EBENEZA MARCH 9 2014

EBENEZA MARCH 9 2014

Monday, February 24, 2014

BUNGE LA KATIBA SASA TAREHE NYINGI

DALILI za Bunge Maalum la Katiba kushindwa kumalizika ndani ya siku 70 za mwanzo, na hivyo kuhitaji kuongezwa siku nyingine zisizozidi 20 kisheria, zimeanza kuonekana mapema.
Tayari ufunguzi rasmi wa Bunge hilo lililopewa siku 70 kumaliza shughuli zake, uliotarajiwa kufanyika leo, umepigwa kalenda na sasa Rais Jakaya Kikwete, anatarajiwa kufungua Bunge hilo siku yoyote wiki hii.
Hata hivyo kama shughuli za ratiba ya awali iliyovurugwa zikiruhusiwa kufanyika kabla ya ufunguzi huo, matarajio ya ufunguzi huo yatakuwa Ijumaa wiki hii.
Kalenda
Awali, kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa wiki iliyopita kwa vyombo vya habari na Katibu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk Thomas Kashillilah, ufunguzi huo ungefanyika leo saa 8 mchana.
Ufunguzi huo ulitarajiwa kufanywa na Rais Jakaya Kikwete, ambaye alitarajiwa kufika hapa jana, lakini sasa hautafanyika kwa mujibu wa ratiba hiyo kutokana na kuchelewa kukamilika kwa Kanuni za Bunge hilo.
Ilitarajiwa kazi ya kuandaa Rasimu ya Kanuni ifanyike Jumatano na Alhamisi iliyopita na Ijumaa zingepitishwa na Bunge na kufuatiwa na uchaguzi wa Mwenyekiti wa Bunge na Makamu wake na baadaye kuapisha wajumbe.
Ratiba hiyo ya zamani pia ilionesha kuwa viapo kwa wajumbe vilitarajiwa kufanyika kwa siku tatu kabla ya ufunguzi wa Bunge.
Hivyo kama Rasimu ya Kanuni itapitishwa leo au kesho na kisha uchaguzi wa Mwenyekiti na Naibu kufanyika, ni dhahiri kazi ya kuapisha wajumbe itakamilika Alhamisi au Ijumaa asubuhi ndio ufunguzi ufanyike.
Mbali na matarajio hayo yanayotokana na uhalisia wa shughuli ambazo zinapaswa kufanyika kabla ya ufunguzi, pia mmoja wa maofisa wa Serikali, alilieleza gazeti hili kuwa uwezekano wa ufunguzi wa Bunge hilo ni Ijumaa kutokana na hali inavyokwenda sasa bungeni.
Kinachoendelea
Mwenyekiti wa Muda wa Bunge Maalum la Katiba, Pandu Ameir Kificho jana alitarajiwa kukutana na Kamati ya wajumbe wateule 20 kupitia Kanuni hizo ambayo ingempatia maelezo ya awali, kabla ya leo au kesho kuziwasilisha kwa wajumbe wote wateule bungeni.
Aidha, Kamati ya wajumbe wateule ambao ni wabunge wa CCM, ilitarajiwa kukutana jana jioni, lakini kikao hicho kiliahirishwa na haikutajwa tarehe nyingine ya kukutana. Jumanne iliyopita mkutano wa wajumbe wateule wa Bunge hilo ulianza, ambapo wajumbe hao walipewa maelekezo ya ukaaji na jiografia ya ukumbi.
Siku hiyo mchana, kulisomwa tangazo la kuitishwa kwa Bunge Maalumu na baadaye kukafanyika uchaguzi wa kumchagua Mwenyekiti wa Muda.
Spika wa Baraza la Wawakilishi, Pandu Ameir Kificho, alishinda kiti cha Mwenyekiti wa Muda akiwabwaga gwiji wa sheria, Profesa Costa Mahalu na mwanasheria mwingine, Magdalena Rwebangira. Kificho alipata kura 393, sawa na asilimia 69.19, huku wenzake kila mmoja akipata kura 84 sawa na asilimia 14.79 ya kura 568 zilizopigwa na wajumbe.
Baada ya kukalia kiti hicho, kulianza kazi ya kuandaa rasimu ya Kanuni za Bunge hilo, ambapo Jumatano wajumbe wateule walikabidhiwa rasimu hiyo Alhamisi zikawasilishwa rasmi na watendaji wa Bunge kwa wajumbe hao.
Baada ya kuwasilishwa huko, Kificho aliunda Kamati ya wajumbe wateule 20 ya kumshauri kuhusu kuandaa Kanuni hizo na aliahirisha vikao hadi leo.
Bunge Maalumu la Katiba lina wajumbe wateule 629, ambao ni wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na wajumbe 201 waliotokana na makundi mbalimbali katika jamii.
Kamati ya Posho
Taarifa tulizopata kutoka katika Kikao cha Kamati ya Posho, zilidai kuwa wajumbe wa Kamati hiyo, walipokea maombi ya nyongeza ya posho kutoka Sh 300,000 kwa siku mpaka Sh 700,000.
Pamoja na maombi hayo, inadaiwa Kamati hiyo imekubaliana na kilio cha wengi katika jamii na kupinga nyongeza hiyo ya posho.
Hata hivyo, taarifa za ndani zimedai kuwa Kamati hiyo imependekeza posho hiyo ya Sh 300,000 itolewe mpaka siku za mwisho wa wiki, tofauti na ilivyo sasa.

Kwa sasa wajumbe hao katika siku za mwisho wa wiki na sikukuu, wanalipwa posho ya Sh 80,000 tu ambayo ni ya kujikimu na siku za kazi ndio wanapewa posho hiyo ya kujikimu na posho ya kazi ambayo ni Sh 220,000 kwa siku.
Kampeni Mwenyekiti
Ingawa kazi ya kuandaa Rasimu ya Kanuni inaonekana kuchukua muda mrefu, kubwa kwa sasa ni uchaguzi wa Mwenyekiti wa Bunge, ambao tayari umezua mijadala katika kila kona ya Bunge kuliko hata uchaguzi wa Naibu wake.
Ingawa sio rasmi, lakini ‘mafahali’ wawili ambao ni wajumbe wateule wa Bunge hilo, Samuel Sitta na Andrew Chenge, wanatajwa kuwa katika kinyang’anyiro.
Wenyewe wamekataa kuthibitisha hilo, lakini wapambe wao wamekuwa wakipita kwa wajumbe kila mmoja akivutia upande wake.
Mjumbe mteule wa Bunge hilo ambaye pia ni Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, akifungua semina ya Jumuiya ya Wazazi ya CCM mjini hapa juzi, alikiri kuwa Bunge Maalumu la Katiba limeanza na changamoto nyingi.
Pinda alienda mbali zaidi na kukiri kuwa uchaguzi wa Mwenyekiti ni sehemu ya changamoto hizo, lakini akabainisha kuwa chama kimejipanga vizuri na anaamini watavuka salama na kusonga mbele.
Baada ya Rais Kikwete kuzindua Bunge Maalumu la Katiba, utafuata uwasilishwaji wa Rasimu ya Katiba, na kuanza kwa mijadala yake ambayo imepangwa kufanyika hadi ukomo wake, Aprili 30, mwaka huu.
>>>>Habari leo

No comments:

Post a Comment