Jumatano Usiku, Man United ilichapwa Bao
3-1 na Bayern Munich kwenye Robo Fainali ya UCL, UEFA CHAMPIONZ LIGI,
na kutupwa nje kwa Jumla ya Bao 4-2 katika Mechi mbili.
Matokeo hayo yanamaanisha Msimu wa Mabingwa hao wa England sasa umekwisha.
Yapo matumaini madogo mno kwamba
wanaweza kuliua pengo la Pointi 7 kati yao na Timu iliyo nafasi ya 4
kwenye Ligi Kuu England huku wakiwa wamebakiza Mechi 5 ili wao wacheze
UCL Msimu ujao.
Kwa mujibu wa Darren Fletcher, ambae
aliongea mara baada ya kufungwa huko Munich, kilichobaki ni kwa
Wachezaji hao hao walioiangusha Timu Msimu huu kujituma katika Mechi
zilizobaki ili wabakie kwenye Kikosi kipya Msimu ujao.
Jana, Meneja wa Timu, David Moyes,
alidokeza kuwa mwishoni mwa Msimu wataijenga upya Timu na wapo Wachezaji
ambao washawasuka ili kuhamia Old Trafford.
Uamuzi huu unamaanisha kuwa wapo Wachezaji kadhaa itabidi wauzwe ili wapya waje.
Fletcher amefafanua: “Wachezaji ni
lazima wacheze vizuri ili wabaki kwenye mipango ya Meneja. Ipo
minong’ono mingi kuwa yatakuwepo mabadiliko makubwa!”
Wachambuzi wamedai Moyes atalazimika
kusaini Wachezaji kadhaa wapya wakiwemo, Sentahafu, Mafulbeki wawili na
Viungo wawili ili kuimarisha Timu na kuanza kuijenga upya.
Akigusia uwezekano wa kukosa kucheza
UEFA CHAMPIONZ LIGI kwa mara ya kwanza tangu Mwaka 1995, Fletcher
alisema: “Hatutafikiria hilo, tutafikiria kutwaa Ubingwa na kurudi Ulaya
kama Mabingwa!”
Kuhusu uwezekano wa wao kucheza EUROPA LIGI Msimu ujao, Fletcher alisema: “Tuikumbatie! Twende na kutwaa Kombe!”
No comments:
Post a Comment