Mwanza. Waziri Mkuu Mstaafu,
Frederick Sumaye ameonya kuwa iwapo kutakosekana mipango ya kuimarisha
hali ya uchumi wa nchi , Taifa linaweza kujikuta likitumbukia kwenye
janga la mifarakano kutokana na vijana wengi kukabiliwa na tatizo la
ukosefu wa ajira.
Akizungumza kwenye kongamano
lililoandaliwa na Chuo cha Biashara (CBE) Mwanza, Sumaye alisema pamoja
na kwamba tatizo la ajira ni janga linaloendelea kuzikabili nchi nyingi
duniani ikiwamo Tanzania, Serikali inapaswa kuweka mikakati ya dhati
kukabiliana na hali hiyo.
Kongamano hilo lililohudhuriwa na jumuiya ya chuo
hicho na wananchi, lilijadili mada iliyopewa jina la “Maendeleo ya
Vijana na Tatizo la Ajira”.
Sumaye alisema inawezekana kukawa na njia za
kurekebisha hali hiyo, lakini jambo kubwa linalopaswa kuzingatiwa na
serikali ni kuwa na mikakati ya ujenzi na ukuzaji uchumi imara.
“Uchumi dhaifu huzaa nchi maskini ambayo watu wake
huishi katika mazingira magumu na serikali husika haiwezi kuwa na uwezo
wa kutoa huduma muhimu kwa watu wake kwa viwango vinavyotakikana’
Alisema.
Alisema uchumi dhaifu pia huweza kuhatarisha
usalama wa nchi kwa kuwa ni rahisi kusababisha mifarakano na wananchi
kuichukia serikali yao.
Alisema kuwa kumekuwa na jitihada mbalimbali za
kuwakwamua vijana ili kuondokana na hali duni za maisha, lakini jambo
linalopaswa kuzingitiwa sasa ni kutoa elimu kwa vijana hao pamoja na
wananchi kwa ujumla ili waweza kukabiliana na changamoto zinawazunguka.
“Suala uelimishaji wa wananchi hasa vijana
wanaokua ni la msingi katika kujenga uchumi utakaomudu ushindani katika
nyanja mbali mbali za sayansi na teknologia na biashara za kimataifa.
Nchi nyingi zilizopata maendeleo ya haraka
ziliwekeza katika elimu yenye malengo hasa katika eneo la sayansi na
teknolojia. Tukiamua kuwekeza katika elimu isiwe bora elimu bali
tuhakikishe tunatoa elimu ya viwango vinavyokubalika na siyo elimu ya
kujitafutia sifa isiyo na viwango” alisema.
Pia alihimiza haja ya kuendelea kuwepo ushirikiano
wa karibu baina ya serikali na sekta binafsi akisema kuwa pasipo kuwepo
hali hiyo suala la kuwa na uchumi endelevu linaweza kuwa ndoto kutokana
na kila upande kuwa ni mchango mkubwa wa uendelezaji wa jamii.
source: mwananchi
source: mwananchi
No comments:
Post a Comment