JUZI
USIKU, ‘Albiceleste’, kama inavyojulikana Timu ya Taifa ya Argentina,
ilitoka Sare 0-0 na Romania, Timu ambayo haipo Fainali za Kombe la
Dunia, na kuonyesha dhahiri ubutu wao lakini Kocha wa Nchi hiyo hataki
kusikia lolote kuhusu Carlos Tevez ambae sasa ni Supastaa huko Serie A
akivurumisha Mibao kila kukicha akiwa na Klabu yake Juventus.
Kocha wa Argentina, Alejandro Sabella,
amekataa kabisa kusikiza hoja yoyote ya kumwita Carlos Tevez kuichezea
Nchi yake licha ya Nchi hiyo kuonyesha waziwazi wana ubutu kwenye Fowadi
yao hasa baada ya kufifia Fowadi yao ya kina Lionel Messi, ambae kwenye
Mechi hiyo na Romania alikuwa akitapika Uwanjani, huku Sergio Aguero,
Gonzalo Higuain, Rodrigo Palacio na Ezequiel Lavezzi wakiwa ni magoigoi
tu.
Akiwa na Juve Msimu huu, Carlos Tevez
ametoboa nyavu mara 15 na anaonyesha ni mpiganaji hodari lakini
Alejandro Sabella hataki kusikiza lolote.
Alipohojiwa kuhusu Tevez, Alejandro
Sabella, alijibu: “Nina imani na Wachezaji wangu na nawaamini Mastraika
wangu. Wote ni Nyota wa Argentina. Sitaki kuzungumzia Mchezaji yeyote
ambae hayuko hapa.”
Tevez, mwenye Miaka 29, hajaitwa Timu ya Taifa ya Argentina tangu Kocha Alejandro Sabella ateuliwe wadhifa huo Agosti 2011.
Mwezi Desemba Tevez aliwahi kutamka:
“Kama Sabella hajaniita siwezi kumpigia Simu na kumuuliza kwanini
hakunichagua. Sabella asiombwe kunichukua…mwacheni afanye kazi yake kwa
amani kwa sababu si rahisi Sabella kuniacha mimi. Najua ipo presha kubwa
toka kwa Mashabiki.”
Tevez, ambae amewahi kuzichezea Klabu za
England za Manchester City, Manchester United na West Ham, amesema yeye
ana uhusiano mzuri na Wachezaji wa Timu ya Taifa ya Argentina pamoja na
Nahodha wake Lionel Messi.
Tevez alisema: “Sina tatizo na kundi
lile na naelewana vizuri mno na Messi. Sipotezi usingizi kwa sababu ya
Kombe la Dunia. Sidhani kama nitaitazama kwa sababu inauma kuiona Timu
ya Taifa, ni mbaya kwangu!”
Mara ya mwisho kwa Tevez kuichezea
Argentina ni kwenye Robo Fainali ya Copa America ya Mwaka 2011 ambapo
Argentina ilifungwa na Uruguay.
Pia Tevez alikuwemo Kikosi cha Argentina
kilichocheza Fainali za Kombe la Dunia za Mwaka 2006 huko Germany na
Afrika Kusini 2010 ambako mara zote ilitolewa Robo Fainali.
Argentina, ambao wametwaa Kombe la Dunia
Mwaka 1978 na 1986, kwenye Fainali za Kombe la Dunia za Brazil Mwakani
wapo Kundi F pamoja na Bosnia, Iran na Nigeria.
No comments:
Post a Comment