Taarifa iliyotumwa jana kwa vyombo vya habari, ilieleza kuwa Rais hakumtembelea Maranda, kama ilivyoripotiwa na gazeti moja la kila siku na wala hajawahi kumtembelea siku yoyote, iwe ni hospitalini ama kwingineko.
“Kwa hakika, ni jambo la kusikitisha kuwa gazeti lenye heshima na hadhi linaweza kujiingiza katika utunzi na uandishi wa uongo wa kiasi hiki,” ilieleza taarifa hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Rais alitembelea Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Upasuaji wa Mishipa ya Fahamu (MOI) katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili juzi, kuwajulia hali wanahabari wawili; Salum Mkambala wa Channel Ten na Margaret Chambili, ambaye sasa yupo Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).
Rais alianza kumtembelea Mkambala ambaye amelazwa wadi binafsi D, baada ya kupata ajali ya gari iliyomfika kwenye eneo la Visiga, Mkoa wa Pwani, akiwa njiani kwenda Morogoro mwishoni mwa wiki. Chumba hicho kilikuwa na wagonjwa watatu.
“Baada ya kuzungumza na Mkambala, Rais, kama ilivyo kawaida yake anapotembelea wagonjwa hospitali, aliwasalimia na kuwajulia hali wagonjwa wengine wawili, ambao wako katika chumba hicho kimoja na Mkambala. “Wagonjwa hao wawili ni John Mhina, ambaye huko nyuma alipata kusoma na Rais na Reuben Nyanga,” ilieleza taarifa hiyo.
Baada ya kumaliza kuwajulia hali wagonjwa hao, taarifa hiyo ilieleza kuwa Rais alikwenda kwenye wadi nyingine binafsi Namba K, ambako alimjulia hali Margaret, ambaye ni mgonjwa pekee aliyelazwa katika chumba hicho na baada ya hapo, Rais Kikwete aliondoka Muhimbili kurudi Ikulu, Dar es Salaam.
“Hakuna wakati wowote, Rais alimtembelea Maranda ama mgonjwa mwingine kwenye hospitali hiyo ya Muhimbili,” ilisisitiza taarifa hiyo.
No comments:
Post a Comment