NA MSHAM NGOJWIKE
RAIS Mpya wa Shirikisho la Soka Nchini (TFF), Jamal Malinzi amewazawadia wajumbe wa
mkutano mkuu ofa ya kuendelea kubaki jijini Dar es Salaam kwa siku moja zaidi
ikiwa ni pamoja na kuwalipa posho.
Awali wagombea hao walitakiwa kuondoka jijini jana na
kurejea makwao kufuatia kumalizika kwa uchaguzi mkuu wa shirikisho hilo
uliofanyika juzi na kumalizika usiku wa manane katika ukumbi wa Waterfront
jijini Dar es Salaam.
Akizungumza mara baada ya kuachiwa kiti hicho cha urais kutoka
kwa Leodegar Tenga aliyekaa madarakani toka 2005 – 2013, Malinzi alimwaga
cheche pale alipotamka kutoa ofa ya wajumbe kuendelea kubaki jijini kwa siku
moja huku akiahidi kulipa gharama za hoteli waliyofikia ya Landmark pamoja na
posho zao.
“Mbali na kukaa katika hotel hiyo kwa siku moja zaidi nawapa
ofa pia ya kuwapa posho yao ya mda huo mpaka watakapoondoka siku inayofuata
kwani watakuwa wamechoka kutokana na uchaguzi kumalizika usiku wa manane, ”alisema.
Alisema pia anamshukuru mpinzani wake Athuman Nyamlani kwa kufanya
kampeni za amani bila ya kuchafuana hivyo kuwa tayari kushirikiana naye pamoja
na wengine wote katika kuendeleza soka la Tanzania.
“Natoa pia shukrani kwa wajumbe wote wa mkutano mkuu wa uchaguzi 2013 kwa kunikubali
na hata wale walionipinga kwani ndiyo demokrasia, kwa ujumla nawashukuru kwa kunipa
dhamana ya kuwa Rais wa TFF,”alisema
Aliongeza: “Kweli dunia imekuwa kijiji, kwani kipindi cha
masaa 72 baada ya kuzindua ilani yangu ya uchaguzi, nimepokea salamu, maoni na
mapendekezo toka ndani na nje ya Tanzania ikiwa ni pamoja na Burundi, Ivory
Coast, Denmark na NewZealand, nitatumia vizuri mawazo hayo kujenga soka letu”alisema.
No comments:
Post a Comment