EBENEZA MARCH 9 2014

EBENEZA MARCH 9 2014

Thursday, January 16, 2014

Maandamano yaja kupinga bei ya umeme


MBUNGE WA JIMBO LA UBUNGO mh: JOHN MNYIKA
RAIS Jakaya Kikwete ameshauriwa katika mchakato wa mabadiliko ya Baraza la Mawaziri kumtaka Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo kujieleza kwake na umma ili kuwezesha hatua stahiki kuchukuliwa dhidi yake kutokana na ongezeko la bei ya umeme.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na Waziri Kivuli wa Nishati na Madini, John Mnyika (CHADEMA), Rais Kikwete anapaswa kutambua kuwa Waziri Muhongo alisema uongo kwa nyakati mbalimbali mwaka 2012 na 2013 alipowahakikishia  wananchi kuwa bei ya umeme haitapanda hata baada ya Shirika la Umeme Nchini (TANESCO) kuwasilisha mapendekezo ya kupandisha bei ya nishati hiyo.
Alisema kinyume na kauli za Prof. Muhongo, Bodi ya Wakurugenzi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura), katika kikao cha Desemba 10, mwaka jana, ilitoa maamuzi ya ongezeko la bei za umeme kwa viwango mbalimbali kwa makundi mbalimbali ya wateja, hatua ambayo itaongeza mzigo wa gharama za maisha kwa wananchi na itaathiri uchumi wa nchi.
Wakati Mnyika akisema hayo, wananchi wamependekeza kwamba iwapo mamlaka husika hazitapunguza kiwango cha ongezeko la bei ya umeme; maandamano yaandaliwe kuishinikiza serikali kuchukua hatua za haraka za kunusuru uchumi wa nchi na maisha ya wananchi kutokana na ongezeko hilo.
Mnyika ambaye ni mbunge wa Ubungo, alisema kuwa uamuzi wa kupandisha nishati hiyo ulifikiwa Oktoba 11, mwaka jana, baada ya TANESCO kuwasilisha maombi ya kurekebisha bei ya umeme kwa Ewura, iliyopendekeza kuongeza bei kwa asilimia 67.87 kuanzia  Oktoba 1, mwaka jana, asilimia 12.74 kuanzia Januari 1, mwaka huu na asilimia 9.17 kuanzia  Januari 1, mwaka 2015.

“Vilevile TANESCO waliomba kuidhinishwa kwa kanuni ya kurekebisha bei ya umeme kulingana na mabadiliko ya bei za mafuta, mfumko wa bei na mabadiliko ya thamani ya shilingi ya Kitanzania hatua ambazo nazo zina athari katika uchumi na maisha ya wananchi,” alisema.
Kuhusu wananchi kuandamana, alisema kuwa kutokana na ongezeko hilo aliomba kufikishiwa maoni ya wadau katika kipindi cha wiki moja juu ya athari za ongezeko hilo na hatua ambazo wananchi wanapendekeza zichukuliwe kurekebisha hali hiyo.
“Kabla ya kipindi hicho kumalizika tayari nimepokea maoni ya wananchi kutoka katika mikoa mbalimbali nchini. Hakuna mwananchi yeyote mpaka hivi sasa kati ya waliotuma maoni kwa njia ya barua pepe aliyeunga mkono ongezeko hilo la bei ya umeme,” alisema.
Mbunge huyo alisema kuwa wananchi hao wameelezea athari ambazo wameanza kuzipata huku wakipendekeza hatua ambazo zinapaswa kuchukuliwa kunusuru uchumi wa nchi na ongezeko la gharama za maisha linalotokana na ongezeko la bei ya umeme.
Alisema kuwa wananchi wamependekeza kwamba badala ya mamlaka kukimbilia kupandisha bei ya umeme ni muhimu kuchukua hatua za kupunguza mzigo mkubwa wa gharama za uzalishaji, usafirishaji na usambazaji wa umeme pamoja na uendeshaji wa sekta ya nishati.
SOURCE:CHADEMA BLOG

No comments:

Post a Comment