EBENEZA MARCH 9 2014

EBENEZA MARCH 9 2014

Tuesday, February 25, 2014

SIMBA SC YAUMBUKA KOCHA ZDRAVICKO AWEKA KILA KITU HADHARANI SABABU ZA WAO KUPOTEZA MICHEZO YAO

INADAIWA kuwa chanzo cha Simba kufanya vibaya katika mechi za Ligi Kuu ni ukali wa kocha pamoja na ukata.
Simba imekuwa haina mwenendo mzuri tangu kuanza kwa mzunguko wa pili wa Ligi Kuu, na juzi ilifungwa mabao 3-2 na JKT Ruvu, matokeo yaliyowashangaza wengi hasa kwa vile Ruvu ilifungwa mabao 6-0 dhidi Prisons katika mechi iliyopita.
Habari za uhakika kutoka kwa wachezaji wa Simba ambao hawakutaka majina yao yaandikwe gazetini zinadai kuwa, kocha Zdravko Logarusic tangu kupewa timu hiyo amekuwa mkali kwa wachezaji na asiyetaka kusikiliza ushauri wa benchi lake la ufundi.
Matokeo ya Simba ya juzi, imewafanya kuwa kwenye wakati mgumu katika kushiriki michuano ya kimataifa mwakani, kwani endapo hali itaendelea hivi katika mechi zilizosalia, inaweza isiambulie kitu.
“Sio siri hatukupenda kufungwa na Ruvu, lakini kiukweli wachezaji hatuna morali, tunacheza tu kwa vile tumesajili timu hii,” alisema mmoja wa wachezaji hao.
“Unajua lazima tuseme ukweli, uongozi hautulipi maslahi yetu, tumekuwa watu wa kuishi kwa kubangaiza, ukija uwanjani napo kocha anakufokea kama mtoto mdogo, morali hiyo utaitoa wapi mchezaji?” Alihoji mchezaji huyo.
“Kocha amekuwa mtu wa kutugombeza kila kukicha, bila kujua kama wachezaji wake tunaishi
kwenye mazingira magumu, yeye akifika uwanjani ukikosea kidogo anagomba tu, anatufanya kama watoto wadogo wakati sisi ni watu wazima mpira ndio ajira yetu, kwanini tufanya makosa makusudi, mambo mengine ni bahati mbaya tu,” alisema mchezaji mwingine.
“Na ukumbuke kuwa kocha huyo hatugombezi peke yake, anatutolea hadi lugha ya matusi, kiukweli kabisa timu yetu haina morali,” alisema.
Aidha, wachezaji hao wamelalamika kitendo cha kocha kuwaweka nje baadhi ya wachezaji kama Betram Mombeki na Issa Rashind ambao walikuwa msaada mkubwa kwa timu, lakini tangu amefika Logarusic anaona wachezaji hao hawafai.
“Halafu huyu ni kocha gani ambaye hataki ushauri wa wasaidizi wake? Sasa wapo kwenye timu kwa ajili gani? Hata kwenye kufanya mabadiliko ukimwambia usimtoe huyu anasaidia timu, yeye anafanya anavyojua yeye, hakukuwa na maana basi awe na wasaidizi kumbe yeye mwenyewe anaweza kwanini alipewa wasaidizi,” alihoji mchezaji mwingine wa timu hiyo.
Aidha, wachezaji hao walisema ukata nao unachangia kuwashusha morali, kwani kwa sasa hawapati malipo yao inavyotakiwa na pia hakuna posho zozote kwao.
“Unajua timu hizi mara nyingine zinakuwa na watu wake wa karibu kusaidia, sasa Simba tulikuwa nao Friends of Simba hawa walikuwa wakiisaidia sana timu hata inapokuwa na shida kifedha, lakini wale sasa hawapo kwenye timu, mwisho hatumuoni kiongozi yeyote kuja hata kuzungumza nasi kambini na kusikiliza matatizo yetu,” alisema mchezaji mwingine.
“Sasa mwisho unakuta tupo kama mayatima, timu ikienda kucheza mikoani posho zetu zinachelewa, mara nyingine unatoka Morogoro unakwenda Tanga, mnafika huko ile posho ya Morogoro hamjalipwa wakati na sisi tuna familia zetu hivyo tunashindwa kutekeleza majukumu yetu,” alisema.
Gazeti hili lilimtafuta Mwenyekiti wa Simba, Ismail Rage azungumzie hilo, lakini alisema atafutwe Katibu Mkuu Ezekiel Kamwaga kwa vile yeye yupo bungeni Dodoma.
Hata hivyo Kamwaga hakupatikana kuzungumzia hilo baada ya simu yake ya mkononi kuita bila majibu, hali kama hiyo ilitokea kwa msemaji wa Simba Asha Muhaji ambaye simu yake haikupatikana karibu kutwa nzima ya jana.
>>>HABARI LEO

No comments:

Post a Comment