Rais
mpya wa Madagascar Hery Rajaonarimampianina akiapishwa rasmi rais wa nchi hiyo
mjini Antananarivo kufuatia ushindi mkubwa alioupata katika uchaguzi mkuu
uliofanyika nchini humo mwezi Desemba 2013.
Rais
mpya wa Madagascar Hery Rajaonarimampianina akisani kiapo chake tayari kuanza
kazi ya kuwatumikia wananchi wa Madagascar mbele ya Jaji Mkuu wan chi hiyo Jean
–Michael Rasolonjatovo (kushoto) wakati wa sherehe za kumuapisha rais huyo
zilizofanyika mjini Antananarivo.
Rais
mpya wa Madagascar Hery Rajaonarimampianina akizungumza na wananchi wa
Madagascar waliofurika ndani ya uwanja wa Antananarivo mara baada ya kuapishwa
kuwa rais mpya wa nchi hiyo mjini. Picha na 5 na 6. Viongozi mbalimbali na
wanachi waliohudhuria sherehe za kuapishwa kwa Rais mpya wa Madagascar Hery
Rajaonarimampianina mjini Antananarivo.
Tanzania
imesema kuwa itaendelea kushirikiana na Madagascar katika masuala mbalimbali na
kuhakikisha kuwa vikwazo ilivyowekewa nchi hiyo na jumuiya za kimataifa
vinaondolewa kufuatia nchi hiyo kurejesha utawala wa kidemokrasia.
Akizungumza
katika mahojiano maalum mjini Antananarivo, Madagascar, Waziri wa Mambo ya Nje
na Ushirikiano wa Kimataifa Mh. Benard Membe amesema kuwa sasa serikali ya
Madagascar imefungua ukurasa mpya wa ushirikiano sio tu na Tanzania bali nchi
za Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC), Umoja wa Afrika
(AU) na Jumuiya za kimataifa.
Waziri
Membe ambaye alikuwa amemwakilisha Rais Jakaya Kikwete katika sherehe za
kuapishwa kwa rais mpya wa Madagascar Bw. Hery Rajaonarimampianina
zilizofanyika katika mji mkuu wa nchi hiyo Antananarivo jana amesema kuwa
Tanzania imefurahishwa na hatua hiyo na kuongeza kuwa huo ni ushindi mkubwa kwa
SADC.
Amesema
kuwa mwaka 2009 Madagascar iliingia katika machafuko yaliyosababisha serikali
halali iliyokuwepo madarakani ya Rais Mark Ravalomanana kupinduliwa na
kufafanua kuwa Tanzania ikiwa Mwenyekiti wa Kitengo cha Amani na Usalama cha
nchi za jumuiya ya SADC (TROIKA) imekuwa mstari wa mbele kuhakikisha kuwa amani
ya kudumu inapatikana nchini humo.
“Kiongozi
mpya wa Madagascar aliyepatikana na kuapishwa ni ushindi kwa Tanzania kwa
sababu Rais Jakaya Kikwete amejihusisha sana na upatikanaji wa kiongozi huyo,
kama tunakumbuka rais Kikwete alimuita nchini Tanzania kwa mazungumzo rais
aliyekuwa madarakani Bw. Andry Rajoelina mara nne, mazungumzo haya yamezaa
matunda tunayoyaona leo” amesema Mh. Membe.
Amefafanua
kuwa yapo mambo makubwa ambayo Tanzania imeyafanya kufanikisha kupatikana kwa
amani ya kudumu nchini Madagascar ikiwemo upatikanaji wa katiba ambayo
ilikamilika mwezi wa 8 mwaka 2013 ,kufanikiwa kuwashawishi Andry Rajoelina na
Mark Ravalomanana waliokuwa mahasimu kutoshiriki kugombea katika uchaguzi mkuu
wa nchi hiyo.
Amesema
Tanzania imefurahishwa na kitendo cha rais Andry Rajoelina aliyeingia
madarakani kwa kufanya mapinduzi kukubali kuachia madaraka na kuachia utawala
wa demokrasia utawale nchini humo.
Ameeleza
kuwa Tanzania sasa iko tayari kushirikiana na Madagascar na kama mjumbe wa SADC
itahakikisha kuwa vikwazo ilivyowekewa nchi hiyo vinaondolewa pia kuhakikisha
kuwa kiongozi huyo mpya anashiriki mkutano wa wakuu wa nchi za Afrika
utakaoanza tarehe 30 mwezi huu.
“Tulimwahidi
rais aliyekuwa madarakani Bw. Andry Rajolina kuwa atakapotekeleza hayo
tunayoyataka ikiwemo kuanzisha mchakato wa katiba, kuruhusu utawala wa demokrasia,
na kuruhusu uchaguzi ili kupata rais mpya sisi tutakuwa mstari wa mbele
kushawishi nchi za SADC na nchi za AU kuwaruhusu kushiriki mikutano yote ili
waweze kuijenga nchi yao na jambo hilo tutalifanya ” amesisitiza Mh.Membe.
Katika
houtuba yake mara baada ya kuapishwa rais Rajaonarimampianina amesema kuwa
utawala wake unaanza ukurasa mpya wa kuijenga upya nchi hiyo iliyokuwa
imegawanyika kisiasa na kusababisha chumi wake kudorora huku akiueleza umati
mkubwa wa watu waliohudhuria sherehe za kuapishwa kwake kuwa ataongeza
mapambano dhidi ya rushwa na kuleta amani, utulivu na maridhiano kwa
mustakabali wa taifa hilo.
Madagascar
ambayo sasa inaingia katika utawala mpya wa rais Hery Rajaonarimampianina
ambaye hapo awali alikuwa Waziri wa Fedha wa nchi hiyo iliingia katika
machafuko yaliyosababisha kuondolewa kwa utawala wa rais Mark Ravalomanana
aliyekimbilia uhamishoni nchini Afrika Kusini.
Hery
Rajaonarimampianina akiungwa mkono na rais aliyepita Andry Rajoulina anakuwa
rais wa 4 wa nchi hiyo kufuatia ushindi mkubwa alioupata katika uchaguzi mkuu
uliofanyika nchini humo mwezi Desemba 2013 uliompatia asilimia 53.3 dhidi ya
mpinzani wake Bw. Jean Louis Robinson aliyepata asilimia 46.5.




No comments:
Post a Comment