Wapiganaji wa kundi la Mai-Mai waliojisalimisha na kuweka silaha chini
jimboni Kivu ya Kaskazini nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, wameanza
kupatiwa mafunzo ya kuwa askari chini ya uongozi wa serikali.
Waziri wa mambo ya ndani wa nchi hiyo Rishali
Muyeji ametembelea takribani vijana elfu moja na mia mbili, kando ya mji wa
Goma Mashariki mwa nchi hiyo ambao wameanza kupatiwa mafunzo hayo.Waziri Muyeji aliyewatembelea vijana hao kwenye mji wa Bweremana Magharibi mwa Goma amewapongeza kwa kuitika wito wa raia na serikali ya Congo kwa uamuzi wa kuacha uasi na kuweka silaha chini.
Aidha vijana hao baada ya kuacha uasi, wametoa mahitaji yao kwa waziri Muyeji kuwa wanahitaji mavazi, mahali pa kulala na chakula jambo ambalo waziri amesema kuwa rais Kabila ameandaa mpango wa kuhakikisha wanapata mahitaji hayo.
Hadi sasa jumla ya vikundi ishirini na tano vimetoa watu takribani 1002, kujiunga na kambi ya mafunzo ya kuwa raia wa kawaida, ama kujiunga na jeshi huku vikundi vingine navyo vikiendelea kuweka silaha chini.
No comments:
Post a Comment