TORONTO, Canada
MWANAMUZIKI, Justin Bieber
amefunguliwa mashitaka ya shambulizi dhidi ya dereva wa teksi
alilofanya mwezi mmoja uliopita mjini Toronto nchini Canada.
Habari kutoka nchini humo zilieleza
jana kuwa, Bieber aliwasili Kituo cha Polisi mjini Toronto na kulakiwa na
umati wa wapiga picha, waandishi wa habari na mashabiki hali ambayo iliwalazimu
polisi wa kituoni hapo kulazimika kutengeneza njia ili kumsindikiza,
Bieber aweze kupita mlangoni na kuingia ndani ya kituoni hicho.
Kwa mujibu wa taarifa za
Polisi, tukio hilo lilitokea baada ya dereva wa gari hilo kupeleka kundi
la watu sita kwenye klabu moja ya usiku mjini Toronto muda wa saa 9 alfajiri
Desemba 30 mwaka jana.
"Wakati dereva akiwapeleka watu
hao sita hotelini yalitokea mabishano kati ya dereva na mmoja wa
abiria," ilieleza sehemu ya taarifa hiyo ya polisi.. "Baada ya
mabishano hayo abiria mmoja alimpiga nyuma ya kichwa mara kadhaa
dereva hali ambayo ilimlazimisha kusimamisha gari na kuita
polisi,”iliongeza sehemu ya taarifa hiyo.
Taarifa za kituo cha televisheni cha
CTV, Bieber aliondoka kwenye kituo cha polisi mjini Toronto
usiku wa kuamkia jana na polisi wanasema kwamba anatarajia kurejea
kituoni hapo Machi 10 mwaka huu.
No comments:
Post a Comment