VIONGOZI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika
halmashauri ya Mtwara Vijijini, wametakiwa kuwa makini na viongozi wa serikali
za vijijini wanaojihusisha na uuzaji ardhi kiholela, ili kudhibiti upungufu wa
ardhi siku za usoni, kunakotokana na ardhi kupungua huku vizazi vikiongezeka.
Rai hiyo imetolewa na mkuu wa wilaya ya Mtwara,
Williman Kapenjama Ndille wakati akiwasilisha Utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha
Mapinduzi (CCM), kwa miaka miwili ya kuanzia January hadi Disemba 2012 na
January hadi Disemba mwaka 2013, katika mkutano wa halmashauri kuu ya CCM
Mtwara vijijini na kufanyika katika ukumbi wa mikutano wa Benjamini Mkapa
uliopo katika chuo cha ualimu Mtwara Kawaida.
Amewakumbusha viongozi hao wa chama kuwa, wajibu wao
mkubwa ni kutoa elimu kwa wananchi juu ya faida za kuhifadhi ardhi kwa manufaa
yao ya sasa na vizazi vinavyokuja, ili kuja kuiwekeza kwa faida kwa siku za
baadae.
Akizungumzia sekta ya kilimo amesema kuwa mwaka huu
hali ya chakula hairidhishi, kutokana na upungufu wa mvua, na wakati mwingine
kunyesha kwa kiwango cha juu hali inayochangia kuharibu mazao yaliyo
mashambani.
Awali akizungumza katika mkutano huo wa halmashauri
kuu ya CCM Mtwara Vijijini, Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Mtwara Mohammed Sinani
amesisitiza kuwa ni wajibu wa viongozi wa chama kuwajengea wananchi mazingira
ya kuondokana na umasikini, kwa kuhakikisha wanawaelekeza kwa wataalamu walio
katika halmashauri mkoani humo.
Katika hatua nyingine mwenyekiti huyo amewaonya wale
wote wenye nia ya kutangaza kugombea nafasi mbalimbali za uongozi ikiwemo
ubunge na udiwani kuwa muda huo bado, na amewataka kuwaacha wali madarakani
kumaliza vipindi vyao vya uongozi, huku akiwataka viongozi wote kulipigia
kelele suala hilo, ili kuepuka siasa za makundi, kubaguana na kupakana matope.
Chanzo, CCM.
No comments:
Post a Comment