue wawakilishi wao ili wakakae kikao na watu wa serikali ili kupata ufumbuzi wa matatizo hayo.
 Naibu Waziri wa Nishati na Madini Ndugu Stephen Masele akifafanua mambo kadhaa ambayo Wizara yake inataka wananchi wafaidike na migodi ikiwa pamoja na kuwasaidia wachimbaji wadogowadogo ambao wanatakiwa wajiunge kutengeneza vikundi.
 Katibu Mkuu wa CCM Ndugu Abdulrahman Kinana pamoja na Katibu wa NEC Itikadi na Uenezi wakiongea na wananchi wa Nyamongo ,Wananchi wa Nyamongo wameshukuru sana kwa kusikilizwa kwa ukaribu haijawahi tokea na wameahidi kutoa ushirikiano wa kutosha kwa Viongozi hao.
Katibu wa NEC Itikadi na Uenezi Nape Nnauye akisoma moja ya taarifa inayofafanua matatizo ya wakazi wa Nyamongo.
Baadhi ya wakazi wa Nyamongo wakiwa kwenye kikao cha ndani pamoja na Katibu Mkuu wa CCM Ndugu Abdulrahman Kinana,Katibu wa NEC Itikadi na Uenezi Nape Nnauye,Naibu Waziri Nishati na Madini Ndugu Stephen Masele na Viongozi wengine wa Serikali ambapo walikaa na kujadili matatizo yao namna ya kuyatatua.

No comments:

Post a Comment