WAKATI Bunge Maalum la Katiba likisuasua katika kuunda kanuni za
kuongoza wajumbe wake, taarifa zinaonesha katika muundo uliopo wa
serikali mbili, mbali na kuimarisha umoja na mshikamano wa Taifa, pia
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), imekuwa ikinufaika nao
kiuchumi.
Taarifa hizo za kiuchumi, zinaungana na taarifa za kisiasa na kijamii
kusisitiza umuhimu wa muundo wa Muungano wa serikali mbili, tofauti na
wa serikali tatu uliopendekezwa na rasimu ya Katiba mpya,
zilizokwishatolewa na baadhi ya wasomi na viongozi mbalimbali katika
jamii.
Viongozi hao, akiwemo Askofu wa Kanisa Katoliki, Jimbo Kuu la Dar es
Salaam, Mwadhama Polycapy Kadinali Pengo na Profesa Bonaventura Rutinwa
wa Shule Kuu ya Sheria ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM),
wamebainisha kuwa umoja na mshikamano wa Watanzania unalindwa vizuri na
muundo wa serikali mbili, kuliko itakavyokuwa na serikali tatu.
Mhadhiri wa Uchumi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa
Hamphrey Moshi, katika sura aliyoandika katika kitabu cha Katiba Bora
Tanzania, amebainisha kuwa katika muundo uliopo, SMZ imekuwa ikipata
huduma za mambo ya Muungano bila kulipia, huku baadhi ya madeni yake
yakilipwa na Serikali ya Muungano tofauti na itakavyokuwa katika muundo
wa serikali tatu.
“Kama muundo huu (serikali tatu), utakubalika, SMZ lazima ijitegemee
katika kugharimia shughuli zake za kinchi na kwa kuwa Zanzibar itakuwa
sawa na Tanganyika, haitakuwa na maana Zanzibar kuacha kulipia ghama za
Muungano sawa na idadi yake ya watu,” amebainisha Profesa Moshi katika
kitabu hicho kilichochapishwa hivi karibuni.
Gharama za Muungano
Kwa mujibu wa Profesa Moshi, tangu kuasisiwa kwa Muungano, takwimu
zinaonesha SMZ imechangia gharama za shughuli za Muungano mara tatu tu.
Mara ya kwanza ilikuwa mwaka wa fedha 1964/1965, ambapo takwimu
zinaonesha kuwa gharama za mambo ya Muungano zilikuwa Sh milioni 107 na
SMZ ilichangia Sh milioni 10, sawa na asilimia tisa ya gharama za
uendeshaji.
Mwaka wa fedha 1965/1966, takwimu hizo zinaonesha gharama za mambo ya
Muungano ziliongezeka na kuwa Sh milioni 153, na mchango wa SMZ
uliongezeka na kufikia Sh milioni 12 ingawa tafsiri yake ni kwamba
mchango huo ulipungua na kuwa asilimia nane ya gharama hizo.
Takwimu za mwisho za mchango wa SMZ katika shughuli za Muungano,
zimetajwa kuwa ni za mwaka wa fedha 1966/1967, ambapo gharama zilikuwa
Sh milioni 176 na mchango wake ulipungua zaidi na kuwa Sh milioni 8.1,
sawa na asilimia tano ya gharama hizo.
Profesa Moshi amebainisha kuwa hakuna takwimu zaidi zinazoonesha
mchango wa SMZ katika shughuli za Muungano baada ya mwaka wa fedha
1966/1967, wakati gharama hizo zikiongezeka mara dufu.
Kwa mfano mwaka 2000 Bajeti ya mambo ya Muungano iliyotolewa na
Serikali ya Muungano, ambayo sasa inashutumiwa kuwa ni Serikali ya
Tanganyika iliyovaa koti la Muungano, imetajwa ilikuwa Sh bilioni 474
wakati mwaka 2006, mambo ya Muungano yalichukua Sh bilioni 556.1.
“Kwa wastani kwa miaka mitano kati ya 2005 mpaka 2010, Tanzania Bara
imekuwa ikitenga asilimia 22 ya Bajeti yake kugharamia shughuli za
Muungano.
Inaonesha kuwa Zanzibar imeshindwa kutoa mchango wowote katika miaka
hii mitano. “Pamoja na Zanzibar kuonekana kushindwa kuchangia gharama za
shughuli za Muungano, jambo ambalo linapingana na Ibara ya 133 ya
Katiba iliyopo, hakuna ushahidi kwamba SMZ imewahi kuitwa kujieleza
kwanini haitoi mchango wake,” ameeleza Profesa Moshi.
Jaribio la Kurekebisha
Kwa mujibu wa Profesa Moshi, mwaka 1977 Kamati ya Shelukindo,
ilitakiwa kupendekeza fomula ya haki na ya wazi ya mchango wa SMZ katika
gharama za uendeshaji wa shughuli za Muungano.
“Mapendekezo yalikuwa Zanzibar ilipe asilimia 3.9 ya matumizi yote ya
shughuli za Muungano. Hata hivyo, inavyoonekana hili halijawahi
kutekelezwa. “Mbali na Kamati ya Shelukindo, mapendekezo kama hayo
yalitolewa kwa mara nyingine ili kutatua kero hiyo na Tume ya Nyalali
(1992) na Tume ya Kisanga (1998),” amefafanua Profesa Moshi.
Hisa za Zanzibar
BoT Tofauti na ilivyo kwamba Zanzibar imekuwa ikishindwa kutoa
mchango wake katika gharama za Muungano, Serikali ya Muungano kupitia
Benki Kuu (BoT), imekuwa ikitoa gawiwo la hisa za Zanzibar kwa SMZ la
asilimia 4.5 kila mwaka.
Hisa hizo zinatokana na kuvunjika kwa iliyokuwa Jumuiya ya Afrika
Mashariki ambayo Zanzibar na Tanzania Bara zilikuwa nchi wanachama na
wanahisa katika Bodi ya Fedha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EACB).
Baada ya kuvunjika kwa Jumuiya, Zanzibar haikupata hisa zake asilimia
11.05, zilizokuwa zikionesha umiliki wake katika EACB na kugeuka kuwa
sehemu ya kero za Muungano.
“Hata hivyo mwaka 1994, Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF),
lilishauri Zanzibar ipate asilimia 4.5 ya gawiwo kutoka BoT,” ameeleza
Profesa Moshi.
Kiwango hicho cha gawiwo kimekokotolewa kwa kuzingatia sehemu ambayo
Zanzibar inachangia katika uchumi wa Tanzania na idadi ya Watanzania,
ambayo ni wastani wa asilimia tatu.Profesa Moshi amebainisha kuwa tangu
1995, SMZ imekuwa ikipata gawiwo hilo kutoka BoT.
Madeni
Profesa Moshi ameeleza kuwa uwezo wa SMZ kukopa ni mdogo, kwa kuwa
Waziri wa Fedha katika Serikali ya Jamhuri ya Muungano, ndiye mwenye
mamlaka ya kukopa kwa niaba ya serikali zote.
“Hii maana yake ni kwamba SMZ, haina mamlaka ya kutafuta mkopo kwa
ajili ya matumizi yake na kama inataka mkopo, lazima iombe kupitia
Serikali ya Jamhuri ya Muungano. “Serikali ya Jamhuri ya Muungano baada
ya kupokea maombi ya Zanzibar, itaomba mkopo kutoka nje na ikifanikiwa,
itatoa sehemu ya mkopo huo iliyoombwa na Zanzibar na kuipa SMZ,”
ameeleza Profesa Moshi.
Ameeleza kuwa kwa juu juu, inaonekana kuwa Zanzibar inaumizwa
kiuchumi, lakini uchambuzi wa ndani unaonesha namna SMZ inavyonufaika
katika mfumo huo.
Yasiyolipika
Kwa mujibu wa Profesa Moshi, kwa kuwa mikopo ya Zanzibar inadhaminiwa
na Serikali ya Jamhuri ya Muungano, mpaka mwaka 2002 utaratibu ulikuwa
SMZ ikishindwa kulipa deni, linalipwa Serikali ya Muungano kwa niaba ya
SMZ.
Kuanzia mwaka wa fedha 2001/2002, Profesa Moshi amebainisha kuwa SMZ
imekuwa ikiruhusiwa kukopa kwa kuuza hati fungani kupitia BoT.
Hata hivyo kwa mujibu wa Profesa Moshi, BoT ililazimika kuunda
akaunti maalumu, ili SMZ iliposhindwa kulipa deni, benki hiyo ilipe na
kukata katika gawiwo ambalo linapaswa kutolewa kwa SMZ.
Pamoja na madeni hayo ya kiserikali, Zanzibar pia imetajwa kuwa na
madeni makubwa ya kibiashara, likiwemo la Shirika la Umeme (Tanesco) kwa
Shirika la Petroli Zanzibar (ZSFPC).
“Ingawa ZSFPC imeandaa mpango wa kulipa deni lake kwa Tanesco kwa
miaka 15 mpaka 2018/19, uzoefu wa nyuma unaonesha kuwa Serikali ya
Muungano huenda ndiyo itakayolipa deni hilo,” ameeleza Profesa Mushi.
Maoni CUF
Akizungumzia uchambuzi huo wa Profesa Moshi, Naibu Katibu Mkuu wa CUF
Zanzibar, Julius Mtatiro, alisema uchambuzi huo si wa kweli na mfumo wa
serikali mbili unaonesha Tanganyika inajikomba kwa Zanzibar.
Alitoa mfano wa Sekta ya Utalii, kwamba kungekuwa na muundo mzuri wa
Muungano, Zanzibar wangekuwa na ushirikiano na nchi za kimataifa na
kufanya mambo makubwa.
“Tuwaachie walipe polisi wao wenyewe, wanajeshi wao wenyewe wataweza
kwa kuwa wao ni wachache…Tume mbalimbali zimeundwa zimeshauri serikali
tatu, hata Tume ya Mabadiliko ya Katiba ina wazalendo waliofunzwa na
Mwalimu Nyerere, wameona hilo,” alisema Mtatiro.
Alisema ndio maana Katiba ya Zanzibar imeonesha kutangulia kutoka
uhuru wake, lakini Tanzania Bara imekuwa iking’ang’ania Zanzibar kuwa ni
sehemu ya Tanzania,” alisema.
No comments:
Post a Comment