SIKU
moja baada ya Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) kutoa tamko la kumtaka aliyekuwa
Waziri Mkuu, Edward Lowassa, kuacha kukigawa chama kwa madai kuwa hana sifa
kuwa rais, mambo mazito yamezidi kuibuka huku ikitolewa orodha ya wanachama wa
CCM wakiwemo mawaziri, wabunge na makada maarufu wanaodaiwa kukisaliti chama
hicho.
Hatua
hiyo imeenda sambamba na kumtaka Katibu wa Umoja wa Vijana Uhamasishaji na
Chipukizi, Paul Makonda, kuacha kuwanyooshea vidole wenzao, wakati ndani ya
chama hicho kuna wasaliti wakubwa na wasiokuwa na usafi wowote wa kuwasema
wenzao.
Hayo
yamewekwa hadharani Dar es Salaam jana na aliyekuwa Mwenyekiti na mwanzilishi
wa CCJ Taifa, Richard Kiyabo, wakati akizungumza na waandishi wa habari kwenye
ukumbi wa mikutano Idara ya Habari (MAELEZO).
Kiyabo
aliitaka CCM kusafisha wanachama wasio waaminifu ambao ni mamluki wakiwemo
mawaziri, wabunge machachari na makada maarufu kutokana na kushiriki kwao
kuanzisha Chama Cha Kijamii (CCJ) huku bado hawajarejesha kadi za chama hicho.
Kiyabo
alisambaza kwa waandishi wa habari orodha ya wanachama wa CCM 37 anaodai
walishiriki kutoa michango ya fedha kwa ajili ya kufanikisha maandamano ya
amani ya CCJ yaliyolenga kupinga uonevu wa msajili wa vyama vya siasa nchini.
Alisema
tayari ameshamwandikia barua Makamu Mwenyekiti wa CCM (Bara) Philip Mangula
kukiomba chama kichukue hatua za kinidhamu na kimaadili kwa wanachama ambao si
waaminifu na tayari walikwishapoteza sifa za kuwa wanachama, kutokana na
kushirikiana nao kuanzisha CCJ, huku wakiwa wanachama wa CCM.
"Kitendo
cha kuwa wanachama wa vyama viwili kwa wakati mmoja ni kosa kubwa na ni usaliti
ndani ya chama, kosa hili halipishani na kosa la uhaini ndani ya chama, lakini
kwa masikitiko yangu makubwa watu hawa hadi sasa hawajaitwa na vikao vya chama
wala hakuna hatua yoyote iliyochukuliwa au kujadiliwa kwa makosa ya kukisaliti
chama na kuamua kuwa mamluki ndani ya chama," alisema Kiyabo.
Alisema
mwanzoni mwa mwaka 2010 walipokubaliana kuanzisha CCJ malengo makuu ilikuwa
chama hicho kushiriki uchaguzi mkuu na kusimamisha mgombea wa kiti cha urais na
wabunge, pamoja na madiwani kama wangekidhi matakwa ya kisheria.
"Nashangaa
ndani ya CCM bado kuna wanachama na viongozi waandamizi wana kadi mbili za CCJ
na CCM na wanashindwa kuzirudisha na hata kukana, ikiwemo kuwaomba radhi
wanachama kwa kitendo cha usaliti," alisema na kuongeza kuwa anawashangaa
baadhi ya wanachama ambao si waaminifu ndani ya chama.
Mbele
ya waandishi wa habari, Kiabo aliwataja waasisi hao wa CCJ na fedha
walizochangia kwenye mabano kuwa ni pamoja na Dk. Harrison Mwakyembe (sh
300,000), Samuel Sitta (sh 500,000), Anne Kilango (sh 400,000), Nape Nnauye (sh
100,000), Paul Makonda (sh 100,000) na James Lembel (sh 400,000) ambao kwa sasa
ni miongoni mwa wanachama wa CCM wanaotajwa kuwa na makundi ya urais.
Wengine
ni Amina Katemi (sh 300,000), Alex Kisumo (sh 300,000), Baraka Seif (sh
300,000), Sospeter Banigwa (sh 300,000), Saleh Omari (sh 300,000), Sarah
Patrick (sh 200,000), Daniel Mwaijojeli (sh 200,000), Dk. Ngonyani (sh
300,000), Elisha Eliya (sh 200,000), Emanuel Magonja (sh 200,000) na Asma
Watosha (sh 300,000).
Pia
wamo, Kulwa Lulelema (sh 50,000), Hamadi Maduku (sh 100,000), Flavian Nkya (sh
100,000), Gulam kutoka Zanzibar (sh 150,000), Hamad Ferej (sh 200,000), Ally
Harun (sh 50,000), Masudi Kangi (sh 100,000), Gumbo (sh 150,000), Idd Kiriwe
(sh 100,000), Innocent Makala (sh 200,000), Jacob Msambya (sh 200,000),
Ishelula (sh 150,000), Kipute (sh 200,000), Joseph Kashindye (sh 200,000)
Kamala Ng’ombe (sh 200,000) na Daniel Malongo (sh 50,000).
Alisema
ni vyema wakati huu kuelekea uchaguzi CCM ianze kujisafisha ili wale mamluki
waumbuke na wasipewe nafasi ya kugombea wakati ukifika
Makonda
alipoulizwa kuhusiana na madai hayo alijibu kuwa anaelewa kuwa mchezo huo
unachezwa na vibaraka kwani suala hilo halina uzito ndani ya chama.
Alidai
kuwa suala la kuondoa watu wanaotumiwa na Lowassa kukihujumu chama hicho
halijibiwi. Alisema ni muhimu kuelewa kuwa wapambe wote wa Lowassa watatoka na
watakapomalizika atashughulikiwa yeye kichama kwani ndiye tatizo.
“Wapambe
wote watoke na watakapoisha tutashughulika na bosi wao anayewatuma... ninajua
hawajajipanga ndiyo maana wamekurupuka na kuja na hoja rahisi," alisema.
Alisema
wanamtaka Lowassa akanushe kuwatumia hao watu. Kwa Nape, alisema
yalishajadiliwa na mjadala kufungwa ndani ya chama, hivyo madai hayo si mapya
hawezi kuyazungumzia.

No comments:
Post a Comment