EBENEZA MARCH 9 2014

EBENEZA MARCH 9 2014

Wednesday, January 29, 2014

KUFUNGIA MAGAZETI IFIKE MWISHO ASEMA LOWASA SHERIA LAZIMA IBADILIKE


WAZIRI MKUU MSTAHAFU: EDWARD LOWASA

MWENYEKITI wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Edward Lowassa, amesema anakerwa na tabia ya serikali kufungia magazeti na amemfunda Naibu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Juma Nkamia na kumtaka amalize vifungo visivyo na mwisho vya baadhi ya vyombo vya habari nchini.
Pia waziri mkuu huyo wa zamani, amemtaka Nkamia ahakikishe katika majukumu yake mapya ya unaibu waziri anamshauri vizuri waziri wake kuhakikisha wanamaliza migogoro iliyopo baina ya wizara na vyombo vya habari nchini.
Lowassa alitoa kauli hiyo jana jijini Dar es Salaam wakati kamati yake ikimuaga Juma Nkamia aliyekuwa mmoja wa wajumbe wa kamati hiyo kabla ya hivi karibuni Rais Jakaya Kikwete kumteua kuwa naibu waziri wa wizara hiyo.
Lowassa alisema si jambo jema kwa vyombo vya habari kuendelea kukaa katika vifungo visivyojulikana mwisho wake katika zama hizi ambapo uhuru wa vyombo vya habari unatakiwa upewe kipaumbele.
Aliongeza kuwa ni wakati muafaka kwa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo wakaanzisha majadiliano ya kutafuta muafaka na makundi yote yanayojihusisha na masuala ya habari.
Kwa upande wake, Waziri Nkamia alisema licha ya kuwa na siku sita ofisini tangu aanze kazi katika wizara hiyo, ameshaomba mrejesho wa sheria iliyotumika kuyafungia baadhi ya magazeti kwa ajili ya mapitio zaidi.
Pia ameahihidi kumshauri Waziri wake, Fenella Mukangara, akutane na wahariri wa vyombo vya habari kwa ajili ya kumaliza tofauti zao.
Alisema ni aibu kwa kiongozi wa serikali kuacha kuandikwa au kutangazwa na baadhi ya vyombo vya habari kwa sababu ya tofauti ya kimtazamo.
Ushauri wa Lowassa kwa Naibu Waziri Nkamia umekuja ikiwa ni takriban mwaka mmoja na nusu umepita tangu serikali ilipolifungia gazeti la Mwanahalisi kwa muda usiojulikana, kwa madai ya kuandika habari zilizotafsiriwa kuwa ni za uchochezi, uhasama na uzushi dhidi ya serikali.
Katika kulifungia Mwanahalisi, serikali ilitumia Sheria ya Magazeti ya mwaka 1976, kifungu Na. (25) (i).
Kifungu hicho ndicho kinacholalamikiwa na wadau wa habari kuwa kinanyima uhuru wa vyombo vya habari na kwamba ndiyo sheria iliyokuwa ikitumiwa na wakoloni kuwazuia viongozi wa TANU kutoa maoni.
Kwa mfano, mwaka 1958 Tanganyika ikiwa chini ya ukoloni wa Waingereza, Mwalimu Julius Nyerere alishtakiwa kwa kukashifu baada ya kuandika makala iliyodaiwa kuwakashifu wakuu wa wawili wa wilaya.
Mwalimu Nyerere wakati huo alikuwa mhariri wa gazeti la Sauti ya TANU na alishtakiwa kwa vifungu vya uchochezi vilivyoingizwa pia kwenye Kanuni ya adhabu ya sasa na Sheria ya Magazeti ya mwaka 1976.
Kwa kosa hilo, Mwalimu Nyerere alihukumiwa kifungo cha miezi sita jela au kulipa faini ya paundi 150. Nyerere alimaliza kesi hiyo kwa kulipa faini.
Baada ya uhuru, si Mwalimu Nyerere wala marais waliofuatia waliokubali kubadilisha sheria hizo, bali zimeendelea kuwatafuna Watanzania kila mara.

>>Tanzania daima

No comments:

Post a Comment