EBENEZA MARCH 9 2014

EBENEZA MARCH 9 2014

Thursday, January 16, 2014

EPZA yavuka malengo 2013

EPZA Dar es SalaamMAMLAKA ya Ukanda Maalumu wa Uwekezaji nchini (EPZA) imetangaza kuvuka malengo yake kwa mwaka 2013.
Mafanikio hayo yalitangazwa jijini Dar es Salaam jana na Mkurugenzi Mkuu wa EPZA, Dk. Adelhelm Meru, katika sherehe ya wafanyakazi ya kuuaga mwaka 2013 na kuukaribisha 2014.
“Pamoja na changamoto zilizopo hususan umeme, tunafurahi EPZA tumefanikiwa na kuvuka malengo tuliyokuwa tumejiwekea mwaka 2013,” alisema Dk. Meru alipozungumza na waandishi wa habari.

Akizungumzia baadhi ya vigezo walivyotumia kujipima katika mafanikio hayo, alisema mamlaka hiyo ilikuwa imejiwekea lengo la kupata wawekezaji wakubwa 25, lakini hadi kufikia mwishoni mwa mwaka jana walikuwa wamepata wawekezaji 31.
Pia alisema pamoja na kujiwekea malengo ya kuvutia mtaji wa dola milioni 300  za Marekani kwa mwaka jana, mamlaka hiyo ilivuka lengo na kuingiza nchini mtaji wa dola  milioni 498 ikiwa ni thamani ya fedha za wawekezaji walioingia nchini kwa mwaka huo.
Mkurugenzi huyo alisema EPZA ilikuwa imejiwekea lengo la kuzalisha ajira 5,200 kwa mwaka jana, lakini hadi kufikia Desemba jumla ya ajira 10,200 zilikuwa zimezalishwa kutokana na uwekezaji mpya uliofanywa kupitia mamlaka hiyo.
“Tumevuka lengo hili kwa mara mbili na hii inatupa faraja kuwa kazi inafanyika,” alisema.
Akifafanua zaidi alisema EPZA ilikuwa imejiwekea lengo la kuuza nje bidhaa zenye thamani ya dola milioni 100 lakini lengo lilivukwa na kufikia dola milioni 105.
Alisema mafanikio hayo yote ni matokeo ya kufanya kazi kwa bidii na kuwashukuru wafanyakazi wote wa EPZA kwa juhudi hizo.
Pia alishukuru serikali kwa msaada mkubwa inaoipa mamlaka hiyo katika kufanikisha malengo yake  na kwamba malengo ya mwaka 2014 huu ni kuvutia zaidi wawekezaji katika maeneo maalumu ya uwekezaji.
SOURCE:TANZANIA DAIMA

No comments:

Post a Comment