![]() |
| MAHAKAMANI |
NA:FARAJI MAARUFU
Mahakama kuu kanda ya Dar es salaam imetupilia mbali
pingamizi lililokua limewekwa na upande wa serikali, la kupinga makampuni
matano ya simu kuunganisha madai yao dhidi ya serikali, kupinga kuwepo kwa tozo
ya shilingi elfu moja katika laini za simu.
Kesi iliyopo mbele ya jopo la majaji watatu ikiongozwa
na jaji Aloyce Mujunguzi, imefunguliwa na chama cha kutetea walaji nchini
ambacho kinapinga kukatwa kwa kodi hiyo.
Akitoa maelezo hayo kiongozi wa jopo hilo jaji Mujunguzi, amesema kuwa mahakama imeona kuwa
upande wa serikali hauna hoja za msingi, hivyo anaziruhusu kampuni hizo
kuungana na chama cha walaji kupinga tozo hiyo.Katika shauri hilo chama hicho pamoja na kampuni za
simu za Airtel, Zantel, Ttcl, Vodacom na tigo, zinatetewa na mawakili
wanaoongozwa na wakili Fatma Karume, wakati upande wa serikali unaongozwa na
wakili Aloycea Mbuya.
Shauri hilo limepewa muda na jaji hadi tarehe kumi
na tano mwezi huu, ili kampuni hizo ziwe zimewasilisha mambo ambayo wanataka
yafanyiwe kazi, ili yaunganishwe na mambo yaliyokwisha wasilishwa na chama cha
walaji.
Jaji huyo pia ameutaka upande wa serikali, hadi
itakapofika tarehe 21 ya mwezi huu uwe umejibu maelezo ambayo yatakua
yameelezwa na upande wa pili wa walalamikaji, na baada ya hapo mahakama itaanza
kushughulikia kesi hiyo.

No comments:
Post a Comment