EBENEZA MARCH 9 2014
SWACO
royal
tt
NIMO
mvuto
Tuesday, April 22, 2014
KOCHA Mkuu wa Simba, Zdravko Logarusic alisema kilichoiponza timu hiyo kutofanya vizuri msimu huu ni kwa sababu ya wachezaji wengi wadogo wasio na nguvu na uzoefu, kiasi cha kushindwa kuibeba timu hiyo.
Akizungumza juzi Dar es Salaam, Logarusic aliyejiunga na Simba kwenye mzunguko wa pili wa Ligi Kuu mwaka jana, alisema alichogundua Simba ilisajili wachezaji wengi watoto, kwani asilimia kubwa ya walioko kwenye timu hawana uzoefu mkubwa. “Wachezaji wengi ni watoto hivyo wanacheza mpira, lakini sio kiushindani kama ambavyo nilitegemea. Mpira wao ni wa kawaida, lakini hawawezi kuibeba timu kwa vile hawana uzoefu wa kutosha,” alisema Logarusic ambaye ni raia wa Croatia.
Logarusic alitolea mfano wa wachezaji ambao ni wadogo kama Said Ndemla, Ramadhan Singano, Issa Rashid, Jonas Mkude na Haruna Chanongo, kuwa ni kweli wanacheza vizuri ila hawana uzoefu wa kutosha.
Alisema katika kikosi hicho alichokifundisha kwa takribani miezi mitano na nusu, ameona ni wachezaji wachache kama Donald Mosoti, Amisi Tambwe na Joseph Owino ndio wenye uwezo na uzoefu.
“Hao ndio wachezaji wenye uzoefu kidogo kwa sababu wamecheza kwa muda mrefu na wanalijua soka,” alisema kocha huyo akizungumzia wachezaji hao ambao wote ni wageni kutoka Kenya, Burundi na Uganda.
Aliongeza kuwa ili timu hiyo ifanikiwe kwa ajili ya msimu ujao, inahitajika kusajili wachezaji wazuri na wenye uzoefu wa kucheza soka la ushindani.
Pia aliutaka uongozi uwekeze kwa vijana wenye umri wa rika tofauti tofauti ili kutengeneza wachezaji wazuri na wenye nguvu kuanzia ngazi ya chini.
Alisema sio Simba peke yake iliyokuwa na wachezaji watoto pia, ameona katika Ashanti United na nyingine za ukanda wa Afrika Mashariki na wote soka lao hufanana kwani hucheza vizuri, lakini si soka la ushindani.
Kocha huyo aliyeiwezesha timu hiyo kumaliza msimu ikiwa katika nafasi ya nne na pointi 38, alisema anatarajiwa kuondoka Jumamosi ya wiki hii kwenda kwao kwa mapumziko.
Logarusic aliteuliwa kuinoa Simba pamoja na msaidizi wake, Selemani Matola, baada ya kufukuzwa kwa makocha Abdallah Kibadeni na msaidizi wake, Jamhuri Kihwelo ‘Julio.’
Kibadeni aliiacha Simba katika nafasi ya nne, nafasi ambayo ndio iliyomaliza Simba nyuma ya Mbeya City yenye pointi 49, Yanga katika nafasi ya pili na pointi 56 na mabingwa wapya, Azam FC kileleni na pointi 62.
Katika hatua nyingine, Uongozi wa Simba umesema kwamba unaendelea na mazungumzo na kocha Logarusic kuhusu ajira yake, ama kuongezewa mkataba au kuachana naye.
Kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa Simba, Ezekiel Kamwaga, ifikapo mwishoni mwa wiki hii, watakuwa wamefahamu kama kocha huyo ataendelea kuhudumu Msimbazi au atatupiwa virago vyake baada ya takribani miezi sita ya kuwanoa vijana hao.
SOURCE>>>HABARI LEO
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment