Kufuatia ugunduzi wa mafuta na gesi katika mikoa ya
kusini ya Lindi na Mtwara, serikali imewaalika wafanyabishara na wawekezaji
kutoka nchini Finland, kuja kuwekeza hapa nchini hususani katika mikoa hiyo,
ili kuweza kutoa fursa ya kukua kiuchumi kwa wananchi wa mikoa ya kusini.
Kauli hiyo ya serikali imetolewa na Waziri wa Nchi Ofisi
ya Rais Utawala Bora George Mkuchika, wakati akizungumza na mabalozi wa Finland
Afrika, katika maadhimisho ya miaka 40 ya ushirikiano kati ya Finland na mikoa
ya Lindi na Mtwara, sherehe zilizofanyika katika ukumbi wa Veta Mjini Mtwara.
Amesema kuwa uwekezaji huo unaweza kufanyika katika
maeneo ya uzalishaji wa umeme, viwanda, usafirishaji, kilimo, madini,
miundombinu, ambapo amesema kuwa kwa kufanya hivyo wananchi wa mikoa ya Lindi
na Mtwara nao watapata fursa za kupata ajira na kujiongezea kipato na hivyo
kujinasua na lindi la umasikini.
Mkuchika amesema kuwa misaada ya serikali ya Finland
imekuwa ikilenga katika sekta tatu za
ushirikiano ikiwemo sekta ya uvuvi, mazingira na kilimo na kusaidia bajeti ya
Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI).
Waziri huyo amesema kuwa katika maeneo yote hayo ya sekta
za ushirikiano, mkazo mkubwa umewekwa katika kupunguza umasikini na kuimarisha
demokrasia, utawala bora, utawala wa sheria na sera endelevu za maendeleo
katika misingi ya umoja wa mataifa ya malengo ya maendeleo ya millennia.
Awali akizungumza katika sherehe hizo za miaka 40 ya
ushirikiano kati ya Finland na Mikoa ya Lindi na Mtwara, kaimu mkuu wa mkoa wa
Mtwara Ludovick Mwananzila, ambaye ni mkuu wa mkoa wa Lindi amesema kuwa hivi
sasa fursa ni nyingi katika mikoa ya kusini kufuatia kufunguka kwa miundo mbinu
ya barabara na hivyo kufanya shughuli za kibiashara na za kiuwekezaji
kuongezeka kwa wananchi.
No comments:
Post a Comment