EBENEZA MARCH 9 2014

EBENEZA MARCH 9 2014

Tuesday, July 15, 2014

CCT YAMUWASHIA MOTO RAIS KIKWETE KUHUSU KATIBA MPYA


Rais Jakaya Kikwete 
Dar es Salaam. Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) imetoa tamko zito ikieleza kushangazwa na kauli ya Rais Jakaya Kikwete ya kupinga mapendekezo yaliyomo katika Rasimu ya Katiba iliyotokana na maoni ya Watanzania na kusema kitendo hicho kimeishusha hadhi Tume ya Mabadiliko ya Katiba aliyoiteua.
Tamko hilo la CCT ni mwendelezo wa lawama ambazo Rais Kikwete amekuwa akitupiwa na taasisi na watu mbalimbali kutokana na mchakato wa kuandika Katiba Mpya kwenda mrama baada ya mkuu huyo wa nchi kueleza maoni yake dhidi ya mapendekezo ya muundo wa Serikali ya Muungano wakati akilihutubia Bunge la Katiba.
Miongoni mwa watu waliojitokeza kuzungumzia kauli hiyo katika siku za karibuni ni aliyekuwa Msajili wa Vyama vya Siasa, John Tendwa, maaskofu wa Kanisa Katoliki, katibu mkuu wa Chadema, Dk Willbrod Slaa na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Seif Sharrif Hamad.
Jana, CCT iligongomea msumari juu ya lawama hizo ikifananisha kauli ya kiongozi huyo aliyoitoa Machi 21, mwaka huu wakati akifungua Bunge Maalumu la Katiba mjini Dodoma na mama anayeamua kubeba mimba na kujifungua kwa uchungu, kisha kumtelekeza mtoto, badala ya kumfurahia.
Pia katika tamko lake (limechapishwa kwa ukamilifu Uk. 36 wa gazeti hili), jumuiya hiyo imewataka wajumbe wa Bunge hilo kuheshimu maoni ya Watanzania yaliyomo katika Rasimu ya Katiba na kuacha kujadili maoni ya vyama vyao vya siasa.
“Inashangaza jinsi chama kimoja cha siasa kinavyolazimisha wabunge na wanachama wake kukubaliana na mapendekezo yake ambayo yanapingana wazi na yaliyomo katika rasimu ya Katiba,” linaeleza tamko hilo lililotolewa baada ya Mkutano wa 48 wa Halmashauri Kuu ya Jumuiya hiyo uliofanyika Julai 2 na 3 mjini Dodoma.
Tamko hilo pia limetaja mambo mengine saba yanayolikabili Taifa.

Kabla ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba, iliyokuwa ikiongozwa na Jaji Joseph Warioba kutoa rasimu ya pili ya Katiba Desemba 30, CCM ilisambaza waraka kuwaarifu wajumbe wa Bunge la Katiba kutoka CCM kuwa msimamo wa chama hicho tawala ni Muungano wa serikali mbili, tofauti na mapendekezo ya wananchi yaliyo kwenye rasimu hiyo ambayo yanataka serikali tatu.
Licha ya mara kadhaa Jaji Warioba kutetea kile kilichopendekezwa na Tume yake, wajumbe hao kutoka CCM wameyapinga maoni hayo na kusisitiza kuwa yanaweza kubadilishwa kadri Bunge la Katiba litakavyoona inafaa.
Kitendo hicho kilisababisha wajumbe kutoka vyama vingine kuunda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), ambao Aprili 16 uliamua kususia vikao vya Bunge hilo ukitoa masharti kuwa utarejea bungeni kama chombo hicho cha kuandika Katiba kitajikita kujadili mapendekezo ya wananchi kama yalivyowasilishwa na Tume ya Jaji Warioba.
Bunge hilo litaendelea na vikao vyake Agosti 5 na mwenyekiti wake, Samuel Sitta anahaha kushawishi Ukawa walegeze msimamo wao.
Katika hotuba yake ya kufungua Bunge la Katiba, Rais Kikwete aligusia mambo kadhaa yaliyomo katika Rasimu ya Katiba na kutaka yatazamwe kwa kina, huku akibainisha kuwa mengine hayawezekani kutekelezeka, ikiwa ni pamoja na muundo wa serikali tatu kwa maelezo kuwa idadi ya watu waliotaka muundo huo ni ndogo.
SOURCE>>>MWANANCHI

No comments:

Post a Comment