Maandalizi ya Bunge Maalumu la Katiba yanazidi
kupamba moto na sasa mafunzo kwa wabunge yameanza kutolewa jinsi ya kuichambua
Rasimu ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 2013 katika Bunge
hilo linalotarajiwa kuanza mwezi ujao.
Mafunzo hayo yalianza kutolewa jana kwa kundi la kwanza la wabunge, ambao ni wajumbe wa kamati sita za kudumu za Bunge, katika Ofisi Ndogo za Bunge, jijini Dar es Salaam, na wataalamu kutoka Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) na Chuo Kikuu cha Mzumbe. Mafunzo hayo yanatolewa kupitia semina maalumu iliyoandaliwa na Bunge kupitia Mradi wake wa Kuwajengea Uwezo wa Wabunge (LSP) kwa kushirikiana na Shirika la Mpango wa Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP). Wabunge walioanza kupewa mafunzo hayo ni wajumbe wa kamati za kudumu za Bunge za Kilimo, Mifugo na Maji; Katiba, Sheria na Utawala; Fedha na Uchumi; Huduma za Jamii; Mambo ya Nje na Miundombinu.
Mwenyekiti wa Kamati ya
Kudumu ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala, Pindi
Chana, aliwaambia waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam kuwa,
semina
hiyo inalenga kuwajengea wabunge uwezo wa kuelewa namna ya kuichambua
Rasimu ya
Katiba, na kwamba itafanyika kwa awamu tofauti. Kamati nyingine za
Kudumu za Bunge, ambazo wajumbe wake wanatarajiwa kupewa pia
mafunzo kupitia semina hiyo, ni ya Uongozi; Kanuni za Bunge; Haki,
Maadili na
Madaraka ya Bunge na ya Masuala ya Ukimwi. Nyingine ni Sheria Ndogo;
Viwanda na Biashara; Ulinzi na Usalama; Maendeleo ya
Jamii; Ardhi, Maliasili na Mazingira; Hesabu za Serikali na Hesabu za
Serikali
za Mitaa. Chana alisema kutokana na hatua ya mchakato wa mabadiliko ya
Katiba
iliyofikiwa, wananchi wenye maoni wayapeleke kwa wawakilishi wao
(wabunge),
ambao nao wataziwasilisha katika Bunge Maalumu la Katiba. Aidha, alisema
baada ya Bunge hilo itaitishwa kura ya maoni ambayo inaweza
kupigwa mara mbili iwapo zaidi ya asilimia 50 ya wananchi wa Tanzania
Bara na
asilimia 50 ya wananchi wa Zanzibar zinazotakiwa, hazitafikiana katika
kuipitisha Rasimu ya Katiba. Pia alisema iwapo mara zote mbili, kiwango
hicho cha asilimia hakitafika, kuna
haki ya kuitisha tena Bunge Maalumu la Katiba kwa ajili ya kuijadili
upya
Rasimu ya Katiba kabla ya kuirudisha kwa wananchi ili kupigiwa kura ya
maoni. Maandalizi ya Bunge hilo yanafanyika wakati Tume ya Mabadiliko ya
Katiba
ikiendelea na kazi ya kuchambua maoni ya mabaraza ya katiba ya wilaya,
asasi
mbalimbali na makundi maalumu. Tume hiyo inayoongozwa na Waziri Mkuu
mstaafu, Jaji Joseph Warioba, yenye
wajumbe 30; wakiwamo 15 kutoka Tanzania Bara na 15 kutoka Zanzibar,
ilitangazwa
na Rais Jakaya Kikwete, Aprili 6 na kuapishwa Aprili 13, mwaka jana.
Ilianza kazi ya kukusanya maoni ya wananchi Mei mosi, mwaka jana. Baada
ya kukamilisha kazi hiyo, iliyachambua na kuandika Rasimu ya Katiba.
Kazi ya kukusanya maoni hayo iliwahusisha wananchi mmoja mmoja kupitia
mikutano
ya hadhara na ilikamilishwa na Tume Desemba, mwaka jana. Baadaye Tume
ilikutana na makundi maalumu na watu mashuhuri, wakiwamo viongozi
wakuu wastaafu na waliopo madarakani, kati ya 7-28, mwaka huu. Bunge
hilo ambalo litachukua siku 70 litaundwa na wajumbe takribani 600
wakiwamo Wabunge wa Bunge la Jamuhuri ya Muungano, Wajumbe wa Baraza la
Wawakilishi Zanzibar na wajumbe kutoka makundi mbalimbali ya kijamii
166.
No comments:
Post a Comment