![]() |
Jumla ya watoto wa kike 1,056 wameacha masomo ya shule ya msingi, kutokana na mimba zilizosababishwa na mazingira magumu wanayoishi, zikiwamo tamaduni mbalimbali za makabila.
Mtaalamu wa Maendeleo ya Jamii, Rosely Kaihula wa Mfuko wa Maendeleo ya Watoto EKAMA, ametoa takwimu hiyo wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu siku ya mtoto wa kike duniani itakayoadhimishwa Oktoba 11, mwaka huu.
Mtaalamu huyo amesema sababu nyingine ni mazingira magumu, ikiwemo kutokuwa na kipato kwa wazazi ama walezi pindi mtoto anapohitaji mahitaji muhimu, hali inayomsababishia arubuniwe na hatimaye kujikuta na ujauzito.
Kwa upande wake Mratibu wa masuala ya Familia wa Shirika la SOS Children’s Villages, Magdalena George, amesema lengo la maadhimisho hayo ni kuongeza uelewa kwa jamii, juu ya masuala mbalimbali yanayomsibu mtoto wa kike, ambapo yataishirikisha serikali, watoto na NGO’s mbalimbali.
Maadhimisho ya mwaka huu ambayo yatafanyika jijini Dar es salaam na kuhutubiwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Anna Maembe, yatakuwa na kaulimbiu isemayo: “Chochea ubunifu kuboresha elimu ya mtoto wa kike.”


No comments:
Post a Comment