WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu
anayeshughulikia Sera, Uratibu na Bunge, William Lukuvi jana alitembelea
ukumbi wa Bunge maalum la Katiba, linalotarajia kuanza Februari 18,
mwaka huu na kujiridhisha na marekebisho ambayo yamefanyika.
Akizungumza na waandishi wa habari, Lukuvi alisema viti 676 vimeshafungwa pamoja vipaza sauti vyake.
Alisema maeneo kwa ajili ya chakula kwa
wajumbe tayari yamekamilika, ofisi za viongozi wakiwemo Mwenyekiti na
Makamu Mwenyekiti watakaoteuliwa tayari pamoja na kumbi nyingine ndogo.
Lukuvi alisema Ofisi ya Bunge
imeshatafuta kumbi nyingine nje ya Bunge, kwa ajili ya kufanyika
mikutano itakayohitaji wajumbe wengi.
"Maandalizi ya msingi sasa
yameshakamilika, kilichobaki Katibu wa Bunge na Naibu wake ambaye ni
Katibu wa Baraza la Wawakilishi watangaze siku ya kuja," alisema Lukuvi.
Hata hivyo, alisema wabunge wote watatakiwa kuwepo Dodoma kabla ya Februari 18, siku ambayo vikao vya bunge hilo vinaanza.
"Siku moja kabla ya vikao kuanza,
wabunge wataitwa katika ukumbi huu kupewa maelekezo ya jinsi ya kukaa na
jinsi ya kutumia vifaa vilivyomo ikiwemo vipaza sauti," alisema Lukuvi
Februari mosi mwaka huu Rais Jakaya Kikwete alitembelea na kukagua
ukumbi huo, kuona maandalizi yanavyoendelea na aliahidiwa kuwa Februari
10 maandalizi yote ya uwekaji viti na vipaza sauti, yangekuwa
yamekamilika.
Katika hatua nyingine, Katibu Mkuu wa
Chama cha Wananchi (CUF), Seif Sharif Hamad ametaka wajumbe wa Bunge la
Katiba kutoka Zanzibar, kuweka maslahi ya taifa mbele na kuachana na
ushabiki wa kisiasa.
Alisema hayo Chake Chake Pemba wakati
akihutubia wananchi na wafuasi wa chama katika mkutano wa hadhara.
Alisema wajumbe hao wamebeba majukumu makubwa ya hoja mbali mbali za
kunufaisha Zanzibar katika mchakato wa mabadiliko ya Katiba.
“Mchakato wa kupata wajumbe wa Bunge la
Katiba sasa umekamilika ambapo wajumbe wanatakiwa sasa kuweka maslahi ya
taifa mbele na sio ushabiki wa vyama vya siasa,” alisema.
Wakati huo huo Kamati Kuu ya Chama cha
Sauti ya Umma (SAU) imempongeza Rais Jakaya Kikwete anavyoendesha
mchakato wa mabadiliko ya Katiba kwa uhuru na uwazi. Mkurugenzi wa
Uenezi na Uchaguzi Taifa wa SAU, Johnson Mwangosi alisema jana
wanajivunia kuwa na Rais Kikwete .
Alisema bila kujali itikadi za kisiasa, alikaa na viongozi wa vyama vya siasa kitendo ambacho ni cha kiungwana.
Aidha kamati hiyo imesema inaamini
itawakilishwa vizuri kupitia wawakilishi wake, Yusuph Manyanga na Bether
Mpata kwenye bunge hilo.
Habari hii imeandikwa na Sifa Lubasi, Dodoma, Khatib Suleiman, Zanzibar na Hellen Mlacky, Dar.
No comments:
Post a Comment