Ratiba ya awali iliyotolewa na Ofisi ya Bunge ilionyesha kuwa Februari 16 na 17, mwaka huu, ni kuwasili na usajili wa wajumbe wa Bunge hilo, na mkutano kuanza Februari 18 kwa kuanza kupata maelekezo ya ukaaji na jiografia ya ukumbi.
Pia, kusomwa kwa tangazo la kuitisha Bunge Maalum, uchaguzi wa Mwenyekiti wa muda, kuandaa na kupitisha Kanuni za Bunge Maalum.
Februari 19 na 20, kikao cha kazi ya kuandaa rasimu ya kanuni za Bunge Maalum, Februari 21, kupitisha Azimio la kuridhia kanuni za Bunge, uchaguzi wa Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti, kiapo cha Katibu na Naibu Katibu wa Bunge.
Februari 21 ilikuwa ni kiapo kwa Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti na Februari 22 kiapo cha wajumbe wa Bunge, na Februari 24 hadi 30 ufunguzi rasmi wa Bunge, uwasilishaji wa Rasimu ya Katiba kwenye Bunge, mjadala wa kupitisha Rasimu ya Katiba kadiri kanuni zitakavyoainishwa.
Hata hivyo, kilichofanyika hadi juzi kabla ya kuahirishwa hadi leo ni uchaguzi wa Mwenyekiti wa muda na kuwasilishwa kwa rasimu ya kanuni na sheria ya mabadiliko ya Katiba na wajumbe kukabidhiwa na kupewa muda wa kuzisoma huku kamati ya kanuni ikichambua kanuni hizo na itaziwasilisha leo.
Mwenyekiti wa muda, Pandu Ameir Kificho, alisema juzi kuwa Kamati ya Kanuni imeomba siku mbili kukamilisha kazi na leo na kesho wajumbe watakuwa kwenye kikao kazi cha kupitia kanuni na uchambuzi wake.
Ijumaa azimio la kuridhia kanuni za Bunge litapitishwa katika kikao cha Bunge hilo.
Hata hivyo, haijajulikana lini Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti, Katibu na Naibu Katibu wa kudumu watapatikana, kuapishwa kwa wajumbe, uzinduzi wa Bunge na kuwasilishwa kwa rasimu.
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment