Na shafii mohamed ,Arusha
Jumla ya kesi 507 zinazohusiana na matukio ya ukatili na unyanyasaji
wa Kijinsia zimeripotiwa katika Dawati la Jinsia na Watoto la Mkoa wa Arusha ambapoTakwimu
hizo ni toka Novemba 2012 hadi Novemba 2013 mwaka huu.
mkaguzi wa jeshi la polisi Dawati la jinsi na watoto Bi Honorina Msoka akitoa zawadi kwa baadhi ya wagonjwa walio lazwa wold ya kina mama na watoto katika Hospitali ya mkoa wa Arusha mountimeru |
Hayo yalielezwa na Mkuu wa kitengo hicho Mrakibu Mwandamizi wa
Polisi (SSP) Mary Lugola wakati watendaji wa ofisi hiyo walipoungana na wadau mbalimbali
duniani kuadhimisha siku 16 za kupinga Ukatili na Unyanyasaji wa Kijinsia walipotembelea
Shirika lisilo la Kiserikali la Faraja centre linaloshughulika na malezi ya watoto
wanaoishi katika mazingira magumu na wasichana waliojifungua wakiwa na umri mdogo
pamoja na wagonjwa waliolazwa katika hospitali ya Mkoa ya Mount Meru.
Akitoa ufafanuzi kuhusiana na kesi hizo alisema kwamba, idadi
hiyo imeongezeka kwa asilimia 14.7 ikilinganishwa na Novemba 2011 hadi Novemba
2012 ambapo kesi 442 ziliripotiwa.
Alisema ongezeko hilo linatokana na elimu inayotolewa
mara kwa mara na Ofisi hiyo kwa wananchi kupitia mikutano na vyombo vya habari hali
iliyowafanya wananchi wahamasike kupinga vitendo vya ukatili na unyanyasaji kwa
kutoa taarifa katika Ofisi hiyo.
Alisema kati ya kesi hizo, kesi zilizokuwa zinawahusu wanawake
ni 280 wakati wanaumeni 120 huku watoto ni 107. Miongoni mwa kesi hizo tayari kesi
132 zimekwishafikishwa mahakamani huku kesi 375 zinaendelea kupelelezwa.
Mkuu huyo wa Dawati la Jinsia na Watoto (SSP) Mary Lugola alisema
kwamba miongoni mwa kesi zinazoripotiwa katika ofisi hiyo ni pamoja na ubakaji,
kulawiti, ukatili dhidi ya mtoto, migogoro katika ndoa na kadhalika.
Akizungumza wakati anawatembelea watoto wanaoishi katika mazingira
magumu na wasichana waliojifungua wakiwa na umri mdogo ambao wanalelewa na Shirikalisilo
la Kiserikali la Faraja na wagonjwa waliolazwa katika Wodi ya Watoto hospitali ya
Mkoa ya Mount Meru, (SSP) Mary Lugola alisema kwamba katika kuonyesha kujali kitengo
cha Dawati kimeamua kuungana nao kwa kuwatembelea na kutoa zawadi mbalimbali
kwa makundi hayo.
Kwa upande wake msimamizi wa Shirika lisilo la Kiserikali la
Faraja Young Women Development Organization Bi. Martina Siara alilishukuru
jeshi la Polisi mkoani hapa kitengo cha Dawati kwa jinsi linalovyoshirikiana na
kituo hicho cha Faraja katika katika suala zima la ulinzi pamoja na utoaji wa
elimu na ushauri kwa wanafunzi waliopo kituoni hapo hivyo kuwapa mwanga
kuhusiana na haki zao.
Jeshi la Polisi kupitia kitengo cha Dawati Mkoani hapa limeadhimisha
siku 16 za kupinga Ukatili na Unyanyasaji wa Kijinsia kwa kutembelea kituo cha
Faraja na wodi ya watoto katika hospitali ya Mount Meru kwa kutoa zawadi
mbalimbali kwa watoto wa kituo hicho pamoja na wagonjwa waliolazwa hospitalini
hapo huku likiwa na kauli mbiu ya jeshi hilo nchini isemayo “Zinduka tumia Dawati la Jinsia na Watoto
kukemea Ukatili wa Jinsia na Watoto”.
No comments:
Post a Comment