Morogoro. Kiongozi wa Taasisi
ya Kiislamu Tanzania, Sheikh Ponda Issa Ponda ameendelea kusota rumande
baada ya kesi yake kuahirishwa kwa mara nyingine kwa kuwa jalada la kesi
yake, halijarudi kutoka Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam
lilikoitishwa kwa ajili ya mapitio.
Kesi hiyo iliyofunguliwa katika Mahakama ya Hakimu
Mkazi Mfawidhi Mkoa wa Morogoro mwaka jana, iko mbele ya Hakimu
Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Mary Moyo na imekuwa ikitajwa kwa zaidi ya
miezi sita, huku Sheikh Ponda akiendelea kusota rumande baada ya
kunyimwa dhamana.
Sheikh Ponda anakabiliwa na mashtaka matatu ambayo
ni kutotii amri halali iliyotolewa na Mahakama ya Kisutu ya kutokutoa
maneno yenye kuharibu imani za dini na kushawishi watu kutenda kosa
ambayo anadaiwa kuyatenda Agosti 10, 2013 jioni katika eneo la Kiwanja
cha Ndege, Morogoro.
Jana, Sheikh Ponda alifikishwa mahakamani
akisindikizwa na polisi waliokuwa na silaha za moto na mabomu ya
machozi, huku wafuasi wake wakizuiwa nje ya uzio wa Mahakama hiyo kwa
sababu za kiusalama.
Mara baada ya kutajwa kwa kesi hiyo, Hakimu Moyo
alisema jalada la kesi hiyo, bado halijarudi kutoka Mahakama Kuu Kanda
ya Dar es Salaam, hivyo kuiahirisha kesi hiyo hadi Mei 26, mwaka huu
itakapotajwa tena.
Upande wa mashtaka uliwasilisha ombi mahakamani
hapo kutaka Sheikh Ponda kuhojiwa na polisi kuhusiana na mashtaka
yanayomkabili. Hakimu Moyo alikubali ombi hilo na kumtaka Sheikh Ponda
kuwa na imani na Mahakama hiyo, akisema itatenda haki kwa mujibu wa
sheria na si vinginevyo.
SOURCE>>>MWANANCHI
SOURCE>>>MWANANCHI
No comments:
Post a Comment