EBENEZA MARCH 9 2014

EBENEZA MARCH 9 2014

Friday, February 14, 2014

SERIKALI MBILI HAZIPINGIKI WARIOBA ASEMA


MWENYEKITI wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba, amesema muundo wa Muungano wa serikali mbili unawezekana, ilimradi kuwe na nchi moja.
Warioba alisema hayo jana katika mkutano ulioitishwa na Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD), kutafakari na kufikia maridhiano kuelekea Katiba mpya.
Mkutano huo ulishirikisha vyama vya siasa, viongozi wa dini, wa Bunge la Jamhuri ya Muungano na Baraza la Wawakilishi.
Alisema baada ya kuchambua maoni ya wananchi, waliona kuwa ili kuwepo muundo wa Muungano wa serikali mbili, ni lazima kuwe na mamlaka kamili ya kusimamia sehemu zote mbili, kuwe na nchi moja na kuondoa mgongano wa kikatiba.
“Kwa kuondoa mgongano wa kikatiba, ina maana ni lazima Katiba ya Zanzibar isitamke kuwa ni nchi yenye mamlaka kama ilivyo sasa,” alisema Jaji Warioba.
Hata hivyo, alibainisha kuwa mfumo wa serikali mbili umepitia vipindi tofauti tangu mwaka 1964 na hadi sasa, mamlaka ya Serikali ya Muungano Zanzibar yamekuwa yakipunguzwa kidogo kidogo, ndiyo maana walijikuta wakilazimika kuridhia Rasimu ya Katiba mpya, kuwa na mfumo wa Muungano wa serikali tatu.
Kwa mujibu wa Jaji Warioba, waasisi wa Muungano mwaka 1964, waliogopa kuwa na muundo wa Muungano wa serikali moja, kutokana na wasiwasi kwamba Zanzibar ingemezwa, lakini sasa wasiwasi huo ni mkubwa zaidi.
Aliongeza kuwa kati ya mwaka 1964 na 1977, kulikuwa na changamoto kubwa zaidi ya sasa za Muungano, lakini utashi wa kisiasa ulikuwa mkubwa na ndio ulisaidia kutatua changamoto hizo.
Wakati huo kwa mujibu wa Warioba, taasisi za Muungano ziliundwa na vyama vya Afro Shiraz (ASP) na Tanganyika African National Union (TANU) vilipoungana, Muungano ulikuwa mzito zaidi na mwaka 1977, ikaundwa Katiba ya Jamhuri ya Muungano kuunganisha nchi hizo.

“Kwa mara ya kwanza katika nchi hizi mbili, mtu alifanya kazi popote bila kujali anatoka upande gani wa Muungano,” alisema Jaji Warioba.
Aliongeza kuwa bahati mbaya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), ilivunjika mwaka 1977 na mambo ya nchi hizo katika Jumuiya, yaliingizwa kwenye Muungano.
“Kuna wakati tuliamua katika Sheria kutamka Tanzania Bara na Tanzania Visiwani, lakini baadaye tukasema utambulisho wa Zanzibar unapotea, tukasema iwe Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar ili kutenganisha. “Baada ya pale utaifa ulianza kujengeka, watu wa Bara hawataki kufanya kazi Zanzibar… ndipo yakatokea machafuko Zanzibar, msingi wake ulikuwa Serikali tatu,” alisema Jaji Warioba.
Serikali tatu
Alisema wakati wa kutafuta maoni, asilimia tano ya waliotoa maoni Bara, walitaka kusiwe na Muungano, asilimia 13 serikali moja, asilimia 24 serikali mbili na 61, serikali tatu.
Kwa upande wa Zanzibar, Jaji Warioba alisema asilimia 34, walitaka serikali mbili, 60 serikali ya mkataba, 23 serikali nne; yaani serikali ya Muungano, serikali ya Tanganyika, serikali ya Unguja na serikali ya Pemba.
“Hata sisi kwenye Tume tulikuwa kama ninyi, kuna wanaotaka serikali moja, wengine mbili, wengine tatu na mkataba, lakini hakuna aliyetaka serikali nne. Tulilazimika kuachana na mitazamo yetu na kuridhiana kwa kuja na mapendekezo ya serikali tatu,” alisema.
Kutokana na mchanganyiko huo maalumu, unaonesha kuwa hata Zanzibar hawataki serikali tatu, bali wengi wanataka serikali ya mkataba, walilazimika kuangalia katika sababu zao ambazo hata hivyo, hazikuwa mpya.
Sababu hizo kwa mujibu wa Jaji Warioba zilianza kusemwa miaka 30 iliyopita, kwamba Tanganyika imevaa koti la Muungano na pili, kuongeza mambo ya Muungano, ni kupunguza mamlaka ya Zanzibar na kwamba wamekuwa wakisema Zanzibar imepoteza uhuru wake.
Zanzibar kumezwa
Jaji Warioba alisema baada ya kufanya uchambuzi, walibaini kuwa Serikali ya Muungano imekuwa ikishughulika na mambo ya Tanganyika.
“Tuliangalia bajeti na kuchambua wizara zinazopewa kipaumbele, tukagundua ni za Tanganyika, tukaangalia maswali yenye mwelekeo wa uchumi tukakuta yanahoji kuhusu Tanganyika. “Hata kiongozi wa shughuli za Serikali bungeni ni Waziri Mkuu, hana ziara Zanzibar na Serikali ya Muungano haina mamlaka Zanzibar,” alisema Jaji Warioba.
Alifafanua kuwa hata walipoangalia kuhusu rasilimali, walibaini kuwa rasilimali za Serikali ya Muungano ni za Tanganyika na zinatumika kujenga Tanganyika.
“Sasa Zanzibar inafanya mambo ya kiuchumi kivyake na ikitaka rasilimali za nje lazima ipitie kwenye Muungano,” alifafanua.
Zanzibar yajitenga
Kwa mujibu wa Jaji Warioba, Zanzibar ilianza kujitenga taratibu na kutoa mfano wa mwaka 1984, ambapo Baraza la Wawakilishi lilitunga sheria ambayo inataka sheria zinazotungwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano, zisitumike Zanzibar bila kupitia Baraza hilo.
Pia Zanzibar ilitunga sheria kuwa kodi zitakazoidhinishwa na Bunge la Muungano, hazitatozwa Zanzibar mpaka zipitie Baraza la Wawakilishi.
“Sasa tuna utaratibu, sheria inatungwa na kusainiwa na Rais, lakini haitumiki Zanzibar,” alisema Warioba. Na kuongeza kuwa mwaka 1994, ilikubaliwa kuwa vifungu hivyo vifutwe, lakini utekelezaji haukufanyika. “Mwaka 2010, Zanzibar ilirekebisha Katiba yake na kutamka kuwa Zanzibar ni nchi … sasa huwezi kuwa na Katiba inatoa uhuru kwa sehemu moja (Zanzibar) na haitoi kwa sehemu nyingine (Tanganyika),” alifafanua. “Sasa Wabara wanahoji, Zanzibar wana kila kitu chao, kwa nini wanakuja huku kushiriki mambo ya Muungano…tukaona hii italeta mgogoro,” alisema Jaji Warioba.
Maafikiano serikali tatu
Jaji Warioba alisema baada ya kutafakari, wakabaini kuwa baadhi ya mambo yanaitwa ni ya Muungano lakini yalishaanza kuondolewa katika utekelezaji.
“Tulitafakari, je tunaweza kuyarudisha? Je, tunaweza kutunga Katiba iseme Zanzibar si nchi? Ikaonekana uwezekano wa kufanya hivyo ni mdogo tukafikia kuwa na serikali tatu, tushirikiane mambo ya Dola moja huru tu,” alisema.
Dk Bilal
Akifungua kongamano hilo la siku mbili, Makamu wa Rais, Dk Mohammed Gharib Bilal alitaka Wabunge wa Bunge Maalumu la Katiba kuongeza masuala ya afya na elimu kuwa ya Muungano.
“Badala ya kuyapunguza tuangalie uwezekano wa kuyaongeza, mfano afya, ambapo kila mtu anahitaji huduma bora za afya na elimu ili kuwa na mfumo sawa wa elimu kwa watoto wetu,” alisema.
Hata hivyo, maoni hayo yalitofautiana na ya Warioba, ambaye alisema kuongeza mambo ya Muungano ni sawa na kupoteza utambulisho wa Zanzibar.
Dk Bilal pia alikumbusha wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, kwamba kila jambo litaamuliwa kwa kura na wasiporidhika, wasubiri kura ya maoni ya wananchi.
Mtazamo huo pia ulitofautiana na wa Warioba, ambaye alitaka Bunge Maalumu la Katiba kupitisha Katiba hiyo kwa maridhiano na si kwa kupiga kura.
“Lazima Bunge likubaliane kwa maridhiano, mkipitisha Katiba kwa kura mjue kuwa siku moja baada ya kupitisha, itapingwa,” alisema.

No comments:

Post a Comment