Zanzibar. Watu wanne wamejeruhiwa baada ya milipuko minne inayoaminika kuwa ni mabomu kutokea katika maeneo matatu tofauti Zanzibar.
Katika moja ya matukio hayo, watu wanne
walijeruhiwa, mmoja akikatika mguu, katika eneo la Unguja Ukuu, Mkoa wa
Kaskazini Unguja. Majeruhi wawili wamelazwa katika Hospitali ya Mnazi
Mmoja, Unguja.
Mkuu wa Operesheni wa Polisi, Mkoa wa Kusini
Unguja, Hamad Said Masoud alisema mlipuko wa kwanza ulitokea juzi katika
eneo la Fuaoni Maili Nne wakati watu wasiojulikana waliporusha kitu
kinachoaminika kuwa ni bomu wakati waumini wa Kanisa la Evangelist
wakiendelea na ibada ya Jumapili.
Kamishna wa Polisi Zanzibar, Hamdan Omar Makame
alisema tukio la juzi, kitu kinachosadikiwa kuwa ni bomu kilirushwa
wakati waumini wa kanisa hilo wakiendelea na ibada na kutoa mlipuko na
kishindo kikubwa. Alisema wakati wakiendelea na uchunguzi wa tukio hilo,
milipuko mingine mitatu ilitokea jana.
Katika mlipuko wa kwanza kwa jana uliotokea saa
6.30 mchana katika kituo kimoja cha fundi vyuma aliyetambulika kwa jina
la Juma Abdallah huko Unguja Ukuu ndiko kulikokuwa na watu
waliojeruhiwa.
Waliojeruhiwa katika tukio hilo ni Pandu Haji Pandu aliyekatika mguu na Shaaban Khamis Ibrahim ambaye aliumia sehemu za kiuno.
Hamad alisema mtu mmoja aliokota chuma kizito na kukipeleka kwa fundi akitaka atengenezewe nanga kwa ajili ya uvuvi.
Alisema mhunzi huyo alipokea kazi hiyo na
alipokuwa akijiandaa kwa matengenezo ndipo mlipuko huo ulipotokea.
Mlipuko huo ulitokea sambamba na mwingine katika Mgahawa wa Mercury’s
uliopo Malindi, Mkoa wa Mjini Magharibi na kusababisha huduma za chakula
kusitishwa kwa muda.
Tukio la mwisho lilikuwa saa 7:15 mchana katika
Kanisa la Anglikana, Mkunazini. Katibu wa Kanisa hilo Dayosisi ya
Zanzibar, Nuhu Saranya alisema: “Nilisikia kishindo cha mlipuko, wakati
nikitafakari ni kitu gani hicho, nikasikia mlipuko wa pili nje ya kanisa
letu,” alisema.
Mmoja wa majeruhi, Mohamed Ibrahim alisema hakujua
kilichotokea huku akilalamika kuwa masikio yake hayasikii vizuri
kutokana na kishindo hicho.
>>>Mwananchi
>>>Mwananchi
No comments:
Post a Comment