EBENEZA MARCH 9 2014

EBENEZA MARCH 9 2014

Thursday, April 10, 2014

KIKWETE AELEZA KUHUSU SHERIA YA GESI NA MAFUTA

Rais Jakaya Kikwete, amesema serikali ipo katika hatua za mwisho kuandaa sheria, kanuni na taratibu kwenye sekta ya gesi na mafuta na kwamba hadi ifikapo Oktoba, mwaka huu, zitakuwa zimekamilika ili wazawa washiriki kikamilifu.
"Mbali na kuwawezesha wazawa pia sheria, kanuni na taratibu hizo, zitafungua milango kwa wawekezaji wa ndani kushiriki kwenye sekta hizo nchini," alisema.

Aliyasema hayo wakati akizindua ripoti ya Taasisi ya Utafiti Kuondoa Umaskini Repoa), kwenye kongamano la 19 la mwaka, jijini Dar es Salaam jana.

Rais Kikwete alisema kwenye uwekezaji wa gesi na mafuta, taifa litapata manufaa makubwa na mabilioni ya Shilingi yataingia.

Hivyo akasema ni nafasi muhimu pia kwa Watanzania wenye biashara za kati na ndogo ndogo kunufaika na uwekezaji huo.

Alisema katika uwekaji wa sheria na taratibu, lazima mambo ya urasimu na rushwa viondolewe mara moja ili kuhakikisha sekta hiyo inakuwa na kunufaisha wananchi wote.




Rais Kikwete alisema lazima serikali na wadau wote muhimu wajiridhishe hakuna wizi wala utapeli katika sekta ya gesi na mafuta ili kumletea mwananchi wa kawaida maendeleo.
Alisema lazima serikali ihakikishe inajipanga vizuri ili kuzuia vitendo vyovyote vya hujuma, wizi na rushwa ili kuleta matokeo chanya kwa nchi na watu wake.

Rais Kikwete alisema kwa muda mrefu watafiti wa ndani wamekuwa na msaada mkubwa katika kuisaidia serikali kutambua maeneo yenye mahitaji zaidi na hasa katika kuboresha maisha ya wananchi na kupambana na tatizo la ajira nchini.

“Tafiti hizi za kila mwaka zimekuwa na msaada mkubwa kwa wafanyabiashara wadogo wadogo, wakulima na wananchi wa kawaida katika kufanya uamuzi sahihi kwenye maeneo,” alisema.

Alisema Tanzania kuna ajira ndogo ndogo milioni tatu, lakini wanaofanya ajira hizo ni milioni 5.2 kati yao, asilimia 64 ni wanawake.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Repoa, Profesa Samwel Wangwe, alisema tafiti hizo zinalenga kuwasaidia wananchi wanaojishughulisha na biashara ndogo ndogo ili kupunguza umaskini.

Alisema malengo ya tafiti pia ni kuongeza tija kwa kupata uzoefu kutoka nchi mbalimabali ulimwenguni jinsi ya kujenga viwanda, kusindika chakula na kupambana na tatizo la ajira hasa kwa vijana na wanawake.

 

CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment