MBUNGE wa
Ubungo, John Mnyika (CHADEMA), amemtaka Rais Jakaya Kikwete, kujitokeza
hadharani na kukiri kuwa Ikulu imeshindwa kusimamia kauli aliyoitoa juu
ya ujenzi wa kituo kipya cha mabasi yaendayo mikoani na nje ya nchi
(UBT).
Pia Mnyika
amemtaka Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Dk. Didas Masaburi ajitokeze
ndani ya wiki moja na aeleze sababu ya kumdanganya Rais Kikwete kuwa
kituo kipya cha mabasi yaendayo mikoani na nje ya nchi kingekamilika
Januari mwaka huu.
Mnyika
alitoa kauli hiyo jana alipofanya ziara ya kushtukiza katika kituo cha
mabasi Ubungo kwa ajili ya kujionea miundombinu ya kituo hicho baada ya
kufanyika ubomoaji wa awali na kusitishwa kwa huduma muhimu ndani ya
kituo hicho.
“Kama rais
alitoa agizo na halikusimamiwa, anapaswa arudi na atuambie kuwa
ameshindwa kusimamia kauli yake, lakini pia Meya Masaburi aseme
hadharani kuwa walimuongopea rais juu ya upatikanaji wa kituo kabla ya
Januari mwaka huu, kwa kuwa sasa ni miezi sita imepita na hakuna taarifa
yoyote wala maandalizi ya kuwapo kwa kituo hicho,” alisema Mnyika.
Katika ziara
hiyo Mnyika alishuhudia adha wanazopata abiria ikiwamo ukosefu wa vyoo
vya uhakika, eneo la kujihifadhi wakati wa mvua pamoja na kukosekana kwa
gereji ndani ya kituo hicho.
Aidha,
abiria walimueleza mbunge huyo namna wanavvyolipa kiingilio katika
mageti ya kuingilia ndani huku kukiwa hakuna huduma yoyote wanayopata
wakiwa ndani.
Kwa upande
wao wafanyakazi wa kada tofauti ndani ya kituo hicho walielezea kero
wanazokabiliana nazo baada ya kituo hicho kuvunjwa.
Kwa upande
wa madereva walieleza kuwa licha ya Sumatra kuagiza wamiliki wa mabasi
ya abiria kuwapatia mikataba ya ajira madereva wao suala hilo
halijafanyika mpaka sasa.
Ushindi wa CHADEMA waibua mazito
WAKATI ushindi wa kishindo wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) jijini Arusha ukimweka pabaya Meya wa Jiji la Arusha, mazito mengine yameibuka baada ya Mkurugenzi wa Jiji la Arusha, Sipora Liana, kutoboa siri kubwa.
Mbele ya
madiwani wapya wa CHADEMA wakiongozwa na Mbunge wa Arusha Mjini,
Godbless Lema, Liana alisema alikuwa anafikiria ‘kukimbia’ kutokana na
hali tete ya usalama kugubika jiji hili.
Katika kikao
kifupi cha utambulisho wa madiwani hao wapya, Liana alisema: “Wakati
ninakuja hapa (Arusha) kulikuwa na taarifa za vurugu na maandamano,
jambo ambalo lilinifanya nifikirie kama hali ingeendelea kuwa hivyo
nitaomba niondoke, lakini nimeridhishwa na utulivu uliokuwepo jana
(juzi),” alisema Mkurugenzi Liana.
Kauli hiyo
ilimfanya Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, kumweleza mkurugenzi
huyo kuwa hata wao CHADEMA wataendelea kumpa ushirikiano wa kutosha
kuhakikisha kuna kuwapo maendeleo ya wananchi wa jiji hilo, hasa
kutokana na namna alivyoonyesha ushirikiano wakati wa uchaguzi huo.
Alisema kuwa
halmashauri hiyo inakabiliwa na kashfa za ufisadi wa mabilioni ya fedha
za wananchi, jambo alilosema kuwa madiwani na wabunge wa CHADEMA wako
tayari kumsaidia kuyafumua yote ili wayashughulikie kwa masilahi ya
wananchi wa Arusha na si vyama vya siasa.
“Kwa namna
ulivyotoa ushirikiano (siku ya uchaguzi) kila nilipokupigia simu hata
kwa suala dogo ulikuwa unahakikisha linapatiwa ufumbuzi hata zile
taarifa kuwa uliletwa kuhakikisha CHADEMA haichukui hata kiti kimoja cha
udiwani sasa imeondoka,” alisema Lema.
Lema alisema
kuwa nao wameanza kupata imani na mkurugenzi huyo kwa namna
alivyoendesha uchaguzi huo, kwani awali waliambiwa kuwa aliletwa kwa
ajili ya kuhakikisha CHADEMA hairudishi kata hizo.
Mkurugenzi
huyo alimjibu Lema kuwa yeye yupo kwenye jiji hilo kwa ajili ya
kuwahudumia wananchi wote bila kujali itikadi za vyama, huku akiwaahidi
ushirikiano madiwani hao ambapo alisema kuwa atahakikisha fedha za
wananchi zinalindwa, huku akisisitiza kuwa jambo hilo anaweza kulifanya
hata bila madiwani, kwani hata madiwani hao nao wakienda kinyume huwa
anawakamata.
“Diwani
aliyechaguliwa na wananchi ndiye nitakayefanya naye kazi, ila na yeye
akileta masuala binafsi, hapo na mimi atanikuta,” alisema Liana, jambo
lililofanya watu wote kucheka.
Naye Katibu
wa CHADEMA Kanda ya Arusha, Amani Golugwa, alimpongeza mkurugenzi huyo
kwa namna alivyosimamia uchaguzi huo na kumtaka aendelee hivyo hivyo ili
ile dhana kuwa CHADEMA ndio wanasababisha vurugu Arusha iondoke na
ukweli ujulikane kuwa wanaosababisha vurugu mara zote ni watawala.
Madiwani hao
wapya na kata zao kwenye mabano, Bryson Ngowi (Kimandolu), Emanuel
Kessy (Kaloleni), Millace Kinabo (Themi) na Jeremiah Mpinga (Elerai),
ambao walisindikizwa na msafara mkubwa wa viongozi na mashabiki wa
CHADEMA ulioanzia kwenye ofisi zao za Mkoa wa Arusha zilizoko Ngarenaro
na kupita kwenye Barabara ya Sokoine kuelekea kwenye ofisi hizo za
mkurugenzi, hali iliyoamsha shamrashara kwa wananchi kila walipokuwa
wakipita.
Msafara huo
uliojumuisha magari, pikipiki na waenda kwa miguu, ambapo madiwani hao
pamoja na Lema walikuwa kwenye gari la wazi, hali iliyosababisha
shughuli kusimama kwa muda kila ulipokuwa ukipita, huku kelele za zamu
ya meya kung’oka zikivuma kila mahali.
No comments:
Post a Comment