MWANAMKE mkazi wa Kata ya Lubaga, Sophia
Haji (22) Manispaa ya Shinyanga anadaiwa kupigwa na mumewe na
kusababishiwa majeraha makubwa kwa kile kilichodaiwa alichelewa kupokea
simu ya mumewe.
Polisi inamsaka mwanamume huyo, Daniel
Daud ambaye kutokana na kipigo, mkewe alitokwa na damu nyingi sehemu za
siri. Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Shinyanga, Evarist Mangala alisema
wanamtafuta mtuhumiwa afikishwe kwenye vyombo vya sheria.
Kwa upande wake, mwanamke huyo
aliyelazwa Hospitali ya Mkoa Shinyanga, aliwaambia waandishi wa habari
kwamba alipigwa kutokana na kuchelewa kupokea simu ya mumewe wakati
akivuka ng’ambo ya barabara.
“Nilipofika nyumbani mume wangu alianza
kunipiga,” alisema. Alisema alijitetea kwa mumewe, lakini hawakuelewana,
na zaidi alimtuhumu kuwa ana uhusiano na mwanamume mwingine. Kwa mujibu
wa Sophia, mumewe alimfungia ndani siku mbili huku akiwa na majeraha
pamoja na kumnyima chakula.
"Mimi nilichelewa kupokea simu ya mume
wangu kwa sababu nilikuwa navuka barabara ili kujiepusha na ajali,
nilikuwa na wifi yangu mdogo, lakini nilivyofika nyumbani mume wangu
akawa mkali wala hakunielewa na kuanza kunipiga,” alisema.
Alisema wifi yake alimtetea, lakini
mumewe aliendeleza kipigo. Alisema baada ya kipigo hicho kuzidi, wifi
yake alipiga kelele na majirani walifika kuamua ugomvi huo.
Alisema ilipofika usiku, alihisi maumivu
makali mwilini akamweleza mumewe ambaye hakumsikiliza, zaidi ya
kumfungia ndani siku mbili. Anna Gilbert ambaye ni rafiki wa mwanamke
huyo, alisema baada ya kukaa siku mbili bila kumwona, siku ya tatu
aliamua kwenda nyumbani kwake na hakumkuta mumewe.
Alisema alisikia sauti ya mtu anayelia
ndani na alipochungulia, alimuona yuko mahututi na alichukua jukumu la
kumpeleka hospitali. Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Mkoa wa Shinyanga,
Dk Fredrick Mlekwa alikiri kumpokea mgojwa huyo.
Alisema alimfanyia matibabu katika vidonda vyake, ambavyo vilikuwa vinatoa usaha na alikuwa na majeraha sehemu za mapajani.
SOURCE: HABARI LEO
No comments:
Post a Comment