MJADALA kuhusu lugha ya kutumia kufundishia shuleni umepamba moto, ambapo
baadhi ya wabunge wamejitokeza kupinga Kiingereza kutumika kufundishia shule za
msingi mpaka vyuo vikuu.
Wakati
wabunge hao wakiwa na msimamo huo, jana Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na
Mafunzo ya Ufundi, Profesa Sifuni Mchome, alisema Serikali haijafikia uamuzi wa
kuruhusu Kiingereza kutumkika kuanzia shule za msingi, na hivi sasa
inashughulikia changamoto kubwa zaidi.
“Haya
yote yanaweza kutatuliwa iwapo sekta hii tutaibadili na kuwa ya kisasa zaidi,
katika eneo la vitabu kila mwanafunzi akiwa na kompyuta yake ni rahisi kitabu
kuwekwa kwenye CD na wanafunzi wote wakakisoma kupitia kompyuta zao,” alisema
Profesa Mchome alipozungumza na Habari leo.
Watetezi
wa Kiswahili Mbunge wa Kibiti, Abdul Malombwa akizungumza jana katika ofisi
ndogo za Bunge alipinga matumizi ya Kiingereza badala ya Kiswahili shuleni na
kusisitiza kuwa kitendo hicho si tu kitaua Kiswahili bali pia kitaondoa uwezo
wa mwanafunzi kuelewa.
“Kwenye
ripoti yetu tumeweka wazi kuhusu hili, tunataka lugha ya Kiswahili itumike
kufundishia hadi vyuoni, na tumetoa mapendekezo yetu ya namna ya kutekeleza
mfumo huu, ikiwamo kuboresha Kiswahili chenyewe ili kiendane na masomo,”
alisema Malombwa ambaye pia ni mjumbe wa Jukwaa la Taasisi na Mamlaka za
Udhibiti wa Ubora wa Elimu nchini.
Aliongeza
kuwa walipendekeza kila mkoa angalau uwe na shule moja ya sekondari ambayo
itafanya majaribio ya kufundisha kwa Kiswahili masomo yote na kuona kama itafaa
au la.
Mbunge
wa Mgogoni, Kombo Khamis Kombo, alisema anasikitishwa na namna Kiswahili
kinavyonyimwa kipaumbele katika elimu, kiasi cha nchi jirani ya Kenya kubeba
sifa ya ujuzi wa lugha hiyo kimataifa.
“Hii
ni lugha yetu lazima tuipe kipaumbele tuijenge, lakini leo nashangaa eti
Wakenya ndio wanaonekana wanaijua vizuri na wanapewa kazi za kufundisha mataifa
mengine, hatukubali hili lazima libadilike,” alisisitiza.
Mchome
“Jukwaa la Taasisi na Mamlaka za Udhibiti wa Ubora wa Elimu nchini limetoa
maoni yake kwa Waziri Mkuu juu ya suala hili la matumizi ya lugha ya Kiswahili
shuleni, tunasubiri kwanza tuone namna ya kufanya,” alisema Profesa Mchome.
Aliongeza
kuwa Serikali inatambua changamoto zote zinazoikabili sekta ya elimu na ndiyo
maana ina mikakati ya kuboresha sekta hiyo, ili kukabiliana na changamoto
zilizopo. Alisema kwa sasa moja ya changamoto katika sekta hiyo ni pamoja na uhaba
wa walimu na vifaa.
Alifafanua
kuwa tayari katika nchi zilizoendelea, sekta ya elimu imekua, kiasi cha
matatizo kama walimu kuwa historia kwani mwalimu mmoja haijalishi yuko wapi,
anaweza kufundisha darasa kokote aliko kwa kutumia mitandao inayomwezesha
kuonana ana kwa ana na wanafunzi kupitia kompyuta kubwa.
Kwa
muda mrefu tangu uhuru, shule zote za msingi za Serikali zilikuwa zikitumia
Kiswahili kufundishia masomo yote isipokuwa somo la Kiingereza.
Baada
ya kumaliza shule ya msingi, mwanafunzi akiingia sekondari alikuwa akibadilisha
mfumo ghafla na kuanza kufundishwa masomo yote kwa Kiingereza isipokuwa somo la
Kiswahili.
Shule
za msingi za Serikali ambazo zilikuwa zikitumia Kiingereza kufundisha masomo
yote ni shule za msingi za Olympio na Diamond za Dar es Salaam na ya Arusha,
jijini Arusha.
Lakini
mwaka huu tayari shule ya Oysterbay ya Dar es Salaam, imeanza mchakato wa
kuhama kutoka Kiswahili kufundishia masomo yote na Kiingereza kuwa somo la kawaida,
mpaka kufundisha masomo yote kwa Kiingereza na Kiswahili kuwa somo la kawaida.
Mbali
na shule hiyo, Meya wa Manispaa ya Kinondoni, Yusuf Mwenda, alisema zipo shule
zingine Kinondoni, zimeshapeleka maombi kutaka kuhamia mfumo wa kufundisha
masomo yote kwa Kiingereza.
>>Habari leo
>>Habari leo
No comments:
Post a Comment