EBENEZA MARCH 9 2014

EBENEZA MARCH 9 2014

Saturday, June 7, 2014

Serikali yaanza kusambaza kompyuta vyuoni

WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda amesema Serikali kwa sasa imeanza kusambaza kompyuta katika vyuo vikuu nchini kwa lengo la kuboresha elimu kwa wanafunzi. Pia, amesema baadaye Serikali itaanza kusambaza kompyuta ndogo zinazobeba vitabu kidijitali, maarufu kama tabuleti (tablets) kwa wanafunzi.

Alisema hayo bungeni jana wakati wa kipindi cha maswali ya papo kwa hapo. Alikuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu, Maryam Msabaha (Chadema).
“Nchi zilizoendelea zimewekeza sana katika elimu, lakini sisi Tanzania kwa nini hatuwekezi katika elimu ?” Alihoji.
“Sisi hapa mtoto akienda shule asubuhi anabeba fagio, lakini kwa wenzetu anabeba kompyuta. Hata kwa majirani zetu Kenya, mtoto anabeba lap top asubuhi.”
Msabaha aliongeza “Je huoni kwamba wakati umefika sasa kwa wanafunzi wetu wa darasa la Kwanza hadi la Saba wawe na lap top?” Akijibu swali hilo, Pinda alisema Serikali imejitahidi kuboresha Sekta ya Elimu nchini, kuanzia shule za msingi, sekondari, vyuo na vyuo vikuu.
Waziri Mkuu alisema inachofanya Serikali kwa sasa ni kutatua matatizo hayo ya msingi katika Sekta ya Elimu hatua kwa hatua. Kuhusu suala la kusambaza kompyuta shuleni na vyuoni, Waziri Mkuu alisema kwa sasa lengo la Serikali ni kusambaza kompyuta katika vyuo vikuu na baada ya hapo ndipo zitafuata shule za sekondari na msingi.
Waziri Mkuu alisema Serikali ingependa wanafunzi wawe na tabuleti na lap top, lakini uwezo wa Serikali ni mdogo na ndiyo maana wameamua kuanza na wanafunzi wa vyuo vikuu.
Waziri Mkuu aliulizwa swali lingine na Mbunge wa Ilemela, Highness Kiwia (Chadema), ambaye alitaka kujua ni lini atawarejesha madarakani madiwani watatu wa Jimbo la Ilemela Mkoa wa Mwanza, waliofukuzwa na Meya wa Manispaa hiyo.
“Meya wa Ilemela alifukuza madiwani watatu wa Chadema, kwa madai hawakushiriki vikao vitatu vya Baraza la Madiwani. Nilikuletea vielelezo na wewe ulifanya uamuzi wa kuwarejesha, lakini nasikia ulipata pingamizi kutoka Mkoa wa Mwanza. Sasa ni mwaka mmoja na miezi sita tangu wamefukuzwa. Je, ni lini utawarejesha?” Alihoji Kiwia.
Waziri Mkuu alisema hakuna kitu chochote cha makusudi kinachochelewesha kutoa uamuzi wa mwisho wa suala hilo.
Alisema ni kweli alishafanya uamuzi wa kuwarejesha, lakini alipata pingamizi (counter request) kwamba maelezo aliyopewa hayakuwa sahihi.


Alisema baada ya hapo, alirejesha tena suala hilo kwa wataalamu na mamlaka zingine ili wamshauri tena na kwamba ni juzi tu amepata mapendekezo ya wataalamu hao na mamlaka hizo. Pinda alimtaka Mbunge huyo kuwa na subira, kwani uamuzi atautoa hivi karibuni.
“Tarehe siwezi kusema ni lini. Lakini suala hili nitalipa umuhimu mkubwa. Nitafanya uamuzi hivi karibuni na nitarejesha uamuzi huo mkoani Mwanza,” alisisitiza.
Waziri Mkuu ndiye mwenye dhamana na Serikali za Mitaa.
SOURCE>>HABARI LEO

No comments:

Post a Comment