EBENEZA MARCH 9 2014

EBENEZA MARCH 9 2014

Thursday, April 10, 2014

JESHI la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani limewafukuza kazi askari wake 10 kwa kosa la kwenda kinyume cha kanuni na sheria za jeshi hilo.

Kamanda wa Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani nchini, Mohamed MpingaJESHI la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani limewafukuza kazi askari wake 10 kwa kosa la kwenda kinyume cha kanuni na  sheria za jeshi hilo.
Akizungumza na waandishi wa habari  jijini Dar es Salaam jana, Kamanda wa Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani nchini, Mohamed Mpinga, alisema  kuwa askari hao walipatikana na hatia baada ya kufunguliwa mashitaka ya kijeshi.
Alisema: “Baada ya kufunguliwa mashtaka yaliyokuwa yakiwakabili ya kwenda kinyume na mwenendo wa Jeshi la Polisi, walipatikana na hatia hivyo wengine tuliwafukuza na wengine kuwabadilisha vituo vyao vya kazi.”
Mpinga alisema wameamua kuwashughulikia askari hao ili kurejesha imani kwa wananchi ambao baadhi yao wameanza kupoteza imani wakiamini kuwa wapo askari wa barabarani wanaokiuka maadili ya jeshi hilo, lakini wanalindwa.
Ingawa Kamanda Mpinga hakutaja makosa ya askari hao, lakini habari za kipolisi kutoka ndani ya jeshi hilo wanadaiwa kuwa walijihusisha na vitendo vya rushwa, kinyume cha maadili na sheria za jeshi hilo.
“Hali hiyo imechangia kwa kiasi kikubwa utendaji wa kazi kuwa mgumu na jamii kutoamini kazi zinazofanywa na jeshi hilo, ndiyo maana tumeamua kuchukua hatua kali na tutaendelea kufanya hivyo kwa wengine wenye tabia hiyo,” alisema Mpinga.
Askari hao wamefukuzwa ikiwa ni siku chache baada ya Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam kutangaza kuwafukuza kazi askari wake wanne kwa makosa ya utovu wa nidhamu, ikiwemo kujihusisha na vitendo vya ujambazi.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam,  Suleiman  Kova, askari hao wanadaiwa kushiriki kwenye tukio la ujambazi lililotokea Machi 9, mwaka huu, eneo la Mbezi Beach baada ya kuvamia ofisi za Kampuni ya Kichina ya Hong Yang inayojishughulisha na kazi za ujenzi.
Polisi wadaiwa kuua tena
Katika hatua nyingine, Jeshi la Polisi mkoani Tabora kwa mara nyingine limeingia katika kashifa nzito, kufuatia baadhi ya askari wake kudaiwa kuua raia mmoja aitwaye Mbeyu Mkuya (35) kwa kumpiga risasi mgongoni iliyopenya ndani ya mwili wake na kutokea shingoni.
Tukio hilo limetokea Aprili 7, mwaka huu majira ya saa 3 usiku katika Mtaa wa Kanoni, Kata ya Isevya, Manispaa ya Tabora.
Habari zinadai kwamba baadhi ya askari polisi waliokuwa katika doria walikwenda nyumbani kwa marehemu kwa ajili ya kusaka pombe haramu aina ya gongo na kumkuta marehemu huyo akiwa ndani na kumkamata.
Taarifa hizo zinadai kuwa baada ya kumkamata marehemu huyo mmoja wa askari hao, alimpiga kofi marehemu akimshinikiza aseme ukweli kuhusu kama anajihusisha na uuzaji wa pombe ya gongo ambapo walianza kumshambulia na baadaye waliondoka naye hadi alipopatikana ameuawa kwa kupigwa na risasi mgongoni.
Kutokana na  hali hiyo, ndugu wa marehemu Mbeyu Mkuya, wamekataa kuuchukua mwili wa marehemu huyo kwenda kuuzika hadi ufanyike uchunguzi wa kina wa tukio hilo na kumwomba Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP) Ernest Mangu, afike mkoani Tabora ili ajionee mwenyewe vitendo vya kinyama vinavyofanywa na baadhi ya askari wake.
Wakizungumza na waandishi wa habari mjini hapa, ndugu hao wa marehemu,  Rajabu Rashidi, ambaye ni mjomba wa marehemu na Ally Mkuya, kaka wa marehemu, walidai kwamba ndugu yao alikamatwa na polisi nyumbani kwake usiku na kuanza kupigwa kwa tuhuma za uuzaji wa pombe haramu ya gongo.
Walidai kuwa polisi hao baada ya kumpiga waliondoka na marehemu huyo wakidai wanampeleka katika shimo la mchanga ili wakamsulubu zaidi hadi ashike adabu katika tukio lilitokea Aprili 7, mwaka huu majira ya saa 3 usiku katika Mtaa wa Manoni, Kata ya Isevya, Manispaa ya Tabora.
Baada ya marehemu huyo kuchukuliwa na polisi hao, ndugu hao walikwenda katika kituo kikuu cha polisi kwa ajili ya kumdhamini ndugu yao lakini wakajibiwa kuwa jina la mtu huyo halipo kituoni hapo, na kwamba wajaribu kwenda kuulizia Kituo cha Polisi cha Relwe ambako nako hawakumpata hadi walipopata taarifa kwamba kuna mtu ameokotwa polini akiwa amekufa.
Walisema baada ya kwenda hospitali waligundua kuwa ni marehemu Mkuya aliyekamatwa na polisi, hali ambayo inaleta sintofahamu kwa wakazi wa mjini Tabora.
Hata hivyo katika hali isiyokuwa ya kawada taarifa za kipolisi wilayani Uyui zilidai kwamba kuna mtu kaokotwa akiwa amekufa katika pori la Kata ya Ibiri na Inonelwa wilayani Uyui.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama Wilaya ya Tabora ambaye pia ni mkuu wa wilaya hiyo, Sulemani Kumchaya, alisema amezipata taarifa hizo na kwamba anazifuatilia zaidi ili hatua za kinidhamu nichukuliwe kwa wahusika.

“Taarifa hizo ninazo, ninachowaomba muwe wavumilivu kidogo ili na mimi niweze kufuatilia jambo hilo,” alisema Kumchaya.
Naye Kamanda wa Polisi mkoani Tabora, Suzana Kaganda, alithibitisha kutokea tukio hilo lakini akasema mwili wa marehemu huyo ulikutwa katika pori la Ibiri, Wilaya ya Uyui mkoani hapa.
Alisema baada ya mwili huo kuokotwa na wananchi na polisi kwenda kuuchukua kuupeleka hospitali, ndugu wa marehemu walijitokeza na kudai kuwa mwili huo ndio wa ndugu yao marehemu Mkuya aliyekamatwa na polisi siku ya tukio hilo.
“Ninachoweza kusema kuwa ni kweli tukio lipo, na hawa ndugu wa marehemu ni kweli wamekataa  kuuchukua mwili wa ndugu yao, lakini kesho utafanyika uchunguzi mwingine ili kubaini ukweli wenyewe,” alisema kamanda huyo.
Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tabora, Kitete, Dk. Leimond Wilson, alikiri kupokea mwili huo na kufafanua kwamba mwili huo ulikutwa ukiwa na jeraha mgongoni la kupigwa risasi na kutokezea shingoni.
“Ni kweli tuliupokea mwili wa marehemu huyo na baada ya kuufanyia uchunguzi ilibainika ulikuwa na jeraha la mgongoni kitu kinachosadikiwa kuwa ni risasi,” alisema Dk. Wilson.

No comments:

Post a Comment