EBENEZA MARCH 9 2014

EBENEZA MARCH 9 2014

Thursday, January 16, 2014

Mradi DART wapata nguvu mpya

MRADI wa mabasi yaendayo kasiMRADI wa mabasi yaendayo haraka umepiga hatua nyingine baada ya kupatikana kampuni ya washauri itakayofanya kazi ya kupatikana watoa huduma muhimu kwa mradi huo unaotarajiwa kuanza mwishoni mwa mwaka huu.
Hatua hiyo imefikiwa baada ya Kampuni ya REBEL Group ya Uholanzi kushinda zabuni na kusaini mkataba wa kufanya kazi na Wakala wa Mabasi yaendayo haraka (DART).
Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu, Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Jumanne Sagini, aliyeshuhudia utiaji saini huo aliwaambia waandishi wa habari baada ya kusainiwa kwa mkataba huo kuwa mradi huo sasa unaelekea hatua za mwisho kuanza kufanya kazi za usafiri wa Jiji la Dar es Salaam.
Kampuni hiyo iliyosaini mkataba na DART ilishinda zabuni miongoni mwa kampuni sita zilizoingia katika hatua ya mwisho ya ushindani huo.

Kwa upande wa kampuni hiyo mkataba huo ulisainiwa na Mshauri wa masuala ya fedha, Guillaume Remy, wakati DART iliwakilishwa na Kaimu Ofisa Mkuu Mtendaji, Asteria Mlambo.
“Hatua hii ni muhimu kwa mradi huu nyeti kwa nchi yetu,” alisema katibu mkuu huyo.
Wadau wengine watakaoshiriki katika mchakato huo ni pamoja na DART wenyewe, watoa huduma za daladala na wananchi wote katika kufanikisha jambo hilo.
“Tumewaambia wenzetu wa kampuni hii kuwa kazi hii ni nzito lakini lazima tushinde kwa ajili ya kutoa usafiri mzuri kwa wananchi,” alisema na kuongeza suala hilo litasaidia kukabiliana na changamoto ya foleni jijini Dar es Salaam.
Aliitaka kampuni hiyo kuhakikisha inafanya kazi hiyo vizuri na kuwa serikali ipo tayari kutoa msaada pale zitakapojitokeza kero ambazo ni kikwazo kwa utekelezaji.
Alisema mradi huo unatekelezwa kwa ushirikiano wa sekta ya umma na binafsi (PPP) ambapo sekta binafsi itawekeza dola milioni 180 na sekta ya umma dola milioni 250.
Ofisa Mwandamizi kutoka kampuni hiyo ya Rebel Group, Jeroen Kok, alisema kampuni yao ipo tayari kufanya kazi iliyoomba, ili kusaidia Tanzania kupata huduma ya kisasa ya usafiri na kupunguza foleni ambayo ni kero kubwa.
Naye Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Daladala Mkoa wa Dar es Salaam (DARCOBOA), Sabri Mabruki, alisema mradi huo ni mkubwa na utasaidia katika kufikia malengo ya serikali katika sekta ya usafirishaji jijini Dar es Salaam.
SOURCE TANZANIA DAIMA

No comments:

Post a Comment