0
Dar es Salaam. Utafiti
uliofanywa na Taasisi ya Utafiti wa Uchumi na Jamii (ESRF), umebaini
asilimia 33.4 ya Watanzania wameghubikwa na umaskini uliokithiri jambo
linalosababisha vifo, msongo wa mawazo, afya duni na utegemezi.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa Kituo cha Redio
cha Maendeleo kwa ajili ya kutoa taarifa za maendeleo kwa umma
iliyozinduliwa na ESRF jana, Mhadhiri wa Uchumi wa Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam, Dk Oswald Mashindano alisema Watanzania wengi wanakabiliwa na
umaskini uliokithiri kwa sababu ya kukosa nyenzo, mitaji na uwezo wa
kuzalisha.
“Umaskini uliokithiri au umaskini sugu, hautumii
kigezo cha kipato cha chini pekee lakini yapo matatizo yanayowakabili
Watanzania muda mrefu na hayajapatiwa ufumbuzi,” alisema Dk Mashindano.
Alisema mtu anayeshindwa kuyatatua matatizo haya
hushindwa kumudu huduma muhimu kama maji, afya, elimu na kuongeza kuwa
ni umaskini wa maisha yote kwa baadhi ya watu na huendelea kizazi hata
kizazi.
“Utafiti wetu ulitumia kipimo cha kimataifa cha
kuangalia umaskini uliokithiri kwenye nchi zinazoendelea (Multi
dimensional Poverty Index),” alisema Dk Mashindano.
Aliongeza kuwa umaskini huo ni sugu kwa sababu
tangu Tanzania ipate uhuru, Serikali imeshindwa kuuondoa na asilimia
kubwa ya Watanzania wameghubikwa na hali hiyo.
Akizindua studio hiyo, Mkurugenzi wa Idara ya
Kuondoa Umaskini wa Wizara ya Fedha, Anna Mwasha aliwapongeza ESRF kwa
kuzindua studio hiyo ambayo itakuwa daraja muhimu kati ya wananchi na
Serikali. Mwasha alisema lengo la kuanzisha kituo hicho ni kuboresha
uaandaji na utoaji wa taarifa.
“Ni wakati ambao taarifa nyepesi zinazohitajiwa
ziwafikie wanajamii kwa sababu matarajio ya Serikali ni kuona
zinawafikia watu kwa urahisi ili kuondoa huo umaskini sugu,” alisema
Mwasha.
Pia, Mwasha alisema kituo hicho kikitumiwa vyema
kitasaidia kuondoa umaskini sugu miongoni mwa Watanzania asilimia 33.4
waliotajwa kwenye utafiti huo wa ESRF.
Mkurugenzi wa ESRF, Dk Bohela Lunogelo alisema
kituo hicho cha redio kitaandaa vipindi vya maendeleo kama kilimo, elimu
na afya kwa kutumia vyanzo vya habari kama Taasisi ya Utafiti wa Tiba,
(NIMR), Chuo cha Kilimo, (Sua) na tafiti zinazofanywa ndani ya nchi.
Taarifa hiyo imekuwa ikifanya utafiti mbalimbali nchini.
SUORCE:MWANANCHI
No comments:
Post a Comment