EBENEZA MARCH 9 2014

EBENEZA MARCH 9 2014

Thursday, November 27, 2014

CCM YAVUNJIKA SASA WABUNGE WAGAWANYIKA TENA MBELE YA MANGULA

Philip Mangula
Kashfa ya kampuni ya Independent Power Limited (IPTL) ya uchotwaji wa zaidi ya Sh. bilioni 300 kwenye akaunti ya Tegeta Escrow, iliyoko Benki Kuu (BoT) imewagawa wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mbele ya Makamu Mwenyekiti wa chama hicho Tanzania Bara, Philip Mangula.

Hali hiyo ilijitokeza katika kikao cha wabunge wa CCM, kilichofanyika mjini hapa juzi usiku na kuhudhuriwa na Mangula.

Habari zilizopatikana mjini hapa zinaeleza kuwa, Mangula anadaiwa kuhudhuria kikao hicho akitekeleza maelekezo aliyopewa na ngazi ya juu ya uongozi wa chama kufanya hivyo ili kuwaweka sawa wabunge.

Kwa mujibu wa habari hizo, maelekezo hayo yalitolewa kwa Mangula baada ya Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, ambaye awali alitakiwa yeye kushiriki, kukwama kutokana na ubovu wa miundombinu uliopo katika eneo alikokuwa juzi.

Kinana anaendelea na ziara zake za kukiimarisha chama na kukagua utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya 2010-15 na hadi jana alikuwa katika vijiji vilivyoko mkoani Mtwara.

Vyanzo mbalimbali kutoka ndani ya kikao hicho kilichofanyika juzi usiku vinaeleza kuwa mgawanyiko wa wabunge hao ulitokana na baadhi yao kutaka watu, wakiwamo mawaziri na wabunge wa CCM watakaobainika kuhusika na kashfa hiyo wawajibike na wengine kupinga.

Hata hivyo, vyanzo hivyo vinaeleza kuwa katika mgawanyiko huo, Mangula alikuwa upande wa wabunge wanaotaka watu watakaobainika kuhusika na kashfa hiyo wawajibike.
Chanzo kimoja kinasema sababu zilizotolewa na kundi la wabunge wenye msimamo huo ni kuwa hatua hiyo itasaidia kukisafisha chama dhidi ya matope, ambayo kimepakwa tangu kashfa hiyo iibuliwe bungeni.

Kinasema sababu zilizotolewa na wabunge wanaopinga suala hilo ni kwamba, hatua ya watuhumiwa kuwajibika itakichafua zaidi chama, kwani itawafanya watu waamini kuwa chama hicho ni cha mafisadi.

Habari zinasema kuwa hali hiyo ilisababisha kuzuka mvutano mkubwa kati ya makundi hayo mawili katika kikao hicho, huku kila moja likijitahidi kutumia kila aina ya ufundi kujenga hoja zake dhidi ya lingine.

Kundi linalopinga watuhumiwa kuwajibika, linadaiwa kutiwa chachu na Mbunge mmoja anayetoka katika moja ya majimbo yaliyoko mkoani Pwani.

Habari zaidi zinaeleza kuwa mbali na makundi hayo mawili kuvutana, kikao hicho kilitoa fursa kwa Waziri wa Nishati na Madini, Prof. Sospeter Muhongo na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Jaji Frederick Werema,  kujitetea.

Habari zinasema katika utetezi wake, Werema alida kuwa taratibu zote za utoaji fedha kwenye akaunti hiyo zilifuatwa na kuwashangaa wabunge kwa kuwa waoga, kwani yeye siyo mwoga na hawezi kujiuzulu.

“Jaji Werema alisema kuwa yeye hawezi kuwajibishwa na Bunge na yeye maumbile yake siyo mtu wa kuogopa. Mwenye mamlaka ya kumwajibisha ni aliyemteua na si vinginevyo," kilisema chanzo kingine.

Kwa upande wake, Prof. Muhongo alitumia fursa huo kujikita zaidi katika kusimulia namna IPTL ilivyoingia nchini hadi kufikia hatua ya sasa.

Inaelezwa kuwa Muhongo alisema hawezi kujiuzulu na yupo tayari kujitetea na kuichambua taarifa ya CAG na PAC.

Habari zinaongeza kwamba Muhongo alidai kuwa taarifa zote hizo mbili hazina ukweli wowote, hivyo yeye na wakurugenzi wa Tanesco wapo mjini hapa kwa ajili ya suala hilo na muda wowote wakiitwa kwa ajili ya utetezi watafanya hivyo.

Baada ya kusema hivyo, Mangula alisema waliyoyaeleza yamesikika, hivyo akatoa nafasi kwa wabunge kutoa michango yao kwenye hilo.Mbunge wa Simanjiro, Christopher Ole Sendeka, aligomea kuchangia maelezo hayo ya Prof. Muhongo na Jaji Werema.

Sendeka alihoji inakuwaje waanze kujitetea wakati ripoti ya ukaguzi wa hesabu za fedha hizo ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) haijafika bungeni?
Mjadala huo ulifungwa, huku Mangula akisisitiza kuwa huko nje chama kimechafuka ikizingatiwa kinaelekea katika chaguzi mbalimbali, ukiwamo wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji unaotarajiwa kufanyika Desemba 14, mwaka huu na uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.

Kwa mujibu wa habari hizo, Mangula alikata shauri kwa kusema kuwa hakuna njia nyingine ya kukisafisha chama isipokuwa kila atakayebainika kuhusika na kashfa hiyo awajibike.

KUMNUSURU PINDA
Kikao kingine cha wabunge wa CCM kilikutana jana mchana bila kufikia muafaka, lakini habari kutoka vyanzo mbalimbali, zinaeleza kuwa waliafikiana kumnusuru Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.

Uamuzi huo ulifikiwa kwa lengo la kuilinda serikali kwa kuwa kumwajibisha Pinda ambaye ni kiongozi wa shughuli za serikali bungeni, kungesababisha serikali nzima kuvunjika.

AMRI YA MAHAKAMA YACHAFUA BUNGE
AMRI ya juzi ya Mahakama Kuu ya Tanzania kanda ya Dar es Salaam kulizuia Bunge kujadili taarifa ya maalumu ya Kamati ya Bunge Hesabu za Serikali (PAC) kuhusu ripoti ya uchunguzi wa kashfa ya kampuni ya IPTL ya uchotwaji wa zaidi ya Sh. bilioni 300 kwenye akaunti ya Tegeta Escrow, iliyoko Benki Kuu ya Tanzania (BoT) jana lilibua mzozo mkali bungeni.

Hali hiyo ilijitokeza baada ya kipindi cha maswali na majibu wakati wabunge walipoomba miongozo kutaka kujua kama majadala kuhusu taarifa hiyo ya PAC ingesomwa au la, kufuatia zuio hilo la mahakama.

Hata hivyo, wakati wabunge hao wakitaka kujua hilo, ratiba ya shughuli za jana za Bunge, ilionyesha kuwa taarifa hiyo ya PAC ingesomwa baada ya hati kuwasilishwa mezani.

SELEMANI NCHAMBI
Mbunge wa Kishapu (CCM), Selemani Nchambi, mbali na kutaka mjadala wa taarifa ya PAC uendelee, alikituhumu Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kwa kitendo cha mwanasheria wake na mjumbe wa kamati kuu, Mabere Marando, kuwa miongoni mwa mawakili waliopeleka pingamizi mahakamani kuzuia mjadala kuhusu kashfa hiyo.

Nchambi alisema kampuni ya uwakili iliyokwenda kupinga suala hilo kujadiliwa na Bunge Marando ni mwanahisa wake, ambaye pia ni mjumbe wa Mkutano Mkuu wa Chadema na pia ni mjumbe wa Kamati Kuu (CC) ya Chadema.

”Sisi sote tunataka suala hili lijadiliwe kwa umakini. Watanzania wana kiu ya kusikia habari nzito ya suala hili kupitia Bunge hili, hapo hapo wakili huyu, ambaye ni mjumbe wa CC ya Chadema ndiye aliyekwenda kupinga suala hili kujadiliwa bungeni,” alisema Nchambi.

Aliongeza: “Naomba Watanzania waelewe kwamba, sisi wabunge wa CCM tunayo dhamira ya dhati ya kujadili jambo hili bungeni. Kwa kuwa Chadema wameonyesha waziwazi kupitia mjumbe wao kuwa wanapinga suala hili, naomba mwongozo wako ili wakati tunajadili suala hili zito, tujadili pia kitendo cha mwanasheria wa Chadema kwenda kupinga suala hili lisijadiliwe bungeni.”

Kauli hiyo ilisababisha wabunge wengi wao wakiwa ni wa upinzani kuanza kumzomea Nchambi, huku wengine wakisikika wakisema kuwa amepewa fedha.
Hali hiyo ilitulizwa na Mwenyekiti wa Bunge, Mussa Zungu, baada ya kuwataka wabunge kutulia, wamvumilie na pia kutishia kusitisha shughuli za Bunge iwapo wangeendelea kuleta zogo bungeni.

TUNDU LISSU
Mwongozo huo wa Nchambi ulijibiwa na Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu, ambaye alisema wakili wa Kampuni ya Pan African Power Solutions ndiye aliyefungua kesi juzi Mahakama Kuu.

“Wakili huyo anaitwa Gabriel Mnyele, ni mkazi wa Mpanda na ni mwana CCM. Kwa wasiomfahamu, mimi nimesoma naye, ndiye aliyeua mke wake halafu kesi yake ikafutwafutwa,” alisema Lissu.

Aliongeza: “Ni kweli kwamba, Mnyele anafanya kazi kwenye kampuni moja ya uwakili na Mabere Marando, isipokuwa Wakili Marando hajahusika vyovyote vile na kesi iliyopelekwa mahakamani na Mnyele.”

Akizungumzia kuhusu zuio la Mahakama Kuu, Lissu alisema kitendo hicho hakijawahi kutokea tangu Mahakama Kuu ya Tanganyika ianzishwe mwaka 1922.“Kilichotokea jana (juzi) ni shambulio la moja kwa moja na wazi la mamlaka, uhuru na hadhi ya Bunge hili,” alisema Lissu.

Aliongeza: “Ibara ya 4 (1,2) ya Katiba ya Jamuhuri ya Muungano iliweka mgawanyo wa madaraka kati ya Bunge, Serikali na Mahakama.”

“Bunge lako tukufu lina uhuru wa majadiliano na uhuru huo hauwezi ukaingiliwa na chombo chochote, na mahakama yoyote kwa mujibu wa ibara ya 100. Hivyo, Bunge hili liendelee na mjadala wa taarifa ya PAC.”

OLE SENDEKA
Mbunge wa Simanjiro (CCM), Christopher Ole Sendeka, alisema Ibara ya 100 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inasema kutakuwa na uhuru wa mawazo, majadiliano na utaratibu katika Bunge.

“Uhuru huo hautavunjwa wala kuingiliwa na chombo chochote katika Jamhuri ya Muungano au katika mahakama au mahali pengine nje ya Bunge,” alisema Sendeka.

Aliongeza: “Watanzania macho yao yote yapo hapa, wanasubiri ripoti ya PAC iingizwe bungeni, wanasubiri Bunge hili liweze kutenda haki kwa wahalifu dhidi ya raslimali za nchi, wanasubiri Bunge hili liungane bila mpasuko wa kambi za vyama vya siasa.”

“Watanzania wanasubiri vielelezo vilivyoambatanishwa na Kamati ya PAC, wanasubiri kusikia aliyeweza kuingia na dola laki tatu, akastahili kulipwa mtambo wa mabilioni na bilioni 306 wakati ameweka dola laki tatu, wanataka majibu hapa bila ushabiki wa chama.”

“Mheshimiwa Mwenyekiti, tuendelee na mjadala usiruhusu mjadala usio na msingi kuendelea.”

KHALIFA SULEIMAN
Mbunge wa Gando (CUF), Khalifa Suleiman Khalifa, aliwataka wabunge kutokuwa na hofu kuhusu suala hilo kujadiliwa bungeni kwa kuwa Spika wa Bunge, Anne Makinda, alishatoa uamuzi wake juzi.

“Waheshimiwa wabunge, tuna wasiwasi wa nini kama kuna mtu kaenda mahakamani, kaenda msikitini au kanisani, Bunge litajadili. Tunahofia nini kupoteza wakati kuuliza? Sisi tunachosubiri hapa ripoti iletwe hapa tujadili,” alisema Khalifa.

DEO SANGA
Mbunge wa Njombe Kaskazini (CCM), Deo Sanga, alisema Spika alishasema taarifa ya mahakama haipo na kutaka mjadala uendeleee hata kama taarifa hiyo itapelekwa.
Mbunge wa Longido,Lekule Laizer (CCM) Mbunge wa Longido (CCM), Michael Lekule Laizer, alisema haoni sababu ya mjadala wa miongozo kuendelea kuwapo wakati ratiba ya jana ya shughuli za Bunge tayari ilishaonyesha kwamba, taarifa ya PAC ingesomwa jana.

JOSHUA NASSARI
Mbunge wa Arumeru Mashariki (Chadema), Joshua Nassari, alimtaka Mwenyekiti wa Bunge kutumia busara na kulielekeza Bunge kuacha kutaja vyama vyao vya siasa, badala yake wajadili fedha za wananchi zilizoibwa.

“Ripoti iletwe, tuanze mjadala. Watanzania wanataka kujua kina nani wamekula pesa na kina nani wanawajibika,” alisema Nassari.

ESTHER BULAYA
Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Esther Bulaya, alisema mahakama zinatumika vibaya na kwamba, Bunge halitakubali kutii amri hiyo ya kusitisha mjadala.“Narudia tena, Bunge hili halitakubali mahakama kutumika vibaya, waliofungua kesi ndiyo hao wanaotuhumiwa,” alisema Bulaya.

Aliongeza: “Mimi ni mbunge wa Chama Cha Mapinduzi, siwezi kumlinda waziri aliyechukua hela wakati kuna watu kule wanakosa Sh. 50,000 ya kuchangia maabara, siwezi kufanya hivyo.”

MUSSA ZUNGU
Akijibu baadhi ya miongozo, Mwenyekiti wa Bunge, Mussa Zungu, aliwataka wabunge kutokuwa na wasiwasi kwa kuwa taarifa hiyo ipo kwenye ratiba na hati ilishawasilishwa mezani.

“Hati ikishawasilishwa mezani maana yake tayari ni ‘public document’ (waraka wa umma). Hadi sasa taarifa ya kiti bado Bunge haijapokea barua yoyote ya kukataza mjadala wa Escrow kujadiliwa bungeni, miongozo mingine nitajibu jioni,” alisema Zungu na kisha akasitisha shughuli za asubuhi hadi jioni.

WAKESHA KULINDA TAARIFA YA PAC
Katika hatua nyingine, wajumbe wa PAC, wakiongozwa na Mwenyekiti wao, Zitto Kabwe, juzi walikesha kulinda nyaraka za taarifa ya kamati hiyo kuhusu kashfa ya IPTL baada ya kuhofu kwamba, ingeibwa.

Hilo lilithibitishwa na Makamu Mwenyekiti wa PAC, Deo Filikunjombe, na wajumbe; Abdul Marombwa (Kibiti-CCM) na Amina Mwidau (Viti Maalumu-CUF).

FEDHA ZAMWAGWA KUWAHONGA WABUNGE
Pia habari za kuaminika zinaeleza kuwa mmoja wa wabunge alionekana akigawa fedha kqa wabunge wenzake kati ya Sh milioni mbili, tano hadi milioni 50 kuwashawishi wapinge Bunge kujadili kashfa ya IPTL na kama litajadili wahakikishe wanawakingia kifua wote watakaobainika kuhusika ama katika kuchotama kupata mgawo wa fedha za akaunti ya Tegeta Escrow.

Imeandikwa na Muhibu Said na Editha Majura, Dodoma.

CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment