Kamanda wa Polisi Mkoani Kagera,George Mayunga.
Kamanda wa Polisi Mkoani Kagera, George Mayunga, amesema Mchungaji huyo, alikamatwa kwa tuhuma za kutoa mahubiri ya kichochezi kanisani na kusababisha nyumba tatu pamoja na migomba kuharibiwa.
Alisema Mchungaji huyo anashikiliwa kwa tuhuma za kuchochea vurugu, kudhuru miili na kuharibu mali kinyume cha sheria.
Alisema katika mahubiri yake hayo, Mchungaji huyo aliwataja kwa majina wamiliki wa nyumba na mazao hayo akidai kuwa ni wachawi, jambo lililowatia hasira wananchi na kwenda kuharibu nyumba zao na mazao.
Kutokana na hali hiyo, shirika lisilo la kiserikali linalotoa huduma kwa wazee na watoto yatima la `Kwa Wazee', limewachukua waathirika wa tukio hilo na kuwahifadhi katika nyumba maalum ili kunusuru maisha yao.
Kamanda Mayunga, aliongeza kusema kuwa mbali ya Mchungaji huyo, pia watu wengine watatu wanashikiliwa polisi kwa tuhuma kama hizo na kwamba uchunguzi wa jeshi hilo umebaini baadhi ya wananchi wakiwamo ndugu wa watuhumiwa hao walifanya ukatili huo muda mfupi baada ya kuhubiriwa na Mchungaji huyo.
NIPASHE baada ya kuzungumza na wananchi waliotuhumiwa kwa ushirikina, Fabian Albert na mkewe Gaudensia Fabian, walisema chanzo cha tukio hilo ni watoto wao kutaka kurithi mashamba mapema na kwamba walikuwa wakitaka kuuza ardhi ya wazazi wao na walipozuiliwa walikuwa wakiwatishia kuwaua.
Walikanusha kujihusisha na vitendo vya kishirikina huku wakidai kuwa ni mpango ulioundwa siku nyingi na hata walipokuwa wakienda kwa viongozi wa serikali ya kijiji hicho kutoa taarifa walikuwa wakifukuzwa na kuelezwa kumtafuta diwani wa kata hiyo au kwenda polisi.
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment