EBENEZA MARCH 9 2014

EBENEZA MARCH 9 2014

Wednesday, February 26, 2014

CHADEMA YAPATA PIGO

Madiwani  wawili wa Chama cha  Demokrasia na Maendeleo (Chadema)  katika Manispaa ya Shinyanga wametanganza kujiuzulu nyadhifa zao wakidai uongozi ngazi ya taifa  wa chama hicho unaendekeza majungu na  kudhalilisha baadhi ya viongozi kwa kuwaita wahaini au wasaliti bila kuchambua ukweli.
Madiwani hao, Sebastiani Peter  kutoka kata ya Ngokolo na Zacharia Mfuko kutoka kata ya Masekelo, jana walizungumza na waandishi wa habari mjini Shinyanga na kusema wamechukua uamuzi huo kutokana na makosa yaliyofanywa na viongozi wa kitaifa wa Chadema kwa nyakati tofauti.

Peter alitaja sababu tatu zilizopelekea kujiuzulu kwake, ya kwanza alisema ni Novemba mwaka 2013 kikundi cha ulinzi cha chama hicho (Red Brigade) kiliandika  barua kwa Katibu Mkuu, Dk. Willibrod  Slaa  (pichani chini) kuwa wamehongwa Sh. milioni 90 na CCM kukisaliti chama chao.
Alisema sababu ya pili ni kutokana na kutotimizwa kwa ahadi ya Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, ya kujenga nyumba ya aliyekuwa mgombea ubunge wa chama hicho Jimbo la Shinyanga Mjini, marehemu Shelembi.

Jambo la tatu alisema ni tabia  iliyozuka ndani ya chama hicho kuwadhalilisha viongozi wa chini kwa kuwabatiza majina mbalimbali kama wasaliti na wahaini wa chama.

Kwa upande wake, Masekelo alisema uamuzi wake wa kujiuzulu ni kutokana na kuwapo ubabaishaji ndani ya chama hicho na kwamba kuna sakata la  mwenyekiti wa mtaa kukigawa kiwanja  huku kukiwa na kamati ya ugawaji lakini aliwaeleza viongozi wa chama mpaka sasa hakuna kinachoendelea.

Katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 Manispaa ya Halmashauri ya Shinyanga ilipata madiwani  18, kati yao 10 ni wa CCM na wanane Chadema.

Akizungumzia hatua hiyo kwenye mkutano wa kampeni za uchaguzi mdogo Jimbo la Kalenga jana, Dk. Slaa, amesema kujiuzulu kwa madiwani hao ni mpango maalum uliosukwa na mahasimu wao kisiasa kwa ajili ya kuivuruga Chadema isiwe mshindani mkuu wa CCM katika uchaguzi mkuu ujao.

Kwa mujibu wa Dk. Slaa, madiwani hao wamejiondoa Chadema baada ya kulipwa Sh. milioni 20 kila mmoja ili wajivue nyadhifa zao.

CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment