EBENEZA MARCH 9 2014

EBENEZA MARCH 9 2014

Tuesday, February 11, 2014

sumaye aipa somo serikali ya TZ

0
Share

Mwanza. Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye ameonya kuwa iwapo kutakosekana mipango ya kuimarisha hali ya uchumi wa nchi , Taifa linaweza kujikuta likitumbukia kwenye janga la mifarakano kutokana na vijana wengi kukabiliwa na tatizo la ukosefu wa ajira.
Akizungumza kwenye kongamano lililoandaliwa na Chuo cha Biashara (CBE) Mwanza, Sumaye alisema pamoja na kwamba tatizo la ajira ni janga linaloendelea kuzikabili nchi nyingi duniani ikiwamo Tanzania, Serikali inapaswa kuweka mikakati ya dhati kukabiliana na hali hiyo.
Kongamano hilo lililohudhuriwa na jumuiya ya chuo hicho na wananchi, lilijadili mada iliyopewa jina la “Maendeleo ya Vijana na Tatizo la Ajira”.
Sumaye alisema inawezekana kukawa na njia za kurekebisha hali hiyo, lakini jambo kubwa linalopaswa kuzingatiwa na serikali ni kuwa na mikakati ya ujenzi na ukuzaji uchumi imara.
“Uchumi dhaifu huzaa nchi maskini ambayo watu wake huishi katika mazingira magumu na serikali husika haiwezi kuwa na uwezo wa kutoa huduma muhimu kwa watu wake kwa viwango vinavyotakikana’ Alisema.
Alisema uchumi dhaifu pia huweza kuhatarisha usalama wa nchi kwa kuwa ni rahisi kusababisha mifarakano na wananchi kuichukia serikali yao.
Alisema kuwa kumekuwa na jitihada mbalimbali za kuwakwamua vijana ili kuondokana na hali duni za maisha, lakini jambo linalopaswa kuzingitiwa sasa ni kutoa elimu kwa vijana hao pamoja na wananchi kwa ujumla ili waweza kukabiliana na changamoto zinawazunguka.
“Suala uelimishaji wa wananchi hasa vijana wanaokua ni la msingi katika kujenga uchumi utakaomudu ushindani katika nyanja mbali mbali za sayansi na teknologia na biashara za kimataifa.
Nchi nyingi zilizopata maendeleo ya haraka ziliwekeza katika elimu yenye malengo hasa katika eneo la sayansi na teknolojia. Tukiamua kuwekeza katika elimu isiwe bora elimu bali tuhakikishe tunatoa elimu ya viwango vinavyokubalika na siyo elimu ya kujitafutia sifa isiyo na viwango” alisema.
Pia alihimiza haja ya kuendelea kuwepo ushirikiano wa karibu baina ya serikali na sekta binafsi akisema kuwa pasipo kuwepo hali hiyo suala la kuwa na uchumi endelevu linaweza kuwa ndoto kutokana na kila upande kuwa ni mchango mkubwa wa uendelezaji wa jamii.
source: mwananchi

No comments:

Post a Comment