Wakuu wa shule, Waalimu na viongozi mbalimbali
nchini, wametakiwa kushirikiana na serikali pamoja na taasisi zilizokasimiwa na
mamlaka ya kusimamia uendeshaji wa huduma ya usafiri wa majini na nchi kavu
(SUMATRA), ili kuhakikisha kuwa elimu ya haki na wajibu inafika kwa usahihi kwa
walengwa wa utumiaji wa huduma hiyo.
Wito huu umetolewa na Afisa Elimu Mkoa wa Mtwara
HIPSON KIPENYA, wakati wa hotuba yake ya kuzindua vyama vya wanafunzi mashuleni
vya watumiaji wa huduma ya usafiri wa nchi kavu na majini katika mkoa huo.
Amesema kuwa kwa kutoa elimu ya haki na wajibu kwa
mtumiaji wa vyombo vya usafirishaji, kutasaidia vyombo hivyo kutoa huduma kwa
mujibu wa matakwa ya sheria, na mikataba baina ya watumiaji na mtoa huduma ya
usafiri.
Kipenya amewataka walimu wakuu wa shule, wakurugenzi
wa halmashauri, kwa kushirikiana na Baraza la SUMATRA mkoa, kufuata sheria na
taratibu zilizopo za ufundishaji katika sekta ya elimu, kwa kuwapa nafasi
wanafunzi kujifunza na kushiriki matukio pale inapobidi.
Afisa Elimu huyo ameitaka kamati na Baraza kuwa
makini, kuweka mikakati na mbinu madhubuti za kuwaelimisha wananchi kufahamu
haki na wajibu wao na kupata mwitikio wa watumiaji wengi wa huduma za usafiri
wa majini na nchi kavu.
Chanzo, SUMATRA, Mary Mpandula – Pride fm.
No comments:
Post a Comment